Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Watu wanane wafariki katika mlipuko unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Marburg Tanzania
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mlipuko unaoshukiwa kuwa wa virusi vya ugonjwa wa Marburg umewaua watu wanane katika mkoa wa Kagera Kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Taarifa ya shirika hilo iliyochapishwa mtandaoni inasema kuwa mnamo tarehe 10 Januari 2025 ''WHO ilipokea ripoti za kuaminika kutoka kwa vyanzo vya ndani kuhusu visa vinavyoshukiwa vya ugonjwa huo katika mkoa wa Kagera, Kaskazini magharibi mwa Tanzania. Watu sita waliripotiwa kuathiriwa na virusi hivyo, watano kati yao walikufa.''
Matukio yaliyo na dalili zinazofanana za maumivu ya kichwa, homa kali, maumivu ya mgongo, kuhara, kutokwa na damu (kutapika kwa damu), malaise (udhaifu wa mwili) na katika hatua ya baadaye ya ugonjwa, kutokwa na damu kwa nje (kutokwa na damu kwenye matundu).
Serikali ya Tanzania haijatoa taarifa yoyote kuhusu mlipuko huo, na BBC inaendelea na juhudi za kutafuta mamlaka za nchi hiyo. Hata hivyo, taarifa ya WHO imekuja siku mbili baada ya Wizara ya Afya ya Tanzania kukanusha taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu mlipuko wa ugonjwa usiojulikana katika mkoa wa Kagera.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema katika ukurasa wake wa X kuwa;
"WHO imetoa msaada wake kamili kwa serikali ya Tanzania, na kwa jamii zilizoathirika"
"Tunapendekeza nchi jirani kuwa macho na tayari kudhibiti kesi zinazowezekana kutokea. Hatupendekezi vikwazo vya usafiri au biashara na Tanzania kwa wakati ."
Kwa mujibu wa taarifa ya WHO, hadi kufikia Jumamosi tarehe 11 Januari 2025, watu tisa walioshukiwa waliripotiwa ikiwa ni pamoja na vifo vinane katika wilaya mbili, Biharamulo na Muleba. Sampuli kutoka kwa wagonjwa wawili zimekusanywa na kupimwa na Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma.
Matokeo yanasubiri kuthibitishwa rasmi.
''Wahudumu wa afya wamejumuishwa miongoni mwa kesi zinazoshukiwa kuathiriwa, ikiangazia hatari ya maambukizi hospitalini. Chanzo cha mlipuko huo kwa sasa hakijajulikana. Ripoti ya WHO imeeleza.
Kuripotiwa kwa kesi zinazoshukiwa za mlipuko wa virusi vya Murbag kutoka wilaya mbili zinaonesha kuenea kwa kijiografia.
Kuchelewa kubaini kwa mlipuko huo na kutengwa kwa walioathirika, pamoja na ufuatiliaji unaoendelea wa mawasiliano, inaonesha ukosefu wa taarifa kamili ya mlipuko wa sasa. Kesi zaidi zinatarajiwa kutambuliwa.
Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera ilikumbwa na mlipuko wa kwanza mwezi Machi 2023. Mlipuko huo mnamo Machi 2023 ulidumu kwa karibu miezi miwili, watu tisa wakithibitishwa kuambukizwa ikiwa ni pamoja na vifo sita.
Mkoa wa Kagera pia unapakana na nchi ya Rwanda ambapo ugonjwa huo ulilipuka kutoka Septemba mpaka Disemba mwaka jana ambapo watu 65 walipata maambukizi na 15 kufariki dunia. Hata hivyo WHO haijahusianisha mlipuko wa Rwanda na mlipuko unaoshukiwa kutokea Kagera kwa sasa.
Ugonjwa wa Marburg ni nini?
Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt. Ujerumani na Belgrade huko Serbia.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.
Nchi kadhaa za Afrika zimewahi kuripoti mlipiko wa virusi ikiwa ni pamoja:
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
- Kenya
- Afrika Kusini
- Uganda
- Zimbabwe
Mlipuko wa mwaka 2005 nchini Angola ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 300. Lakini barani Ulaya, ni mtu mmoja tu amefariki katika kipindi cha miaka 40, na mmoja nchini Marekani,baada ya kurejea kutoka katika safari ya kuzuru mapango nchini Uganda.
Milipuko mikubwa:
2017, Uganda: visa vitatu, watu watatu walifariki
2012, Uganda: vis 15, watu wanne walifariki
2005, Angola: visa 374, watu 329 walifariki
1998-2000, DR Congo: visa 154 cases, watu 128 walifariki
1967, Ujerumani: visa 29, watu saba walifariki
Chanzo: WHO
Je, hueneaje?
Popo wa matunda aina ya rousette wa Misri mara nyingi huwa na virusi. Nyani wa kijani kibichi na nguruwe wanaweza pia kubeba.
Miongoni mwa wanadamu, huenea kupitia maji ya mwili na malazi yaliyochafuliwa nao.
Na hata watu wakipona, damu au mbegu zao za kiume, kwa mfano, zinaweza kuwaambukiza wengine kwa miezi mingi baadaye.
Je, inaweza kutibiwaje?
Hakuna chanjo maalum au matibabu ya virusi.
Lakini aina mbalimbali za bidhaa za damu, madawa ya kulevya na matibabu ya kinga yanatengenezwa, WHO inasema.
Na madaktari wanaweza kupunguza dalili kwa kuwapa wagonjwa waliofika hospitali maji mengi ili kuchukua nafasi ya damu iliyopotea.
Vinawezaje kudhibitiwa?
Watu barani Afrika wanapaswa kuepuka kula au kushika nyama ya porini, Gavi, shirika la kimataifa linalokuza upatikanaji wa chanjo, linasema.
Watu pia wanapaswa kuepuka kuwa karibu na nguruwe katika maeneo yenye mlipuko, WHO inasema.
Wanaume ambao wamekuwa na virusi wanapaswa kutumia kondomu kwa mwaka mmoja baada ya kupata dalili au hadi mbegu zao za kiume zitakapothibitishwa mara mbili kuwa hazina virusi.
Na wale wanaozika watu ambao wamekufa kutokana na virusi wanapaswa kuepuka kugusa mwili.
Imeandikwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Athuman Mtulya.