Mpango wa utalii wa Visit Rwanda 'haulingani na maadili ' ya PSG – Mulumbu

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Sara Menai & Rob Stevens
BBC World Service
Nahodha wa zamani wa DR Congo, Youssouf Mulumbu ametoa wito kwa Paris St-Germain kutafakari upya ushirikiano wake na mpango wa utalii wa Rwanda wa Tembea Rwanda (al maarufu Visit Rwanda )wakati akijaribu kuhusu kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu katika nchi yake ambao umewaacha watu "wakiishi kwa hofu".
Waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, wameuteka mji muhimu wa mpakani wa Goma na maeneo makubwa ya ardhi katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC huku takwimu za hivi karibuni kutoka Umoja wa Mataifa zikionyesha kuwa takriban watu 700,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao mwaka huu.
Rwanda imeshutumiwa na kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa si kwa kuunga mkono kundi la M23 pekee bali pia kwa kunufaika na utajiri wa madini yanayoporwa nchini humo.
Rwanda imekanusha madai hayo na kusema kuwa ina nia ya kuimarisha mpaka wake.
Vita vya kudhibiti mji wa Goma viligharimu maisha ya watu 3,000 na kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na pande zote mbili, afisa wa Umoja wa Mataifa amesema.
"Hali ni ngumu sana na inauma sana, na mgogoro huu wote unategemea fedha," Mulumbu aliiambia Newsday kwenye BBC World Service.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Sio vita vya kidini au vya eneo. Ni vita vya kiuchumi na watu wanapaswa kujua hilo.
"Nilipokea ujumbe mwingi kutoka kwa marafiki ambao wanaishi Goma. Wananiambia tu kwamba wanaishi kwa hofu.
"Kuna watoto wanaishi bila wazazi wao, wanawake kubakwa na kuchomwa moto gerezani. Hali ya mambo ni ya ajabu."
Chuma kama vile tantalum, ambayo ni muhimu kwa utendaji mzuri wa smartphone, hutolewa kutoka baadhi ya maeneo muhimu ya madini ambayo kwa sasa yapo chini ya udhibiti wa M23.
Mulumbu alisafiri kwenda Goma mwezi mmoja uliopita, kabla ya mapigano hayo kuongezeka, na marafiki zake wameathiriwa na mgogoro huo.
"Rafiki yangu alinikaribisha mjini Goma. Wakati wa mapambano hayo, alijaribu kutoroka na kumpoteza mkewe. Ni jambo la kusikitisha," alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38.
"Sina maneno ya kuelezea kile kinachoendelea. Ni vigumu sana kwangu, kwasababu ninaishi mbali na ninahisi wakati mwingine sina maana.
"Ni miaka 30 sasa Congo imekuwa ikiishi katika hali hii na tunachotaka ni amani."
Ushirikiano wenye 'doa la damu'
Mapema mwezi huu waziri wa mambo ya nje wa DRC Thérèse Kayikwamba Wagner alimwandikia barua rais wa PSG Nasser Al-Khelaifi, akiitaka klabu hiyo kusitisha mkataba wake wa "kumwaga damu" na Visit Rwanda ulioanza mwaka 2019.
Barua kama hizo pia zilitumwa kwa Arsenal na Bayern Munich, wakihoji maadili ya ushirikiano wao na bodi ya utalii ya Rwanda.
Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda, alisema: "Ushirikiano wa michezo wa Rwanda na kampeni ya Visit Rwanda huleta furaha kubwa kwa Wanyarwanda pamoja kutoa ajira, watalii zaidi na mapato."
Wiki iliyopita afisa mkuu mtendaji wa Bayern Jan-Christian Dreesen aliiambia DW kwamba klabu hiyo imetuma wafanyakazi wawili nchini Rwanda kufuatilia hali hiyo na kwamba inawasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani.
Arsenal na PSG hawajajibu maombi ya kuwataka kutoa maoni.
"Nataka kumshukuru waziri, kwasababu alifanya kazi kubwa sana," kiungo wa zamani wa West Brom Mulumbu alisema.
"Na ninachojua ni kwamba kwa udhamini, kuna sehemu ya kifedha.
"Tutafanya kila tuwezalo kutoa taarifa kuhusu mpango huu na nini kilicho nyuma yake. Nadhani itakuwa hatua kubwa ikiwa tunaweza kufuta [ Ushirikiano] wa Visiti Ewandaii Rwanda."
Ombi kwa PSG

Chanzo cha picha, Getty Images
Mulumbu alianza kazi yake PSG na alicheza mechi 22 klabu hiyo kabla ya kuhamia West Brom mwaka 2009.
"Nimepitia katika chuo cha PSG. Walinifundisha kuhusu thamani ya mchezo, umoja, kuhusu maadili," alisema.
"Hayalingani na Visiti Rwanda [mpango]."
Mulumbu anaunga mkono ombi lililoanzishwa na mashabiki wa PSG ambalo linawataka mabingwa hao wa Ligue 1 kusitisha ushirikiano huo, na kisha ana matumaini kufanya mkutano wake na Al-Khelaifi.
Ombi hilo linalenga kukusanya saini 100,000 na kufikia saa sita mchana siku ya Jumatano alikuwa na saini 68,500.
"Nataka kuwa na mkutano, labda na baadhi ya watu ambao wanaweza kufanya uamuzi, na kisha tutawajulisha kuhusu ushirikiano huu na kile kinachoendelea DR Congo," Mulumbu alisema.
"Sitaki kuweka shinikizo kwa klabu, kwasababu sio watu wanaofanya hivyo, lakini wanahitaji kufahamishwa na kisha baada ya hapo watachukua uamuzi wao wenyewe.
"Hii ndiyo sababu tunapigana na kuzungumza."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












