Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Shambulio la treni Nigeria: 'Jinsi nilivyonusurika kutekwa na kuzuiliwa'
Na Halima Umar Saleh
BBC News Hausa, Abuja
Kurejeshwa tena kwa usafiri wa treni ya mwendo kasi nchini Nigeria miezi tisa baada ya tukio la utekaji nyara wa kidhalimu kunarejesha kumbukumbu za kiwewe miongoni mwa baadhi ya manusura, ambao wanatatizika kupona kutokana na masaibu waliyopitia katika mkasa huo.
Watu wenye silaha walichimba njia kati ya mji mkuu, Abuja, na mji wa kaskazini wa Kaduna jioni ya tarehe 28 Machi, na kulazimisha treni iliyobeba abiria 362 kusimama.
Risasi zilipigwa kutoka pande zote huku washambuliaji wakiizingira treni hiyo, iliyokuwa na polisi waliokuwa wamejihami na kufanikiwa kuwateka nyara abiria 62. Takriban watu tisa walifariki katika shambulio hilo hayo.
Miongoni mwa wale waliotekwa nyara alikuwa Hassan Usman, wakili anayeishi Kaduna, na mkewe.
Aliambia BBC kwamba kundi la watu waliotekwa nyara - wanaume 39, wanawake 18 na watoto watano - walilazimika kusafiri kwa siku nne hadi eneo la mbali ambako walipaswa kuzuiliwa, wakitembea kwenye jua kali bila chakula na kupewa maji ya kunywa mara kwa mara
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 47 alikua msemaji mkuu wa mateka hao ambao baadhi yao walizuiliwa kwa miezi mitano na tangu wakati huo ameanzisha kundi la WhatsApp kwa ajili ya manusura hao ili waweze kupeana faraja na kusaidiana.
Ukimuona wakili huyo aliyevalia nadhifu, ni vigumu kuamini ndiye mwanamume aliyejawa na mvi kichwani ambaye aliomba serikali isikilize matakwa ya watekaji nyara huku mateka wengine kando yake wakichapwa viboko kwenye video iliyotolewa Julai na wapiganaji hao.
Anasema ilikuwa ni hali ya kutisha kwa wafungwa wote lakini walioathirika zaidi ni wanawake ambao walilazimika kukabiliana na mazingira chafu.
Hawakuwa na taulo za hedhi na walilazimika kutumia vitambaa. Wote walikunywa maji kutoka kwenye ziwa dogo lililokuwa karibu ambako waliruhusiwa pia kuoga.
"Katika miezi michache ya kwanza, tulikuwa tukilala nje hadharani ardhi wakati mwingine kuna unyevu unyevu, lakini mvua ilipoanza kunyesha waliweka kambi za muda na kuturuhusu kuingia ndani hadi mvua ilipoisha," alisema Bw Usman.
Mateka walikula mara moja kwa siku saa 11:00 - kwa kawaida supu iliyotengenezwa na unga wa mahindi na majani ya mbuyu
"Tuligundua kuwa vyakula hivyo vilikuwa vikiingizwa kinyemela na kupata mahitaji ni shida, mara kwa mara walileta mchele ambao tuliupika kwa kutumia mafuta ta mawese tu na wakati mwingine maharage," alisema.
Kulikuwa na siku ambapo walipewa chakula cha pili saa kumi na mbili jioni, lakini hii ilikuwa nadra.
"Wanawake walipika na wanaume walifanya kazi nyingine kama vile kuchota maji, kuni na kuosha vyombo."
'Boko Haram walitushawishi tuungane nao'
Kwa wiki kadhaa, utambulisho wa watekaji nyara haukujulikana - huku kukiwa na uvumi kwamba walikuwa wanachama wa vikundi vya majambazi maarufu kwa utekaji nyara kwa ajili ya fidia kaskazini-magharibi.
Lakini Bw Usman alithibitisha kuongezeka kwa tuhuma kwamba watu hao wenye silaha walikuwa wanachama wa kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram ambalo kwa kawaida huendesha harakati zake kaskazini-mashariki ambapo walianza uasi mwaka 2009.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mapendekezo kwamba kundi hilo, ambalo linasema linataka kupindua serikali na kuanzisha taifa la Kiislamu, linapanuka kuelekea kusini.
"Walituambia kuwa wao ni Boko Haram na walitukamata ili kushinikiza baadhi ya matakwa yao kutoka kwa serikali.
"Wakati mwingine walitupa simu zao ili kusikiliza mengi ya wanayohubiri," alisema, akifafanua haya ni pamoja na mahubiri kutoka kwa viongozi wawili wa kwanza wa Boko Haram Mohammed Yusuf na Abubakar Shekau - ambao wote wamekufa.
"Walijaribu hata kutushawishi kujiunga na kikundi chao na kueneza sababu yao." Wakati wowote wa mateka walipougua au kuhitaji dawa, wapiganaji wangetafuta ushauri.
"Kila mara wangeuliza wataalamu miongoni mwetu, dawa zinazohitajika kutibu watu na mara nyingi walinunua [yao]," wakili alisema.
"Madaktari wao wachanga pia waliwadunga wagonjwa sindano hasa kwa matibabu ya malaria na homa ya matumbo."
Wakati mmoja, kiongozi wa watekaji hao alipendekeza awapeleke mateka wachanga nyumbani kwake kwa uangalizi bora, lakini wazazi walikataa, Bw Usman alisema.
'Maskini baada ya kulipa fidia'
Wakati baadhi ya wahasiriwa wa shambulio la treni waliachiliwa baada ya familia zao na washirika kulipa fidia kubwa, watekaji nyara hao walishikilia wengine kutoa matakwa ya serikali.
Baadhi ya wachambuzi wanasema hii inaweza kuwa ni pamoja na kuachiliwa kwa wanamgambo waliokuwa gerezani - ingawa hili halijawahi kuthibitishwa.
Bw Usman alisema familia yake ilijadiliana kuachiliwa kwake na wanamgambo hao – lakini hawajawahi kupewa maelezo ya makubaliano hayo.
Anachojua ni kwamba haukuwa utaratibu wa moja kwa moja na siku ambayo alitakiwa kuachiliwa mambo hayakuenda kama ilivyopangwa .
"Askari waliokuwa wakishika doria kwenye walikataa kuwaruhusu watu wangu kufika eneo la kunichukua."
Hii iliwafanya wapiganaji kutengeneza video ya mateso na aliachiliwa tu siku iliyofuata.
Baada ya kulipa fidia baadhi ya familia ziliachwa na umaskini - alisema kila amateka aliyeachiliwa huru alitozwa naira milioni 100 sawa na dola 225,000 za Kimarekeni.
Kwenye kikundi cha WhatsApp, ambapo walionusurika sasa wanachukuliana kama familia mojailiyoungana, wahanga hao wanasimulia hali zao mbaya.
“Wengi hawawezi kumudu milo mitatu kwa siku, wengine walipewa notisi ya kuondoka na wenye nyumba zao,” alisema Bw Usman.
Wakili huyo alisikitika kwa kukosa usaidizi uliotolewa kwa walionusurika, ambao wengine wao wanahitaji matibabu ya kiwewe.