Mwanafunzi wa udaktari anayebuni tiba ya kisukari itakayotumia mwanga

Mwanafunzi wa shahada ya uzamivu nchini Benin Marie Marthe Chabi ni mmoja wa vijana 30 wa kike wenye vipaji vya kisayansi kutoka Afrika mwaka wa 2024

Chanzo cha picha, Marie Marthe Chabi

Maelezo ya picha, Mwanafunzi wa shahada ya uzamivu nchini Benin Marie Marthe Chabi ni mmoja wa vijana 30 wa kike wenye vipaji vya kisayansi kutoka Afrika mwaka wa 2024
    • Author, Ibrahim Zongo
    • Nafasi, BBC Africa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mnamo Desemba tarehe 10, Taasisi ya L'Oréal na UNESCO ilitangaza washindi wa Tuzo za Vijana wa Talanta kwa Wanawake katika Sayansi barani Afrika.

Tuzo hii, ambayo iko katika toleo lake la 15, iliwatunuku mwaka 2024 watafiti 30 kutoka Afrika katika nyanja ya sayansi, wakiwemo wanafunzi 25 wa shahada ya uzamivu na wanafunzi 5 wa baada ya shahada ya uzamivu kutoka nchi 15 za Afrika.

Miongoni mwao ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu kutoka Benin, Marie Marthe Chabi.

Pia unaweza kusoma:

Marie Marthe Chabi anajitokeza kwa utafiti wake katika sekta ya afya, akilenga ugonjwa unaozidi kuathiri Waafrika: Kisukari.

Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 24 walikuwa na kisukari barani Afrika mwaka 2021, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 55 ifikapo 2045, ongezeko la asilimia 129.

gg

Chanzo cha picha, Getty Images

Ugonjwa huu, ambao unachukuliwa kama janga barani Afrika, unajitokeza kwa aina mbalimbali kulingana na shirika la afya duniani WHO.

Aina za Kisukari:

  • Aina ya Kisukari cha Kwanza (Type 1): WHO inasema hii inatokana na uzalishaji mdogo wa insulini mwilini, na hivyo inahitaji usambazaji wa nje wa insulini kwa mwili wa mgonjwa. Dalili ni pamoja na kukojoa mara kwa mara, kiu isiyokoma, njaa ya mara kwa mara, kupungua uzito, matatizo ya kuona, na uchovu.
  • Aina ya Kisukari cha Pili (Type 2): WHO inasema hii inatokana na uzalishaji mdogo wa insulini au mwili kushindwa kutumia insulini vizuri. Aina hii ya ugonjwa, ambayo awali ilikuwa inawaathiri watu wazima, "imeenea kwa watoto wengi," inasema WHO. Dalili zake ni kama za aina ya kwanza, na husababishwa na uzito kupita kiasi na ukosefu wa mazoezi. Hii imeonekana kwa asilimia 95% ya watu waliogundulika na kisukari.
  • Kisukari cha Ujauzito: Hali hii ya sukari ya juu mwilini hutokea kwa wanawake wajawazito na ina hatari kubwa ya matatizo wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua. "Watoto wao pia wako katika hatari kubwa ya kupata kisukari cha aina ya pili," anasema WHO.
Marie Marthe Chabi aliamua kufanya utafiti kuhusu kisukari cha pili

Chanzo cha picha, Marie Marthe Chabi

Maelezo ya picha, Marie Marthe Chabi aliamua kufanya utafiti kuhusu kisukari cha pili

Mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika sayansi ya biolojia, Marie Marthe Chabi, alichagua kuzingatia utafiti wake katika kisukari cha aina ya pili, na chaguo hili si kwa bahati mbaya.

"Kwa upande wangu, najua watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu na lazima kutambua kuwa wengi wao wana maisha ya uchochole kutokana na magonjwa yanayotokana na kisukari cha aina ya pili," anasema Bi. Chabi.

Ikiwa kisukari kinatambuliwa kama ugonjwa unaojulikana na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu, kwa mujibu wa Marie Marthe Chabi, ugonjwa huu unazidi hali hiyo.

"Unatanuka hadi kuwa magonjwa kama ya moyo, magonjwa ya neva, na hata matatizo ya macho," anasema.

Kadri mambo yanayohitaji kufuatiliwa ili kuwa na maisha bora yanavyopuuziliwa mbali, ndivyo ugonjwa huu unavyoendelea kuathiri na hata kusababisha vifo vya waafrika wengi.

"Ndio maana napigania kupambana na ugonjwa huu wa kisukari," anasema Marie Marthe Chabi.

Mwanga kama tiba ya kisukari

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tiba hii inahusisha kutumia mwanga kwenye mwili wa mgonjwa ili kugundua, anasema, mifumo na njia za ishara ambazo zinazuia au kupunguza ufyonzaji wa glukosi.

Lakini je, inatosha kutumia mwanga wowote kwa mwili? Na ni katika sehemu gani ya mwili?

Mchakato huu ni mgumu zaidi, anasema kutoka mwanzo, akiongeza kuwa anazingatia "mwanga mwekundu, mwanga wa sumakuumeme."

"Kweli mwanga ni nishati. Ni kama jua linalotupatia joto tunapokuwa baridi. Huu mwanga una chembe ndogo zinazojulikana kama photon ambazo hutumika kama vyanzo vya nishati kwa mitambo midogo ya nishati inayopatikana mwilini iitwayo mitochondria."

Mtu anapomulikwa na kifaa cha mwanga mwekundu au mwanga wa sumakuumeme, kwa mfano, hizi nishati ndogo katika mwili hugundua nishati hiyo ya mwanga.

Nishati hii itasimamia njia zinazoruhusu ufyonzaji wa glukosi ambao umekatizwa kwa watu wanaosumbuliwa na kisukari cha aina ya pili, anasema.

"Changamoto yetu hapa ni kuonyesha kwamba kwa mwanga mwekundu, tunaweza kurejesha njia hii ili kuboresha ufyonzaji wa glukosi na hivyo kupunguza uchochezi unaopatikana katika viungo vinavyolengwa na insulini," anaendelea kuelezea Chabi.

Gharama ya kufanya utafiti

Mwanafunzi wa udaktari Marie Marthe Chabi anafanya majaribio ya kuridhisha kwa panya.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanafunzi wa udaktari Marie Marthe Chabi anafanya majaribio ya kuridhisha kwa panya.

Kama suluhisho lolote la matibabu, teknolojia inayopendekezwa na Marthe Chabi hutumika kwa maagizo na matibabu ya daktari.

Hii ni hasa kwa sababu, anasisitiza, "kwa sasa, tuko bado katika hatua ya majaribio."

"Tuna majaribio mengi ya kufanya. Tuna marekebisho mengi ya kufanya ili tuweze kumruhusu mgonjwa kutibiwa."

Kwa sasa, Marie Marthe Chabi anaendelea kuboresha utafiti wake kwa kufanya majaribio kwenye mifano ya wanyama.

Ili kufikia bidhaa bora ya mwisho, mtafiti anahitaji kupitia hatua tatu ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa wa muda, maarifa, na hasa rasilimali za kifedha na vifaa.

Hatua ya kwanza, ambayo ni hatua ya kufanyia utafiti ndani ya glasi unao mfanano na kiumbe hai, inafanywa kikamilifu katika maabara.

Hatua ya pili ni ile ya majaribio kwa panya, na ndicho kiwango amefikia wakati wa kuandika makala haya.

Iwapo Marie Marthe Chabi alifanikiwa kutekeleza hatua hizi mbili kwa kutumia rasilimali chache alizonazo, anahitaji fedha zaidi ili kuendelea na hatua ya mwisho.

"Sitasema uongo, utafiti unahitaji fedha nyingi."

"Kwa sasa, hatujaridhika na aina ya ufadhili tulionao, lakini tunajizatiti na kile tulichonacho," anasema, akibainisha kuwa dhamira yake inabaki kuwa ni kutokana na uzoefu wake binafsi ulioelezwa awali.

Kwa tuzo hii kutoka kwa Taasisi ya L'Oréal-UNESCO, anafurahi, "tuna matumaini kupata ufadhili zaidi ili tuendelee na hatua ya majaribio ya kliniki."

Kushinda changamoto na vikwazo

Katika Afrika ya Kusini mwa Sahara, wanawake wanawakilisha asilimia 31 tu ya watafiti na wanapokea mishahara midogo na mara nyingi hawatambuliwi kama wenzao wa kiume, inasema UNESCO.

"Changamoto ya kwanza tunayokutana nayo ni ukosefu wa fedha, hasa katika Afrika ya Kusini mwa Sahara, Magharibi mwa Afrika, katika nchi yangu," anasisitiza Dkt. Chabi.

"Hivyo, natumai kweli kuwa naweza kuvuta umakini wa watu au taasisi zinazovutiwa na mada hii ili waweze kujitolea na kuniruhusu kuafiki ubora wangu ili kutoa bidhaa halisi inayofanya kazi."

Jambo la pili ni imani binafsi kulingana na mwanafunzi huyu wa sayansi za biolojia.

"Nililazimika kufanya kazi sana na kujipa motisha ili niwe na imani na nafsi yangu na najijua kuwa, kadri ninavyotaka jambo fulani, najitahidi nikiwa na lengo la kulifikia."

Hii ni kweli zaidi, anamini, kwa sababu ubaguzi wakati mwingine ni kikwazo.

"Sijakutana na ubaguzi mwingi ,lakini haina maana hakuna ubaguzi."

"Kila wakati ninachukua kwa umakini ushauri kutoka kwa wazee ambaye huniambia kwamba hata kama nitajitahidi, nitahakikisha kila kitu kiko shwari bado nitakosolewa na hilo nisiweke akilini.''

Kwa falsafa hii, "naendelea na utafiti wangu, bila kujali vikwazo vilivyopo," anahitimisha.

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi