Je, ni kwanini shujaa wa propaganda wa Urusi Afrika alirejeshwa nyumbani?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Kukwepa risasi, kulipua mabomu, kulinda siri za serikali. Filamu za propaganda za milipuko yenye sauti kubwa (Bombastic) zinamuonyesha mwanasiasa wa Urusi Maxim Shugalei kama mtu shujaa - ambaye anaacha kila kitu katika jitihada zake za kunadi Urusi nje ya nchi.

Wakati matukio yake bila shaka yametiwa chumvi, katika maisha halisi amekuwa na jukumu muhimu katika kupanua ushawishi wa Urusi katika sehemu za Afrika, akifanya kazi kwa karibu na kundi la mamluki wa Urusi la Africa Corp(zamani Wagner).

Hata hivyo, mtu huyu ambaye hivi karibuni alikuwa maarufu alipata pigo wakati alipokamatwa nchini Chad.

Yeye, pamoja na wafanyakazi wenzake wa Urusi Samer Sueifan na E Tsaryov, walikamatwa mwezi Septemba kwa mashtaka ambayo hayakuelezwa, kabla ya kuachiwa huru na kurudishwa nyumbani mapema mwezi huu, kwa mujibu wa Ubalozi wa Urusi.

Je Maxim Shugalei ni nani?

Shugalei huwa anajielezea kama "mwanasosholojia" lakini wachambuzi wanasema, yeye ni msemaji na wakala wa ushawishi wa Urusi anayejulikana kwa kazi yake katika bara la Afrika.

Amekuwa chini ya vikwazo vya EU tangu 2023 kwa kusimamia kampeni za habari za kulinadi kundi la mamluki wa Urusi, Wagner Group, katika nchi kadhaa za Afrika, na pia ni suala la vikwazo vya Ukraine.

Tangu mwaka 2010, Shugalei alikuwa na uhusiano na mfanyabiashara wa Urusi marehemu Yevgeny Prigozhin, bosi wa Wagner na mshirika wa karibu wa Rais Vladimir Putin.

Wakati Shugalei alikuwa akikanusha uhusiano huu - kama ilivyokuwa desturi kwa wandani wa Prigozhin - hata hivyo alitambuliwa na vyombo vya habari kwa kazi yake na kukamatwa baadaye nchini Libya kwa mashtaka ya upelelezi na kuingilia uchaguzi kwa niaba ya mkuu wa Wagner.

Prigozhin alikuwa amempa jukumu Shugalei kukusanya taarifa na kuandaa mkakati wa kumuunga mkono Seif al-Islam Gaddafi, mtoto wa kiongozi wa zamani Muammar Gaddafi.

Wakati Shugalei aliporudi Urusi, Prigozhin alifichua kwamba alikuwa amempa 18m rubles ($ 173,000; £ 138,000) - 1m rubles kwa kila mwezi alikuwa alipokuwa mateka.

Matukio Shugalei nchini Libya yaliunda msingi msururu wa filamu za televisheni, inayoonekana kufadhiliwa na Prigozhin. Filamu hizo pamoja na mambo mengine, zilibuniwa kutukuza utawala wa mshirika wa wakati huo wa Wagner Khalifa Haftar mashariki mwa Libya na kusafisha shughuli za Urusi barani Afrika.

Nafasi ya Shugalei lilichezwa na muigizaji Kirill Polukhin, na filamu hizo zinauonyesha kama "anayefanana na karibu na James Bond , au Mission Impossible ", anasema Ladd Serwat, Mtaalamu wa kanda ya Afrika katika mradi wa Data ya Migogoro ya Silaha na Tukio (Acled).

"Tunamuonyesha kama mtu jasiri ambaye hakatishwi tamaa kuumizwa au kwa shinikizo au kutoa siri za kitaifa – hivyo basi ana uwezo mkubwa kama mamluki au kiongozi wa kijeshi."

Ukurasa wa shabiki wa kawaida mtandaoni unatoa madai ya uongo kuwa "Shugalei" limekuwa neno la Kiarabu linalomaanisha "mtu wa shupavu ambaye hawezi kukata kutoa siri kutokana na kuumia".

Lakini kama mhusika muhimu katika upanuzi wa ushawishi wa Urusi barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni, pia amehusika katika shughuli za ajabu katika maisha halisi.

Mwaka 2018, uchunguzi wa BBC ulibaini kuwa alikuwa mmoja wa maafisa kadhaa wa Urusi ambao walikamatwa wakitoa mikoba iliyojaa fedha taslimu kwa wagombea urais nchini Madagascar.

Kabla ya shughuli zake nje ya nchi, sehemu pekee ya umma ya kazi ya Shugalei kama mshauri wa kisiasa ilianzia uchaguzi wa 2002 kwa bunge la St Petersburg.

Wakati huo, Shugalei aliwahi kuwa muwakilishi wa mmoja wa wagombea na maarufu alitafuna nyaraka kadhaa wakati wa mkutano wa tume ya uchaguzi ili kuzuia zisiwasilishwe mahakamani.

Shugalei ana ushawishi gani?

Chini ya Prigozhin, nafasi rasmi ya Shugalei ilikuwa mkuu wa Fwakfu wa kulinda maadili ya taifa - Protection of National Values, shirika linalounga mkono Wagner na kampuni ya mahusiano ya umma.

Alifanya kazi isiyo rasmi katika nchi mbalimbali za Afrika kujaribu kuhakikisha serikali zinazopendelea Wagner zinaingia na kubaki madarakani, kama sehemu ya majaribio ya Urusi ya kupata ushawishi katika bara - hasa kwa gharama ya Ufaransa.

Tangu kifo cha Yevgeny Prigozhin kitokee mwaka jana, wanajeshi wanaohudumu chini ya bendera ya Wagner nchini Ukraine na Afrika wameingizwa katika mfumo rasmi jeshi la Urusi.

Hata hivyo, ufalme wa vyombo vya habari vya Prigozhin, ambao Shugalei alikuwa sehemu yake, umeanguka.

Kama mtu ambaye anafanya kazi katika kwa kujificha, ni vigumu kujua hasa ni ushawishi gani anaotumia.

Hatahivyo, kwa mujibu wa baadhi, Shugalei huenda hakupoteza ushawishi mkubwa licha ya kifo cha mshauri wake.

"Bado anaonekana kuwa na kiwango sawa cha ushawishi, licha ya ukweli kwamba Kremlin inaonekana kuwa imechukua shughuli nyingi za kikundi cha Wagner," anasema Beverly Ochieng, mchambuzi mwandamizi anayeshughulikia kitengo cha Francophone Africa for Control Risks.

Anaonekana kuwa hakatai tena uhusiano wake na Wagner na Prigozhin - kituo chake cha Telegram kimejaa machapisho ya kumbukumbu ya oligarch marehemu na kikundi chake cha mamluki, na hata anarudisha habari kuhusu ajira za Wagner.

Hata hivyo, mbali na kukamatwa kwake nchini Chad na safari ya Julai kwenda Angola ambayo aliandika kwenye Telegram, ni vigumu kuelezea kiwango kamili cha shughuli zake za sasa.

Kwanini alikamatwa nchini Chad?

Chad haijatoa sababu rasmi ya kukamatwa kwa Shugalei na washirika wake wawili.

Nadharia nyingi zimetolewa- zingine zinaweza kuwa ni za ukweli zaidi kuliko zingine.

Kituo cha habari kinachodhibitiwa na serikali ya Urusi RT kiliripoti kuwa kukamatwa kwa watu hao kulichochewa na Ufaransa, lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa ni uongo uliobuniwa kulinda hadhi yake , Bi Ochieng ameiambia BBC.

Tangu angalau Mei, Urusi imekuwa ikipigia debe hadithi kwamba ushawishi wa jadi wa Magharibi nchini Chad unapungua.

Lakini, ingawa Chad hivi karibuni imesaini mikataba na Urusi juu ya miundombinu na usalama, bado inashikilia vikosi vya Ufaransa, na ina uhusiano mzuri na nguvu ya zamani ya kikoloni, tofauti na majirani zake kadhaa wa wanaozungumza kifaransa ambao wameelekea Urusi.

Hakuna ushahidi wa kuwepo kwa jeshi la Urusi nchini humo.

Kwakweli, wengine wanasema kuwa Rais wa Chad Mahamat Déby ana uhusiano wa ustadi na Urusi na Magharibi , kwa faida ya Chad.

Urusi inajitahidi kupata utawala kamili wa eneo la Sahel la Afrika Magharibi, na tayari ina uhusiano wa karibu na majirani wawili wa Chad - Niger, na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), ambako Urusi ina ushawishi mkubwa zaidi katika bara hilo.

Wapiganaji wa Wagner wanasemekana kuipenyeza Chad kutoka CAR na kupambana na jeshi la eneo hilo, kabla ya kurudi nyuma.

Ikiwa Urusi inaweza kuileta Chad katika mzunguko wake, hiyo inaweza kuunda uwanja usioingiliwa wa ushawishi unaoenea maelfu ya maili.

Shugalei alikuwa ametembelea Chad mara mbili kabla, na alifanya mazungumzo na timu ya kampeni ya Déby kabla ya uchaguzi wa rais mwezi Mei.

Pia alihusishwa na kituo cha utamaduni cha Urusi , Russia House katika mji mkuu, N'Djamena, ambacho hivi karibuni kilizindua makao makuu mapya katika sherehe iliyohudhuriwa na maafisa wa serikali ya Urusi.

Mwaka jana, idara za ujasusi za Marekani zilisema kuwa ziligundua kuwa Wagner ilidaiwa kupanga njama ya kumuua Déby lakini ilishindwa kutekeleza hilo.

Bwana Serwat anasema hii ndiyo sababu Shugalei alikamatwa.

Bi Ochieng anasema Chad huenda ilikuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wa Shugalei kujaribu kuiyumbisha nchi kwa kueneza taarifa za uongo.

Wakfu wa Shugalei umekanusha kwamba yeye ni "mpelelezi wa Wagner", ukisema Shugalei "hajui chochote hasa kuhusu shughuli za Wagner Group barani Afrika na anajua tu maelezo ya jumla kuhusu kile ilichofanya hapo awali".

Maudhui ya mitandao ya kijamii yanayoungwa mkono na Urusi, vituo vya televisheni na tovuti za habari yanatumwa kueneza ajenda ya kuiunga mkono Urusi na taarifa potofu, hasa barani Afrika, kwa mujibu wa wachambuzi.

Mifano ni pamoja na Afrique Media TV ambayo inatangaza kutoka Cameroon hadi maeneo mbali kama CAR, Ivory Coast, Mali, Burkina Faso, Niger - na pia iko kwenye YouTube ambapo ina maelfu ya wafuasi, na inawafuasi wengi kwenye mtandao wa Facebook.

Shugalei mwenyewe anatania uwepo wake katika nchi mbalimbali za Afrika, wakati mwingine akishirikisha umma video fupi, za chini za bajeti, za mtindo wa vlog ambazo zinaweka wazi hulka yake ya kujionyesha.

Miongoni mwa maudhui ya video yanayowalenga Waafrika, nyingi huchukua mfano kama wa hadithi - moja, inayoitwa LionBear - inaonyesha dubu (ambaye anaashiria Urusi) inayotembea kote ulimwenguni kumtetea simba (rafiki yake wa Jamhuri ya Afrika ya Kati) kutokana na ushawishi mbaya wa fisi.

"Sidhani kama watu lazima wanaziangalia kwa muda mrefu video hizi - watu wanafikiri ni za kuchekesha, utani," anasema Bi Ochieng.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi