Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakama DRC yaombwa Joseph Kabila ahukumiwe kifo kwa tuhuma ukiwemo uhaini
Waendesha mashtaka wa kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamemuombea hukumu ya rais wa zamani wa nchi hiyo Joseph Kabila kwa tuhuma za uhaini na kushirikiana na kundi la waasi la AFC/M23.
Anashtakiwa kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa na vuguvugu la M23, na njama ya kupindua serikali.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya Ijumaa, mji mkuu Kinshasa, Waendesha mashtaka pia uliomba mali zake zote zichukuliwe.
Kabila, ambaye hakufika mahakamani, hajutoa tangazo lolote la umma mara moja kuhusu hukumu hukumu ya kifo aliyoombewa.
Hata hivyo Jumamosi kupitia jukwaa lake la X, Kabila alisema: ''Iwe Mashariki wala Magharibi haitaweza kutugeuza kutoka kwa njia yetu. Watu wa Congo hawatavumilia tena udikteta au udhalimu uliotokana na uchoyo. Mwisho wako tayari umeandikwa, kama jua linalotua kila jioni kwenye upeo wa macho. Kwa maana mapenzi ya watu waliosimama imara yana nguvu kuliko nguvu zote kwa pamoja''.
Baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya maafisa wa serikali ya Kinshasa wamekuwa wakidai kabila sio mtoto halisi wa rais wa zamani wa DRC laurent Desire kabila tuhua ambazo zimekuwa zikiwashangaza baadhi ya Wacongo ambao wamekuwa wakiijadili kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo wakili katika kesi ya Kabila mjini Kinshasha amelaani kauli hiyo akisema ni ya udhalilishaji na Mke wa Lauhrent Desire Kabila anapaswa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa madai hayo:
''Familia ya Joseph Kabila, na hasa Maman Sifa [Mke wa Laurent Desire Kabila], ina kila haki ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Jamhuri na mwandishi wa taarifa hizi za kashfa. Kisheria, madai yoyote lazima yaungwezwe na ushahidi wazi, sahihi, na unaoweza kuthibitishwa. Vinginevyo, haya ni mashtaka yasiyo na msingi ambayo yanadhoofisha heshima, utu, na sifa ya wengine. Mtu yeyote anayetoa madai hayo yasiyo na msingi anawajibika kushtakiwa kwa kashfa na mashtaka ya uharibifu'', alisema
Mwezi Mei mwaka huu, bunge lilimvua kinga, na hakuweza tena kujitokeza kujieleza kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Katika hotuba yake baadaye mwezi huo, Kabila aliukosoa vikali utawala wa mrithi wake, Félix Tshisekedi, akiuita "wa kidikteta."
Pia aliikosoa mahakama ya nchi hiyo kukubali "kutumika wazi kwa madhumuni ya kisiasa."
Mara ya mwisho Kabila alionekana hadharani katika eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23 mashariki mwa DRC.
Mbali na hukumu ya kifo iliyoombwa, Radio Okapi, kituo kinachofadhiliwa na Umoja wa Mataifa kinachofanya kazi nchini DRC, kiliripoti kwamba mwendesha mashtaka mkuu wa kijeshi Lucien René Likulia aliiomba mahakama kuu ya kijeshi :
- kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kusaidia uhalifu wa kivita;
- kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kujaribu kupindua serikali;
- akamatwe mara moja;
- Kulipa gharama za mahakama.
Ferdinand Kambere, katibu wa kudumu wa chama kilichopigwa marufuku cha PPRD cha Kabila, aliliambia shirikaka la habari la Reuters siku ya Ijumaa kwamba hiki ni "kitendo kisichokoma" cha "mateso kwa kiongozi yeyote wa upinzani".
Hapo awali, waendesha mashtaka wa kijeshi walintaka Kabila kulipa fidia ya dola bilioni 24 kwa serikali ya DRC, Radio Okapi iliripoti.
Uhasama baina ya serikali ya Kinshasa na Joseph Kabila ulizidi pale Bwn. Kabila alipozuru eneo linalodhibiwa na waasi la M23 na kukutana na viongozi wa kundi hilo ambapo Kinshasa ilimtuhumu kuunga mkono waasi.
Wakati huo Kabila alisema kuwa amekwenda kukutanza na M23 na viongozi wa kijamii ili kutafuta suluhu la mzozo wa vita ili kurejesha amani, akidai kuwatenga waasi sio suluhu la mzozo.
Wachambuzi wanahoji ni kwanini serikali ya Kinshasa inamlaumu Kabila kuzungumza na waasi ilihali serikali hiyo hiyo imekubali kufanya mazungumzo na waasi.
Kesi hiyo ilianza mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mahakama ya juu zaidi ya kijeshi inatarajiwa kutangaza uamuzi wake kabla ya tarehe ya kwanza ya Septemba ijayo (9).