Kwanini Waafrika Kusini wanamiminika kwenye meli ya matibabu ya China?

Mwanachama wa timu ya matibabu ya jeshi la China akitathmini wagonjwa kwenye Ark of Peace huko Cape Town, Afrika Kusini - 26 Agosti 2024

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wananchi wamekuwa wakipanga foleni tangu Jumatatu ili kuhudumiwa na madaktari wa jeshi ndani ya hospitali inayoelea.
    • Author, Mohammed Allie
    • Nafasi, BBC News, Cape Town
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Hali mbaya ya hewa ya majira ya baridi kali, theluji kwenye Milima na upepo mkali haijapunguza shauku ya wakazi wa Cape Town ya kupata huduma ya matibabu bila malipo kwenye meli ya China, ambayo kwa sasa imetia nanga katika bandari ya jiji la Afrika Kusini.

Mgogoro wa kifedha katika mojawapo ya nchi zenye uchumi mkubwa na ulioendelea zaidi barani Afrika umeathiri huduma za umma zikifedha, na idadi kubwa ya watu hawawezi kumudu huduma za afya za kibinafsi kwa sababu ya kupanda kwa bei.

Inakuja miezi kadhaa baada ya serikali kutia saini kuwa sheria mpango mpya wa afya wenye utata, ambao unalenga kutoa huduma ya afya kwa wote, lakini inakabiliwa na vitisho vya changamoto za kisheria.

Tangu kile kinachojulikana kama Safina ya Amani (Ark of Peace) ya China kuwasili wiki iliyopita, zaidi ya Waafrika Kusini 2,000 wametibiwa ndani ya meli hiyo - kufanyiwa uchunguzi aina mbali mbali wa kimatibabu.

China inafurahia ushirikiano mkubwa wa kisiasa na Afrika Kusini, na hili ndilo onyesho la hivi punde la uwezo wa Beijing.

Lucy Mnyani aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa alifurahi kuona picha za mtoto wake ambaye hajazaliwa kwa mara ya kwanza: "Nilikuwa nikienda hospitali za za Gugulethu na Langa [vitongojini] na hawakuwahi kunifanyia CT scan."

Mtu mwingine aliyepanga foleni, Joseph Williams, aliambia shirika la utangazaji la taifa la SABC: “Unapoenda kliniki unasubiri kwa saa kadhaa kabla ya kuhudumiwa, inategemea hali yako.

“Hapa huduma inatolewa kwa haraka sana hivyo nashukuru nimekuja. Kwa kweli nilipata matokeo ya kile kilichonileta."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maafisa wanasema meli hiyo ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa 700 kila siku na huduma hiyo ni sehemu ya mazoezi ya pamoja kati ya majeshi ya Afrika Kusini na China. Meli hiyo ina wahudumu 100 ndani yake ikiwa na vitanda 300, vitanda 20 vya wagonjwa mahututi, vyumba vya upasuaji, idara za kliniki na hata helikopta ya uokoaji.

Siku mbili za kwanza za Ark of Hope zilishuhudia watu waliochaguliwa awali wakipatiwa matibabu kabla ya milingo kufunguliwa kwa umma siku ya Jumatatu.

"Tulishirikiana na mamlaka ya jiji kutoa huduma kwa watu wanaoishi katika mitaa ya Cape Town kwa sababu hawana huduma yoyote ya afya," Saadiq Kariem, mkuu wa Idara ya Afya ya Western Cape, aliiambia BBC.

Aliongeza kuwa wazee wanaoishi katika nyumba za utunzaji pia wameletwa kwa ajili ya matibabu, na wafanyakazi wa afya wa Cape Magharibi walipewa ziara za afya.

"Tangu kujiandikisha hadi kukamilisha huduma yangu ilinichukua saa moja," alisema Dk Kariem, ambaye mwenyewe alienda kuchunguzwa afya na kujiunga na foleni kama raia wa kawaida.

"Ni jambo ambalo lingechukua muda mrefu zaidi katika vituo vyetu vya afya vya umma kwa sababu kuna watu wengi zaidi wanaohitaji huduma."

Jumla ya upasuaji 57 umefanywa kufikia sasa, sehemu ndogo katika orodha ya wagonjwa 80,000 ya mkoa.

Na hii ni katika jimbo la Western Cape, ambalo lina mojawapo ya mifumo bora ya afya nchini.

"Hizi zimekuwa nyingi za upasuaji wa mifupa, mtoto wa jicho na upasuaji mdogo wa kuunganisha mirija kwa wanawake ambao hawataki tena kupata ujauzito," Dk Kariem alisema.

Umaarufu wa Ark of Hope unatoa ujumbe, alisema Dk Shuaib Manjra, mwenyekiti wa Mpango wa Haki ya Afya: "Inaonyesha mfumo wa afya ya umma katika jimbo na nchini haukidhi mahitaji ya watu inavyopaswa.

“Mara nyingi unakuta watu wanakaa siku nzima kwenye zahanati wakisubiri kuhudumiwa, kuna mrundikano mkubwa hospitalini, bajeti na vituo vinapunguzwa, na mara nyingi hali hii inasababisha watu kukosa kwenda kazini hata siku mbili ili kufanyiwa utaratibu mdogo wa kimatibabu," aliiambia BBC.

Meli ya hospitali ya China, Peace Ark, mjini Cape Town

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wachambuzi wanasema umaarufu wa Ark of Hope unaonyesha kuwa mfumo wa afya ya umma wa Afrika Kusini umezidiwa sana.

Chama cha African National Congress (ANC) kinasema mpango wake wa Bima ya Afya ya Kitaifa (NHI) utakuwa na tija kwani huduma zote katika vituo vya umma na vya kibinafsi zitatolewa bila malipo katika kituo cha huduma - kwa gharama ya serikali.

Waziri wa Afya Aaron Motsoaledi amesisitiza kuwa mpango huo utatekelezwa licha ya chama kikuu kupoteza wingi wake wa wabunge mwezi Mei, na kuingia katika muungano na vyama kama vile Democratic Alliance (DA) vinavyopinga baadhi ya vipengele vya mpango huo.

Itasababisha mtikisiko mkubwa wa sekta ya afya, lakini wakosoaji wanahofia inaweza kuwafanya wataalamu wa afya kutafuta ajira nje ya nchi.

Mpango huo unapingwa vikali na kampuni za afya za kibinafsi kwani unazuia watu kuchukua bima ya afya ya kibinafsi kwa matibabu.

Kwa sasa takriban 14% ya watu wana huduma ya matibabu ya kibinafsi, na 86% iliyobaki wakitegemea kliniki na hospitali za serikali zilizoelemewa.

Wiki iliyopita, Jumuiya ya Biashara ya Afrika Kusini na Jumuiya ya Madaktari ya Afrika Kusini zilikataa kutia saini kile kinachojulikana kama "mkataba wa afya" - makubaliano ya kila mwaka na rais ambayo yanaweka wazi jinsi sekta mbalimbali zinavyopaswa kushughulikia changamoto za afya katika mwaka ujao.

Mashirika hayo mawili - ambayo kati yao yanawakilisha biashara za kibinafsi na madaktari 12,000 - yamekasirishwa na NHI katika hali yake ya sasa, wakihisi kuwa imelazimishwa.

Dk Manjra alisema NHI ni "wazo zuri" lakini anatilia shaka utekelezaji wake.

"Historia yetu ya rushwa na uzembe inaweza kuharibu sekta nzima ya afya. Inakadiriwa kuwa katika baadhi ya matukio hadi theluthi moja ya bajeti ya afya inapotea kwa rushwa."

Kushughulikia masuala haya ndani ya sekta ya afya ya umma kunapaswa kuwa kipaumbele, alisema.

Wanajeshi wa Afrika Kusini wafanya upasuaji kwenye meli ya hospitali ya China mjini Cape Town - Jumatatu tarehe 26 Agosti 2024

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Madaktari wa jeshi la Afrika Kusini pia wamekuwa wakifanya upasuaji kwenye meli hiyo yenye vifaa vya kutosha

Siphiwe Dlamini, msemaji wa jeshi la Afrika Kusini, aliiambia BBC kuwa Safina ya Amani imepokelewa yvyema kwa "umakini na ustadi wa wahudumu wake wa afya".

Hospitali hiyo inayoelea inaondoka Cape Town siku ya Alhamisi kuelekea Angola kabla ya kuhamia nchi nyingine kadhaa. Tayari imezuru Ushelisheli, Tanzania, Madagascar na Msumbiji - katika ziara hii ya 10 tangu kuanzishwa mwaka 2008.

Mpango huo unaonekana kuwa hatua zaidi katika juhudi za China kuongeza ushawishi wake katika bara la Afrika.

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita biashara yake na Afrika imekua kwa kasi, wakati Beijing pia imekuwa ikishiriki zaidi katika sekta ya ujenzi - ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja vikubwa vya michezo katika maeneo kadhaa ya bara.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi