'Nimekuwa nikilala chini ya daraja Lagos kwa miaka 30'

Muda wa kusoma: Dakika 4

Akiwa ameishi kwa nusu ya maisha yake chini ya daraja katika jiji kubwa la Nigeria, Lagos, Liya'u Sa'adu anajiona kama "mlezi" wa watu wengine wengi wasio na makazi ambao wamejiunga naye huko.

Zaidi ya wanaume 60 sasa wanaishi katika eneo la wazi katika eneo lililowakutanisha kwa karibu - na Daraja la Obalende lenye kelele juu yao - kwani wameshindwa hata kumudu kukodisha kibanda cha kuishi.

Bw Sa'adu anawashauri wageni - mara nyingi vijana kutoka miji na vijiji vya mbali - jinsi ya kuishi mitaani katika mji wa Lagos wenye maisha ya kasi, ambapo ni rahisi kutumbukia katika uhalifu na madawa ya kulevya.

“Nina umri wa miaka 60 na kuna vijana waliokuja hapa miezi michache iliyopita au miaka michache iliyopita. Ninaona kuwa jukumu langu ni la kuwaongoza,” anaiambia BBC.

"Ni rahisi sana kupoteza mwelekeo hapa Lagos, hasa kwa vijana kwa sababu hakuna familia ya kutazama mienendo yao."

Sawa na wengi wa wale wanaoishi chini ya daraja, anazungumza Kihausa, lugha inayozungumzwa zaidi kaskazini mwa Nigeria.

Aliwasili hapa kutoka mji mdogo wa Zurmi kaskazini-magharibi mwa jimbo la Zamfara mwaka 1994 - lakini wale wote aliojenga nao urafiki wakati huo ama wamefariki dunia au wamerejea katika miji yao au vijijini.

Tukur Garba, ambaye alianza kuishi chini ya daraja hilo miaka mitano iliyopita, anasema ushauri wa Bw Sa'adu umekuwa wa thamani sana na anaheshimiwa sana na wale wanaofika kujaribu bahati yao katika kitovu cha uchumi cha Nigeria.

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 31 anatoka katika jimbo la kaskazini la Katsina, takriban kilomita 1,000 (maili 621).

"Ni kama kaka yetu mkubwa kwa sababu amekuwa hapa kwa muda mrefu. Tunahitaji maneno ya hekima kutoka kwake kwa sababu ni rahisi kupata matatizo Lagos,” asema.

Unaweza pia kusoma:

Eneo hilo sasa limepewa jina la "Karkashin Gada", ambalo kwa lugha ya Kihausa linamaanisha "Chini ya Daraja".

"Watu wanaokuja hapa wanajua mtu ambaye tayari anakaa hapa au ana mtu ambaye aliwaambia kuhusu Karkashin Gada," Bw Sa'adu anasema.

"Nilipokuja hapa, kulikuwa na chini ya watu 10."

Adamu Sahara, ambaye ameishi katika ghorofa karibu na Karkashin Gada kwa zaidi ya miaka 30, anasema kuwa ukosefu wa makazi unaongezeka Lagos.

"Ukosefu wa usalama (ikiwa ni pamoja na uasi wa makundi ya jihadi) na uchumi duni umewafanya watu wengi kukimbia kaskazini mwa Nigeria," Bw Sahara anasema.

"Viongozi wa Nigeria wanapaswa kufahamu kinachoendelea ili waweze kurekebisha tatizo kwa sababu hakuna binadamu anayepaswa kulala chini ya daraja."

Mkazi huyo wa muda mrefu zaidi wa Karkashin Gada hana mpango wa kurejea Zamfara kwani hakuna fursa za kiuchumi huko huku utekaji nyara na ujambazi ukiongezeka.

Hii imewalazimu watu wengi kuacha biashara na mashamba yao huku wakikabiliwa na hatari ya kuchukuliwa mateka na magenge yanayodai kikombozi.

Ili kufanya maisha kuwa ya starehe iwezekanavyo, Bw Sa'adu amepata godoro, matandiko, kabati la mbao na chandarua.

Ameweka godoro juu ya kabati, na hapo ndipo anapolala.

Bwana Sa'adu ni miongoni mwa watu wenye hali nzuri zaidi kwani baadhi ya wanaume wengine wanaoishi huko hawana samani, na wanashiriki na wengine mikeka ya kulalia ambayo wanaikunja sakafuni.

Kwa bahati nzuri, hatari ya wizi ni ndogo kwani baadhi ya "wakazi" wa Karkashin Gada huwa katika eneo hilo, wakifanya kazi au kufurahia muda wao wa mapumziko.

Wote hutumia bafu ya umma iliyo karibu na choo kwa gharama ya naira 100 ($0.06; £0.05) kila wanapotumia.

Ni mara chache kwa watu wa Karkashin Gada kupika - au kuwasha moto, hata wakati wa majira ya baridi kwani wakazi wake wengi hununua chakula kutoka kwa wachuuzi wanaouza vyakula vinavyopendwa na watu wa kaskazini.

"Hii ni moja ya sehemu za Lagos ambapo unaona idadi kubwa ya watu kutoka kaskazini mwa Nigeria kwa hivyo nauza fura [unga wa mtama uliochanganywa na maziwa yaliyochachushwa] hapa na ninafurahi kusema kuwa watu wengi wananunua," muuzaji wa chakula Aisha Hadi anaiambia BBC.

Katika kipindi cha miongo yake mitatu aliyoishi jijini Lagos, Bw Sa'adu ameendelea kutoka kuwa mfanyabiashara wa kung'arisha viatu hadi kuwa muuzaji wa vyuma chakavu - akiokota chuma mitaani na kwenye karakana kutoka kwenye maduka yanayouza ili kuchakatwa tena.

Inamletea kipato cha wastani wa naira 5,000 ($3; £2) kwa siku, juu ya kiwango cha umaskini uliokithiri cha $1.90 kwa siku lakini ni kiasi kidogo kinachomtosha kuishi.

"Usisahau pia inabidi nitume pesa kwa familia yangu huko Zamfara kila wiki, kwa hivyo ni mapambano yanayoendelea," Bw Sa'adu anasema.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi

Imehaririwa na Maryam Abdalla