Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: 'Mruhusu mtoto asomee anachokitaka'
“Mimi ni miongoni mwa waanzilishi wa kundi la sanaa la Parapanda, ambalo lilipata tuzo na kutambulika sana hapa nyumbani Tanzania lakini tulipata safari nyingi za Afrika na nje ya bara, mfano moja ni ya New York, Marekani”.
Huyo ni Dkt. Mona Mwakalinga (56), msomi aliyebobea kwenye tasnia ya Sanaa bunifu nchini Tanzania na mhadhiri katika chuo kikuu cha Dar es Salaam ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC).
Kwake mafanikio anayatafsiri kupitia uwezo wake wa kufungulia wengine fursa kuonesha ujuzi ama kipaji.
“Furaha yangu hutimia pale ninapoona nimefanikiwa kuinua vipaji vya wengine, kwa kutoa fursa kwa mtu mwingine kuonesha uwezo wake’’
Anasema kauli mbiu yake ni moja kama naweza kusaidia, nafanya kweli, hasa katika kazi za sanaa jambo ambalo analihusudu sana katika maisha yake.
Msukumo wa kuwa hivi aliupata kutoka kwa baba yake mzazi tangu akiwa binti mdogo. Anasema pamoja na msisitizo wa kuzingatia elimu, baba yake mzazi alimuhimiza sana kufanya kazi kwa nguvu na kwa uwezo wake wote bila kujali ukubwa au udogo wa kazi husika.
‘Baba yangu mzazi alikuwa mchungaji alipenda sana kujitolea, nadhani hii tabia nimeitoa kwake. Alikuwa anajitolea hadi tunamwambia sasa baba umepitiliza, lakini kuhusu sanaa nilijikuta tu napenda sana kuimba, nilimpenda sana Michael Jackson lakini nikagundua sauti sina lakini sanaa naipenda nikahamia sanaa za maonesho.’ Anaeleza Mona.
Safari yake kielimu
“Disemba mosi mwaka 1968, mama yangu alinizaa akiwa safarini kutoka Mwakaleli, Mbeya kuelekea Arusha, labda ndiyo maana mimi ni kiguu na njia’’anaelezea Dkt. Mona huku akiangua kicheko.
“Nilipoongeza kimo kidogo baadaye kabla sijamaliza shule ya msingi nilipata bahati ya kwenda Urusi kwa miaka mitatu na shangazi na baadaye Marekani ambako nilimaliza high school. Baada ya hapo nilijiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam na kusomea shahada ya kwanza ya michezo ya jukwaani Theatre art”.
“Nina mambo mengi, napenda kutambulika kama Mwalimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sanaa Bunifu, mimi ni mtu mwenye marafiki wengi, napenda kucheka, sitaki mawazo kabisa, anamalizia kwa kicheko.
Anaongeza: Nilikutana na watu wengi chuoni, lakini kikubwa nilikutana na mume wangu hapo chuo kikuu.
Maisha ya ndoa
“Ninafurahia sana nina miaka 25 ya ndoa hadi sasa.Mimi ninajijua niko muwazi sana, na siogopi kuongea, hivyo, haikuwa ngumu siku nilipomwona huyu ambaye sasa ni mume wangu, alikuwa nje ya nyumba yake anapika, nilipenda sana nikasema huyu tunaweza kuendana kabisa kama anaweza kufanya shughuli zake za nyumbani mwenyewe. Mume wangu amekuwa rafiki yangu tunapendana na kusaidiana sana katika shughuli zetu za kila siku’’anasimulia Dkt. Mona”
Sanaa ni Maisha
Anaeleza vijana sasa hivi wanapaswa kuangalia na kujifunza ili kuweza kufanya sanaa kama nyenzo ya kupata fedha kwa kupitia mitandao kama Instagram na Facebook.
Anaongeza: “Tujifunze kwa mataifa kama Marekani, sanaa ni kitu cha pili kwa kuwaingizia mapato. Sanaa bunifu ni fursa, inafurahisha sasa hivi kuona watu wanafanya sanaa na kupata fedha tofauti na enzi zetu tulifanya na kufurahia tu kuonesha kipaji basi.
Anafafanua kuwa sanaa ni kipaji na taaluma, ni muhimu sana kupata mafunzo ili kufanya kazi za sanaa kwa kuzingatia weledi.
Changamoto kutokana na mitazamo ya kijamii
Mwanzoni watu walikuwa wanakushangaa kabisa kwa nini ukasomee sanaa
Baadhi ya watu hawakuona kama sanaa inaweza kumpa mtu maisha.
Dokta Mona anakumbuka kipindi ambacho sanaa haikuonekana kama kazi.Wasanii walifanya kwa kujitolea tu.
“Watu wanakuita wanakwambia haya njoo tukakutangaze, hawawazi utakula nini”
Wengine wanakwambia tutakupa kitu kidogo tu kama nauli ya usafiri lakini tunajiuliza hivi wakienda kwa wanasheria wanalipia fedha za kutosha ili kupata sahihi au muhuri mbona wanaiheshimu?
Anaitaka jamii kuelewa kwamba sanaa nayo ni kazi inayohitaji kuheshimiwa na kutengewa muda kujifunza kwani kipaji pekee hakitoshi.
Kila mtu alinishangaa nyumbani kwa nini nimechagua masomo ya sanaa, mama yangu aliniunga mkono na kusema ni vizuri niachwe nisome ninachopenda, ushauri ambao baba aliuafiki.
“Mruhusu mtoto afanye kile anachokitaka kwa sababu akifanya vibaya hatakulaumu kuliko ukimchagulia wewe”
Hata sasa na mimi ninaamini katika kumruhusu mtoto kuchagua kusoma kile anachopenda na anachoona kiko ndani ya uwezo wake.
Sasa hivi teknolojia imesaidia sana kupitia mitandao imetoa nafasi kwa watu kubadilishana ujuzi na kujengeana uwezo pia.
Mfano kwa Tanzania sanaa ya muziki kwa sasa imeliweka jina la Tanzania katika ramani ya kimataifa,ni jambo linalotia moyo sana.
Tukiangalia lugha ya Kiswahili sasa hivi inatupeperusha mno duniani hasa ukizingatia Umoja wa Mataifa na hata Afrika kuipa hadhi na heshima duniani.
Ushauri kwa watoto wa kike
Mtoto wa kike kwanza ajiamini, afanye kazi kwa weledi na atafute anachokitaka.
Ni vizuri kutokubali kukatishwa tamaa. Pale unapokataliwa ama kuvunjwa moyo ndiyo wakati haswa wa kuinuka na kupamabana ili kuonesha uwezo uliokuwa nao. Mtu akikukatalia kitu, iwe chachu ya kufanya zaidi. Onekana, jiamini, fanya kazi yako kwa bidii na uwezo wako wote.
Imehaririwa na Florian Kaijage