Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Togo: Miongo sita ya utawala wa familia moja ya Gnassingbé
- Author, Beverly Ochieng & Tom Santorelli
- Nafasi, BBC Monitoring, Nairobi and BBC News, London
Watu wa familia moja wamekuwa na historia ndefu kwa muda mrefu katika kuchagiza hali ya kisiasa ya mataifa mengi ulimwenguni.
Mfano, familia ya Bushes nchini Marekani hadi Kims huko Korea Kaskazini, Bhuttos nchini Pakistani hadi Trudeaus nchini Canada, majina fulani ya ukoo yamekuwa na nguvu na ushawishi wa kisiasa.
Nchini Togo, Afrika Magharibi, familia ya Gnassingbé imetawala kwa zaidi ya nusu karne, huku rais wa sasa, Faure Gnassingbé, yuko madarakani tangu 2005.
Akiendelea na mabadiliko ya katiba ambayo yanaweza kurefusha utawala wake, maswali yanaibuka kuhusu athari kwa demokrasia ya nchi hiyo.
Ukoo wa Gnassingbé
Mwaka 1967, wakati rais wa sasa akiwa na umri wa miezi tisa tu, babake Gnassingbé Eyadéma alinyakua madaraka katika taifa hilo la Afrika Magharibi kupitia mapinduzi ya kijeshi.
Eyadéma alipofariki mwaka 2005, mwanawe Faure Gnassingbé akawa rais. Tangu wakati huo amekumbwa na maandamano makubwa, tishio la mapinduzi ya kijeshi na kupungua kwa umaarufu wa utawala wake.
Rais Gnassingbé anatazamiwa kusalia hadi 2031 baada ya Bunge la Kitaifa, linalotawaliwa na chama chake cha Union for the Republic (UNIR), kupitisha katiba mpya siku ya Ijumaa (19 Aprili) ambayo itabadilisha mfumo wa utawala wa nchi kwa rais na Wabunge.
"Kwa sasa hakuna mrithi wake anayeonekana. Rais haonekani kumpigia upatu mtu yoyote wa kumrithi kwa sasa," anasema msemaji wa Songhai Advisory, kampuni ya ushauri ya uwekezaji barani Afrika.
Kuunda upya katiba
Kubadilisha katiba ndiyo mbinu kuu ambayo Gnassingbé wameitumia kudumisha utawala wao. Wacha tuangalie jinsi jambo hilo lilivyofanyika:
Mwaka 2002, chini ya Rais Eyadéma, bunge liliondoa ukomo wa mihula miwili ya urais ambayo ilikuwa katika katiba ya 1992.
Alipoingia mamlakani mwaka 2005, Faure Gnassingbé alinufaika na mabadiliko haya. Lakini 2017 na 2018, utawala wake wa muda mrefu ulikumbwa na maandamano makubwa ya kutaka aondoke.
Gnassingbé alijaribu kuzima maandamano kwa kurudishan tena kikomo cha mihula miwili. Lakini waandamanaji hawakukata tamaa huku wanaharakati wachanga wakimtuhumu kutojua kinachoendelea.
Vyama vya upinzani CAP 2015 na Pan-African National Party vilisema mabadiliko hayo, yatamruhusu tu Gnassingbé kugombea tena uchaguzi huo, na uwezekano wa kuwa mamlakani hadi 2030.
Kujibu maandamano, mamlaka ilizuia intaneti na kukandamiza maandamano yaliyopewa jina #TogoDebout (Togo Standing), ambayo yalipata uungwaji mkono kubwa hadi katika ngome za kaskazini za Gnassingbé.
Kutokana na hali hiyo, Togo ilitozwa faini ya dola za kimarekani 3,400 na mahakama ya kikanda ya Afrika Magharibi kwa kuzima intaneti. Lakini hilo halikuizuia serikali kuendelea kupiga marufuku maandamano na kukabiliana na wapinzani.
Gnassingbé alisukuma mbele pendekezo lake na bunge likabadilisha katiba mwaka 2019. Alishinda kwa muhula wa nne mwaka 2020 kwa asilimia 71 ya kura na anastahili kuchaguliwa tena mwaka 2025.
Mpatanishi anayeaminika kikanda
Licha ya kukosolewa nyumbani kutokana na uongozi wake, Gnassingbé amekuwa na mchango mkubwa katika upatanishi kati ya serikali zinazoongozwa na jeshi za Afrika Magharibi, ambazo mara kwa mara zimeonyesha imani kwake, na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas).
Umoja wa kikanda umekuwa ukifanya kazi ya kurejesha demokrasia baada ya kurudishwa nyuma na mfululizo wa mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni.
Rais wa Togo alisimamia kuachiliwa kwa makumi ya wanajeshi wa Ivory Coast wanaozuiliwa na jeshi la serikali ya Mali, wakati kukiwa na mzozo juu ya vikwazo vikali vya Ecowas vilivyowekwa baada ya jeshi kuchukua mamlaka 2020 na 2021.
Wanajeshi wa Niger pia walitaka Togo iwe nchi ya kati wakati wakidai vikosi vya Ufaransa viondoke - baada ya kunyakua mamlaka Julai 2023.
Gnassingbé aliwezesha kuondolewa kwa vikwazo zaidi dhidi ya Burkina Faso, ambayo ilishuhudia mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka 2022, na Mali.
Yeye pia ni mlezi wa Kongamano la Amani na Usalama la Lomé, lililozinduliwa rasmi mwaka jana ili kujadili kuhusu usalama wa kanda na bara.
Kuhusu katiba mpya
Chini ya katiba mpya, rais atachaguliwa na wabunge "bila mjadala" - badala ya umma – atatumikia muhula mmoja wa miaka sita kama rais asiye mtendaji kisiasa. Nafasi ya waziri mkuu imeanzishwa ili iwe ndiyo yenye mamlaka ya utendaji.
Tangu upinzani kususia uchaguzi wa wabunge wa 2018, Bunge la Kitaifa limekuwa likitawaliwa na chama cha Gnassingbé UNIR.
Vyama vitatu vya upinzani - Alliance of Democracies for Integral Development (ADDI), Democratic Forces for the Republic (FDR) na National Alliance for Change (ANC) - na kanisa Katoliki vimekuwa vikijaribu kupambana na UNIR.
Majaribio ya kufanya maandamano ya siku tatu kati ya tarehe 11 na 13 Aprili yalishindikana baada ya msako mkali wa vikosi vya usalama.
Tarehe 23 Aprili, kiongozi wa upinzani Gerry Taama aliwasilisha malalamiko dhidi ya mabadiliko hayo katika mahakama ya kikatiba, hukumu bado inasubiriwa.
Juhudi za upinzani kupindua mabadiliko zinaonekana kupungua, wapinzani wa Gnassingbé sasa wanapanga kuhamasisha uungwaji mkono kabla ya uchaguzi wa Aprili 29 wa kikanda na ubunge.
Kudumaa kwa Demokrasia
Mchambuzi kutoka Togo, Paul Amegakpo anasema mabadiliko hayo yanaweza kutishia demokrasia katika eneo hilo.
"Mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari mbaya kwa demokrasia katika eneo la Afrika Magharibi ambapo tunaona demokrasia ikiporomoka kupitia mapinduzi ya kijeshi na kuwepo kwa vipengelee vya katiba vya kumng’ang’aniza rais madarakani."
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, viongozi katika mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi na Kati wamefanya mabadiliko makubwa ya katiba ili kuhalalisha upanuzi wa mamlaka yao na kudhoofisha ukosoaji.
Ukomo wa mihula ya urais uliondolewa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka jana, sasa inamruhusu Rais Faustin Touadera - serikali yake inayoungwa mkono na mamluki wa Kundi la Wagner la Urusi - kusalia madarakani milele.
Tawala za kijeshi nchini Mali na Chad pia zimetumia kura za maoni kuonyesha kuunga mkono mabadiliko ya katiba licha ya kutochaguliwa kidemokrasia.
Mabadiliko ya katiba ya Guinea mwaka 2019 yalimruhusu Alpha Conde kuwania muhula wa tatu. Baadaye aliondolewa madarakani na jeshi kufuatia maandamano makubwa ya kupinga kurefushwa kwa utawala wake.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah