Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afya: Wanasayansi wako mbioni kutengeneza mkate wenye afya zaidi
- Author, Pallab Ghosh
- Nafasi, BBC
Wanasayansi wanajaribu kuunda aina mpya ya mkate wenye afya. Mradi huo umefadhiliwa na serikali ili kuboresha manufaa ya kiafya ya chakula hicho cha Uingereza.
Watafiti wanapanga kuongeza kiasi kidogo cha mbaazi, maharagwe na nafaka kwenye mchanganyiko wa mkate, pamoja na baadhi ya vitamini ambavyo kawaida huondolewa kutoka unga mweupe.
Watengenezaji mkate wamejaribu kufanya mikate meupe yenye afya zaidi hapo awali kwa kuongeza pumba kwenye unga wao, lakini wateja wao hawakupenda ladha na umbile lake.
Namna utakavyo tengenezwa
Mradi wa utafiti bado uko katika hatua za awali.
Dk Catherine Howarth wa Chuo Kikuu cha Aberystwyth, mmoja wa viongozi wake wa utafiti, anasema wanasayansi wameanza kuchambua kwa kina muundo wa kemikali za unga mweupe.
Alisema kuongeza viwango vya lishe huku ladha ikibaki kuwa nzuri. Wanasayansi wanajaribu kuunda aina mpya ya mkate wenye afya lakini uonekane na ladha yake iwe kama mkate mweupe.
Tunataka kujua ni vitamini na madini gani hasa hupotea wakati wa kusuaga," alisema Dk Howarth.
"Kwa kutumia nafaka nyingine tunaweza kuongeza kiwango cha madini ya chuma, zinki na vitamini na muhimu zaidi nyuzinyuzi, kwa sababu mkate mweupe una nyuzinyuzi kidogo sana, ambazo ni muhimu sana kwa afya njema."
Mara tu Dk Howarth atakapokuja na viungo hivyo, Chris Holister, meneja wa ukuzaji wa bidhaa wa kampuni ya kutengeneza unga ya Gloucestershire Shipton Mill, atavigeuza kuwa mkate.
Hatua ya mwisho itakuwa kujaribu mkate mpya kwa watu ili kuona kama wanaweza kuutofautisha na mkate mweupe iliyopo kwenye maduka makubwa.
Inatarajiwa kuwa bidhaa hiyo inaweza kuwa kwenye rafu za maduka makubwa katika muda wa miaka miwili kutoka sasa.
Timu ya watafiti inaamini mbinu yao itafaulu kwa sababu wanaongeza tu safu ya ndani ya mkate, ambayo haina ladha kali na rangi. Wataongeza na nafaka zingine zenye lishe lakini zenye ladha kidogo.
Mkate mweupe lazima uongezwe madini na vitamini kisheria ili kufidia upotevu wa madini na vitamini wakati wa mchakato wa kusafisha.
Lakini Dkt Amanda Lloyd, anaefanya kazi na Dk Howarth na Holister, anaamini matumizi ya viambato asilia yatafanya mkate mweupe kuwa na afya zaidi.
"Ikiwa ubora wa lishe ya mkate wa kawaida itaboreshwa," anasema Dk Lloyd, "basi ubora wa maisha ya watu, afya na ustawi wao yataboreka."
Tim Lang, profesa wa sera ya chakula katika Chuo Kikuu cha City, ambaye ni mtafiti huru katika timu hiyo ya utafiti, anasema, kazi hiyo inaweza kuwa hatua muhimu katika kuboresha afya za watu.
"Waingereza wamekuwa na mapenzi na mkate mweupe kwa zaidi ya karne moja na wataalamu wa lishe wanatamani watu wengi zaidi wale nafaka ya kutosha," alisema. "Utafiti mpya unaonekana kama njia ya kufanya hivyo.
"Wakosoaji wanaweza kusema utafiti huo utawahadaa watu kula chakula cha kuboresha lishe yao, lakini wataalamu wa lishe watasema haijalishi - ni bora kuwafanya watu wasifurahi lakini uboreshe afya zao!
"Lakini mjadala bado uko wazi kama mbinu hii mpya itafanya kazi," aliongeza.
Kulingana na Jumuiya ya Kisukari ya Uingereza (BDA), hatari ya ugonjwa wa moyo, kiharusi na kisukari cha aina ya 2 inaweza kushuka hadi 30% kwa watu ambao hula nafaka nzima mara kwa mara na hatari ya saratani ya matumbo inaweza pia kupungua.
BDA inasema tafiti zinaonyesha 95% ya watu wazima hawali nafaka ya kutosha na mtu mmoja kati ya watatu hali kabisa.
Lakini Chris hafikirii kuwa watu watarudi kula nafaka ya kutosha kama zamani kwa sababu watu wengi wamezoea kula mkate mweupe.
"Mkate mweupe ni wa bei nafuu zaidi kuliko mkate wenye nafaka ya kutosha kwa sababu makampuni yamejipanga kuuzalisha. Na pia ndio ambao watu wengi wameuzoea."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah