Mateka wa Israeli waliosahaulika ambao wameshikiliwa na Hamas kwa miaka kadhaa

tt

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Laurence Peter
    • Nafasi, BBC News

Macho ya ulimwengu yameelekezwa kwa zaidi ya watu 200 waliotekwa nyara na Hamas katika shambulio dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7.

Hata hivyo, hakuna mazungumzo yoyote yanayoendelea kuhusu Waisraeli wengine wawili ambao Hamas imekuwa ikiwashikilia kwa miaka kadhaa.

Ni machache sana yanayojulikana kuhusu Muesraeli mwenye asili ya Ethiopia Avera Mengistu na Muisraeli mwenye asili ya Kiarabu Bedouin Hisham Al Sayed, ambao walitekwa 2014 na 2015 mtawalia.

Hamas, inayoungwa mkono na Iran na kuchukuliwa kundi la kigaidi na nchi za Magharibi, ilidai kikombozi kikubwa sana ili kuwaachilia Waisraeli hao.

Hamas inadai wote wawili ni wanajeshi lakini nyaraka rasmi za Israeli zilizoonekana na Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch zinaonyesha kuwa wote ni raia ambao hawakuruhusiwa kujiunga na jeshi.

Matumaini ya kupatikana kwa Avera na Hisham

Tila Fenta anaongoza kampeni ya kushinikiza kuachiliwa kwa Avera na amesikitishwa na hatua za taifa la Israel katika suala hili.

Hata hivyo, anasema tahadhari ya kimataifa juu ya mateka huko Gaza tangu Oktoba 7 inaweza kusaidia kazi yake.

"Bado tuko katika mshtuko, Waisraeli wote wamo," akimaanisha utekaji nyara mkubwa wa Hamas katika tamasha la muziki siku hiyo hiyo ambapo pia walishambulia maeneo mengine katika eneo la Israel na kuua watu 1,400.

Tangu Oktoba 7, jibu la Israel limelenga zaidi Gaza kwa mashambulizi makali ya mabomu. Mamlaka ya Palestina inakadiria kuwa zaidi ya watu 4,000 wamekufa huko Gaza katika wiki mbili tu za mashambulio ya Israeli.

"Naamini kwamba nafasi za Avera kuachiliwa huru imeimarika, lakini nasema hivyo kwa masikitiko makubwa," Tila Fenta aliiambia BBC.

Pia alieleza kwamba wale wanaofanya kampeni ya kutaka kuachiliwa kwa Avera na Hisham walihisi "wamehuzunishwa" na kushindwa kwa Israeli kuwaokoa kwa miaka hiyo yote.

Avera na Hisham "sio wanajeshi, wote wawili ni wagonjwa, wana matatizo ya kiakili. Hamas inawazuilia katika mazingira magumu kinyume na kanuni zote za ubinadamu."

Fenta alihusisha ukosefu wa mwendelezo wa kesi za Avera na Hisham na hadhi yao duni na ubaguzi katika jamii ya Israeli dhidi ya Wayahudi wa Ethiopia na Waarabu wa Bedouin.

tt

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mama na kakake Avera Mengistu wamekuwa wakilalamikia hali yake kwa miaka mingi.

"Nadhani Avera ni aina ya mtu ambaye jamii haimpendi sana kwa sababu ya rangi yake, ugonjwa wake wa akili na kwa sababu alikulia katika eneo maskini la Ashkelon (mji wa pwani wa Israeli)."

"Yote haya yalimfanya kutengwa. Kama angekuwa mweupe kidogo au kutoka eneo zuri, mambo yake yangeshughulikiwa kwa njia tofauti," alisema. "Najua huu si wakati wa kusema jambo baya kuhusu nchi yangu, lakini ukweli lazima usemwe." ".

Mwanaharakati huyo alishikilia kuwa mashirika makubwa ya kutetea haki za binadamu pia yalipaswa kuongeza juhudi zaidi.

"Hali kadhalika kwa Mabedui: wote wawili wako katika hali ngumu."

Askari ambao hawakurudi tena

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kisa kingine cha mateka wa Hamas waliosahaulika ni kile cha wanajeshi wa Israel Hadar Goldin na Oron Shaul. Wote wawili walifariki wakati wa mzozo kati ya Israel na Hamas mwaka 2014.

Jamaa zao bado wanahangaika kwa majonzi kwa sababu Hamas bado wanahifadhi mabaki yao huko Gaza.

Aviram Shaul, kaka yake Oron, anasema kwa karibu miaka 10 familia yake haijapata habari kuhusu mahali ambapo Hamas imeweka mwili wa Oron.

Pia haijapokea dalili zozote kwamba itarudishwa.

Mnamo 2014, wanajeshi walipata kofia ya Oron na fulana ya kuzuia risasi kwenye handaki la Hamas huko Gaza.

"Ninahisi kama Waisraeli waliwasahau," Aviram aliambia BBC.

"Sasa ni fursa nzuri ya kumrudisha kaka yangu, kwa sababu sasa tunazungumzia familia 200 zilizo na jamaa waliotekwa nyara huko Gaza," alisema.

"Serikali haikufanya vya kutosha kumrudisha kaka yangu, lakini sasa inapaswa kuchukua hatua kubwa."

Kwa maoni yake, "Israel inahitaji kufikia makubaliano ya kibinadamu ili kuwaondoa mateka."

"Kama Hamas inataka umeme na maji, lazima irudishe mateka na miili ya askari kwetu," alisema.

tt

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanaharakati wa Israel watoa wito wa kuachiliwa kwa Avera Mengistu (kushoto) na kukabidhiwa miili ya wanajeshi Oron Shaul (katikati) na Hadar Goldin (kulia).

Uwezekano wa majadiliano ya kuwaachia mateka

Mwaka 2011, baada ya mashauriano ya kisiri, Israel ilimpata mwanajeshi mwingine aliyetekwa nyara, Gilad Shalit, kwa maelewano ya kuwaachilia wafungwa 1,027 wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa katika jela zake.

Israel sasa imedhamiria kuiangamiza Hamas, na kusababisha hasara kubwa na uharibifu katika Gaza kwa mashambulizi ya anga. Kwa hivyo, mashauriano yoyote ya kubadilishana wafungwa itakuwa ngumu na yenye utata.

Huku idadi ya waliouawa Gaza ikiongezeka, uhasama wa Hamas dhidi ya Israel inazidi.

Hagai Hadas, kamanda wa zamani wa jeshi la Israel na afisa wa ujasusi wa Mossad, alichukua jukumu muhimu katika mazungumzo ya kuachiliwa kwa Shalit.

Hadas aliiambia BBC kwamba makubaliano ya kubadilishana wafungwa ni "suala la kisiasa." Katika hali ya dharura ya sasa, na masjambulizi makubwa ya Israel dhidi ya Hamas, "sidhani, itawezekani."

Alisisitiza kuwa mabadilishano ya Shalit yenye utata yaliwezekana kisiasa wakati huo kupitia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Wakati huo, anasema, Netanyahu alijihisi yuko salama na mpango huo ulitimizwa miaka miwili kabla ya kuachiliwa kwa Shalit.

Mnamo Oktoba 2011, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alimpokea mwanajeshi Gilad Shalit baada ya kuachiliwa na Hamas.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo Oktoba 2011, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alimpokea mwanajeshi Gilad Shalit baada ya kuachiliwa na Hamas.

"Sasa ninaamini kwamba kikombozi hakitakuwa kuwaachilia wafungwa wa Hamas, lakini italipwa kwa kutumia zana tofauti," Hadas alisema.

Alibainisha kuwa Israeli ina chaguzi kadhaa : uokoaji wa kijeshi wa moja kwa moja ikiwa taarifa juu ya eneo la mateka ni sahihi, matumizi ya "mali za kiuchumi" au njia mbadala za kibinadamu.

Israel pia inaweza "kuwaacha viongozi wa Hamas kutoroka kutoka Gaza, kwa mfano, hadi Qatar." Akikabiliwa na hali hii, aliongeza: "Tunalazimika kuwashinikiza, tupande ndani yao wazo kwamba ili kuokoa maisha yao wanaweza kufikia makubaliano kama haya."

"Nadhani wengi [wa mateka] wako mikononi mwa Hamas, lakini kadhaa hawako. Nina hakika kwamba Israel inafanya kila juhudi kuwatafuta na kujaribu kuwakomboa kupitia operehseni ya kijeshi."

"Hata katika vita kamili huko Gaza, Israeli itaashinikiza kufikia makubaliano na kuwaachilia mateka. Itajaribu hadi sekunde ya mwisho kutafuta suluhu," alisema.

"Tunathamini maisha na tuko tayari kulipia."

"Hatujawahi kushuhudia kile tulichopitia Oktoba 7," alisema, akimaanisha shambulio la Hamas.