Trident: Silaha mpya ya Ukraine inayoweza kuangusha ndege zinazoruka kwa urefu wa kilomita mbili'

    • Author, Oleg Khornysh
    • Nafasi, BBC Ukraine Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Vadym Skaryevsky, kamanda wa vikosi vya mifumo isiyokuwa na rubani ya jeshi la Ukraine, amedai kwamba Ukraine imeunda silaha ya leza.

Kabla ya tangazo la kamanda wa Ukraine, hakukuwa na taarifa zozote kuhusu Ukraine kuunda silaha za leza.

Nchi chache duniani zina silaha za leza zinazoweza kutumika vitani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax Ukraine, Kamanda Skaryevsky alisema kuwa Ukraine ni nchi ya tano duniani kumiliki uwezo wa silaha za leza.

"Kwa msaada wa leza hii, tunaweza kuangusha ndege inayoruka kwa urefu wa kilomita mbili."

Kwa mujibu wa Skaryevsky, silaha hii imeitwa "Trident" , na Ukraine inajaribu kuiboresha.

Hata hivyo, kutoka kwa kauli ya Kamanda Skaryevsky, haieleweki ni aina gani ya silaha, muundo wake, sifa zake, na kama imejaribiwa katika hali halisi ya vita.

Kauli ya Skaryevsky ilitolewa wakati wa mkutano kuhusu kuimarisha uhusiano kati ya sekta za kijeshi za Ulaya na Ukraine.

leza ni silaha ya aina gani?

Takriban miaka 70 iliyopita, mataifa ya kimataifa yalianza juhudi za kukuza silaha za leza.

Wazo la silaha inayoweza kuunguza vifaa vya adui kwa sekunde chache lilikuwa lenye mvuto mkubwa kwa majeshi ya Sovieti na Marekani.

Silaha kama hii ingeweza kutumika kwa madhumuni ya kujilinda na kushambulia.

Lakini ukweli, kutengeneza silaha kama hiyo ilionekana kuwa ni vigumu sana.

Awali, mataifa hayo mawili, Marekani na Sovieti, zilikiri kwamba walikuwa wameunda silaha za leza ambazo zingeliweza kuangusha ndege za adui kwa urahisi.

Lakini baadaye, yote haya yaligunduliwa kuwa ni porojo tu.

Baadhi ya mifano ya majaribio ya silaha hizi zilikuwa zimetengenezwa, lakini kuzifanyia kazi kulisitishwa kwa haraka kutokana na ukosefu wa fedha na sababu nyingine.

Kikwazo kikubwa katika kukuza silaha hizi za leza kilikuwa hitaji la chanzo cha nguvu kilicho na nguvu kubwa kuendesha leza hizi na hitaji la kuzipoza baada ya matumizi.

Aidha, utegemezi wa hali ya hewa, matatizo katika kulenga vifaa viwili vinavyopaa kwa pamoja na kwa haraka, na gharama ya vifaa vilivyotumika katika silaha hii, zilikuwa ni vikwazo vikubwa.

Mwisho wa karne iliyopita, mataifa makubwa duniani yalianza kutilia mkazo kuboresha silaha za kawaida kama vile makombora ya masafa marefu badala ya kukuza silaha za leza.

Hata hivyo, changamoto zinazojitokeza katika muktadha wa mabadiliko ya hali ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na vita vya Urusi na Ukraine, zimeamsha tena mjadala kuhusu silaha za leza.

Sababu moja ya kuongezeka kwa hamu hii ni kutafuta rasilimali zinazoweza kuwa bei rahisi ili kupambana na ndege zisokuwa na rubani za bei nafuu zinazotumika sasa kwenye vita.

Kwa kuwa ndege zisokuwa na rubani ni za bei nafuu ikilinganishwa na silaha nyingine za kawaida, majeshi yanazitumia kwa wingi, kwasababu kutumia makombora ya kulipua ndege ni ghali sana.

Kwa upande mwingine, juhudi za kushambulia ndege zisizokuwa na rubani kwa bunduki za mashine mara nyingi ni vigumu.

Kuzishambulia na kulipua ndege zisizokuwa na rubani kwa miale ya leza yenye nguvu inaonekana kama suluhisho la bei nafuu na linaloweza kutekelezeka.

Mataifa ambayo yanadai kumiliki silaha ya leza

Kuna nchi chache tu duniani zinazodai kuwa na silaha za leza.

Nchi zinazodai kuwa na silaha za leza ni pamoja na Marekani, Urusi, China, Uingereza, Korea Kusini, Japan, na Israel.

Mbali na leza za kupambana na makombora, maafisa wa Marekani wamesema wamezungumzia kuhusu kukuza silaha hizi kwa ajili ya Jeshi la Wanamaji na Jeshi la Anga.

Inasemekana China imefanikiwa kutengeneza bunduki za leza pamoja na leza zilizo na uwezo wa kulipua ndege zisizokuwa na rubani haraka.

Miaka michache iliyopita, Rais wa Urusi Vladimir Putin alidai kuwa Urusi imeunda silaha inayoweza kupofusha hata setilaiti kwa msaada wa leza.

Jeshi la Israel lilitoa agizo la silaha za leza za boriti ya chuma mwaka huu.

Silaha hizi zinatarajiwa kupelekwa kwa wanajeshi mwishoni mwa mwaka 2025.

Mfumo wa kulipua ndege unaweza kugonga ndege ndogo zinazolengwa kutoka umbali wa kilomita kadhaa.

Korea Kusini na Japan pia zimefanikiwa kutengeneza makombora ya nyuklia na mifumo ya leza ya kupambana na ndege zisizokuwa na rubani.

Uingereza inatarajia kuwa na mfumo wake wa leza unaotoa moto mkubwa katika utumishi wa kijeshi ifikapo mwaka wa 2027.

Dragoni ya moto ni mfumo wa leza wa kilowati 55 unaolenga kwa kutumia miale 37 tofauti.

Mwaka huu, maafisa wa Uingereza walisema hawawezi kuondoa uwezekano wa kuhamisha Dragoni ya moto kwa Ukraine kwa majaribio ya vita.

Silaha ya leza ya Ukraine ni ya aina gani?

Kufikia sasa, hakuna taarifa inayoonyesha kuhusu silaha mpya ya Ukraine, Trident.

Skaryevsky alisema katika kauli yake kwamba Trident ina uwezo wa kuangusha ndege kutoka umbali wa kilomita mbili.

Mfumo wa Uingereza wa Dragoni ya moto unaweza kugonga dango kutoka umbali wa kilomita moja, wakati boriti ya chuma ya Israel ina umbali wa mara mbili ya huo.

Tofauti nyingine kati ya mifumo hii ni kwamba silaha ya Uingereza ina leza ya kilowati 55, wakati boriti ya chuma ina leza ya 100 kilowati.

Ikiwa silaha ya Ukraine kweli ina uwezo wa kuangusha ndege, inamaanisha kuwa wanao mfumo wa kulenga ndege zinazopaa kwa kasi.

Kwa mfano, Dragoni ya moto inaweza kugonga lengo hadi umbali wa kilomita moja kwa usahihi wa milimita 23.

Mtaalamu wa silaha za Ukraine, Oleg Katkov, aliiambia BBC inawezekana kwamba Ukraine imefanikiwa kutengeneza aina hii ya silaha.

Wanatoa hoja kadhaa ili kuthibitisha mtazamo wao, mojawapo ikiwa ni kwamba teknolojia na vifaa vinavyohitajika kutengeneza silaha za leza vimekuwa rahisi kupatikana katika nusu karne iliyopita.

Kwa maoni yake, pamoja na sekta ya kijeshi ya Ukraine, sekta binafsi pia inaweza kutengeneza mfano wa mfumo wa leza.

Anasema kuwa sekta ya ulinzi ya Ukraine ni tofauti kabisa sasa kuliko ilivyokuwa mwaka 2022.

Katkov anasema hawezi kushangazwa ikiwa leza hii imetengenezwa na kampuni binafsi.

Lakini anasema jinsi silaha hii inavyofanya kazi ni swali gumu.

Katkov anasema ufanisi wa Trident unategemea mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na teknolojia inayotumika kutengeneza miale ya leza, uwezo wa kulenga kwa umbali unaohitajika, na ufanisi wake katika hali tofauti za hewa.

Anasema nchi nyingi zina mifumo ya leza ya majaribio, lakini hadi sasa hakuna aliyepima katika hali halisi ya vita.

"Nchi hizi bado zinajaribu tu kugundua jinsi ya kuzitumia."

Kwa maoni yake, ikiwa Trident si mfano wa majaribio pekee na inaweza kufanya kazi katika mazingira ya vita, itakuwa mapinduzi halisi katika zama za silaha.

Lakini bado ni mapema kutoa maoni yoyote kuhusu hilo kwa sasa.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla