Historia ya kupinga uchaguzi Kenya ilivyoimarisha taasisi za kidemokrasia

Na Ambia Hirsi

Mwaka 2010, Kenya ilipitisha katiba mpya ambayo ilielekeza nguvu zaidi katika mfumo wa serikali ikiwa ni pamoja na kutenganisha mamlaka ya mihili mitatu ya utawala -Rais, Bunge na Mahakama.

Mbali na kuwa katiba hiyo mpya ilijikita katika mamlaka yasiyotwishwa muhimili mmoja wa uongozi unaoweza kuhojiwa na kudhibitiwa, pia ilipunguza kwa kiasi kikubwa mamlaka makubwa ambayo hapo awali muhimili wa rais ulikuwa nayo.

La muhimu ni kwamba, katiba mpya ilianzisha kile ambacho Wakenya wengi wanaamini ni mahakama huru, yenye uwezo wa kuhakikisha kwamba shughuli za serikali zinafanywa tu kwa kuzingatia katiba.

Kutokana na mabadiliko yaliyoletwa na katiba nchini, historia ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais ikaandikishwa kwa mara ya kwanza sio tu nchini Kenya bali pia katika bara zima la Afrika.

Historia hiyo inaandamana kwa ukaribu sana na shughuli nzima ya mwanasiasa mkongwe wa Kenya na Waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Raila Odinga kutafuta uongozi wa taifa hilo.

Kwa karibu sana historia inayokumbukwa na Wakenya wengi ni mwaka 2017 ambapo alishinda kesi aliyowasilisha mahakamani kupinga uchaguzi wa rais Uhuru Kenyatta na kufanya matokeo ya uchaguzi huo kubatilishwa.

''Katika uamuzi huo wa kihistoria mahakama ilidhihirishwa kuwa Raila Odinga alikuwa ameibiwa kuru…alikuwa amedhulumiwa, mahakama ikasema kwamba malalamishi yake yalikuwa ni ya haki’’, Mchambuzi wa siasa za Kenya Alutalala Mukhwana aliambia BBC.

Hata hivyo baada ya mahakama kuagiza kwamba uchaguzi urudiwa Bw. Odinga alisusia uchaguzi huo kwa kuhoji utenda kazi wa maafisa wakuu wa uchaguzi wakati huo.

Alitaka mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati na Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo wakati huo Ezra Chiloba wang’atuliwa ofisini kwani uwepo wao hautabadilisha lolote lililofikiwa katika uamuzi huo wa mahakama.

Pia unaweza kusoma:

Historia inayofuata ni ile ya mwaka 2013 wakati wa huo Dkt Willy Mutunga akiwa Jaji Mkuu wa Kenya, ambapo Raila Odinga aliwasilisha malalamishi mahakamani akidai kuwa katiba ilikiukwa, sheria ya uchaguzi nchini Kenya imekiukwa na yeye hakupewa haki kushiriki uchaguzi huo.

Ikumbukwe kwamba wakati huo Raila alipoteza kesi hiyo kwa sababu Jaji Mkuu Willy Mutunga alisema kuwa japo kulikuwa na dosari za hapa na pale zilizotaja Bw. Raila Odinga, dosari hizo hazikutosha kubatilisha uchaguzi.

Katika sheria ya uchaguzi hususan kipengele cha 83 sheria inasema kwamba hata kama uchaguzi haukufanyika kwa misingi muafaka ya kisheria mahakama haitabatilisha uchaguzi kwa misingi hiyo tu kwamba uchaguzi haukufanyika kwa kuzingatia sheria.

Kufafanua hili Bw Alutalala Mukhwana anasema: Iwapo uchaguzi ulifanyika kwa uhaki na usawa lakini kukawa na dosari kidogo na hiyo dosari kwa ujumla haikuathiri kwa njia yoyote matokeo ya uchaguzi, basi haina haja kubatilisha uchaguzi kwa madai kwamba katiba haikufuata asili mia kwa mia.

Kwa misingi hiyo ya kipengele cha 83 cha sheria ya uchaguzi Jaji mkuu Mutunga alitupilia mbali malalamishi ya Bw Odinga mwaka 2013.

Mwaka 2007 upinzani haukwenda mahakamani na badala yake ukaitisha maandamano yaliyozua ghasia na kusababisha maaafa makubwa na watu kufurushwa makwao.

Mwaka 2002 hakukua na malalamishi kwa sababu Mwai Kibaki aliungwa mkono na Raila Odinga ikikumbukwa alivyosema ‘’Kibaki Tosha’’

Kwa hivyo historia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais na kwenda mahakamani imejikita katika vipindi vya miaka 15 kutoka mwaka 2003 hadi leo.

Baada ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2013 kutupiliwa mbali, Bw Odinga alieleza ni kwa nini hakujutia kwenda mahakamani.

"Uamuzi wangu wa kuwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu kupinga uhalali wa uchaguzi ulikuwa kauli ya imani yangu katika uhuru wa mahakama.Tulifanya hivyo kwa ajili ya demokrasia yetu na kwa ajili ya Wakenya wote waliotaka kufanya hivyo."... kutekelezewa haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wao kupitia chaguzi huru na za haki."

Alikuwa akizungumza miaka mitano tu baada ya nchi hiyo kutumbukia katika ghasia za baada ya uchaguzi baada ya madai ya wizi wa kura.

Ghasia hizo za kikabila zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 na kuwalazimisha wengine 600,000 kuondoka makwao.

Bw Odinga pia alikuwa mmoja wa mawakili wakuu wa katiba mpya, ambayo ilipitishwa 2010.

Chini ya katiba iliyotangulia, wakati mwingine ilichukua miaka mitano - muhula kamili wa kisiasa - kusikiliza kesi ya kupinga uchaguzi, wakili Omwanza Ombati alisema.Wakati Bw Moi akiwa mamlakani, kuanzia 1978-2002, upinzani haungeweza kumpatia ilani ya kupinga ushindi wake kwa sababu walihitajika kufanya hivyo ana kwa ana.

"Katiba hiyo ilitoa hadhi maalum kwa mshindi wa uchaguzi," Bw Ombati alisema.

Majaji pia walionyesha uaminifu kwa Bw Moi - "sheria ilitumiwa kama chombo cha kutumikia udikteta wa Moi," aliongeza.

Katiba ya 2010 iliunda Mahakama ya Juu na mchakato wazi na wa haraka ambao hutoa njia kwa walioshindwa katika uchaguzi kutetea kesi yao.

Ombi la hivi punde la Bw Odinga dhidi ya kutangazwa kwa William Ruto kama rais mteule linaonekana kuwa fursa nyingine ya kusaidia kushughulikia baadhi ya masuala ambayo yameibuka wakati wa uchaguzi wa hivi majuzi.

Lakini je, hali hii ya wanasiasa kukimbilia mahakamani kila baada ya miaka mitano inamaanisha nini kuhusu mfumo wa demokrasia wa nchi na sheria zilizopo?

Wataalamu wa sheria wanasema ni haki ya kidemokrasia na ya kisheria kwa yeyote aliyeshiriki katika uchaguzi ama ambaye anahisi au kuona kwamba amedhulumiwa kwenda mahakamani kuwasilisha malalamiko yake.

Kesi hizi zinazowasilishwa mahakamani zinaashiria mambo matatu:

Wakenya wamejifunza kutumia mahakama kama njia ya kutatua mzozo badala ya njia ya fujo.

Japo mahakama zimejitahidi na kufanya kazi nzuri bado kuna changamoto kubwa katika hulka ya wanasiasa wa Kenya na wafuasi wao kwamba bado kuna ile tabia ya kutaka kutumia njia zisizostahili kujipatia nafasi ya uongozi katika mabunge na katika serikali.

''Hiyo ni tabia ambayo imekataa kuwatoka wanasiasa na raia na ndio maana unaona kila mara wanakimbia kwenye mahakama wakidai wamedhulumiwa ama wengine wakidai wale ndio wenye kuwadhulumu'', anasema mchambuzi wa siasa za kenya Alutalala Mukhawana

Faida ya kesi za kupinga uchaguzi kenya

Ufanisi katika upeperushaji matokeo haukuwa wa kubahatisha bali ni matokeo ya kesi iliyoletwa na Bw Odinga baada ya kushindwa katika uchaguzi uliopita akidai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kushindwa kwa tume ya uchaguzi kuwasilisha matokeo yote kwa njia ya kielektroniki kama inavyotakiwa na sheria, ili kupunguza matokeo, jambo ambalo liliwaweka wao katika hatari ya kuibiwa kura.

Katika uamuzi wa wengi, majaji wa Mahakama ya Juu waligundua kuwa "ukiukwaji haramu'' na "kasoro'' zilifanyika na kwa hivyo wakabatilisha uchaguzi wa 2017 na kuamuru urudiwe.

"Kimsingi Mahakama ya Juu ilikuwa ikisema kwamba hakukuwa na uchaguzi.

Kuhesabu na kujumlisha kura haikuwa na dosari - tatizo lilihusiana na uwasilishaji na uthibitishaji wa matokeo. Kwa sababu hii ilikuwa ni ukiukaji wa sheria," alisema Prof Akech.

Kulingana na wakili Omwanza Ombati, ambaye alifanikiwa kutetea ushindi wa mbunge mwaka wa 2008 - wa kwanza tangu kurejeshwa kwa vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 1990 - ingawa Bw Odinga ana rekodi tofauti kuhusiana na changamoto zake za uchaguzi, amechangia "pakubwa" jinsi sheria ya uchaguzi inavyotumika katikauchaguzi wa urais."

Je mahakama imetatua migogoro ya kisiasa?

Kwa kiasi kikubwa mahakama nchini Kenya imefanikiwa kutatua migogoro ya kisiasa.

Mchambuzi wa siasa za Kenya Alutalala Mukwana anasema, ''ukiangalia yaliyojiri mwaka 2007 mpaka tukaokolewana jamii ya kimataifa na baada ya hapo mwaka 2013 Mhe. Raila Odinga alienda mahakama.''

Anaongeza kuwa kiasi cha maandamano hakikushabikiana hata kidogo na machafuko yaliyoshuhudiwa mwaka 2007.

Hii ni ishara kwamba Wakenya wamejifunza kutokana na matukio hayo.

''Japo Raila Odinga alishindwa katika uchaguzi huo na vile vile kushindwa katika mahakama hakukua na machafuko kama yale yaliyotokea miaka iliyopita'', anasema Bw Alutalala.

Mifano hii inaashiria kuwa mahakama imeanza kuchangia katika nafasi ya demokrasia na haki ya uchaguzi nchini Kenya.