'Nilidhani nitakufa'- mateka aliyeachiliwa na wanamgambo wa Burkina Faso asimulia maisha yalivyokuwa katika kambi

Chanzo cha picha, Michael Mvondo
- Author, Thomas Naadi
- Nafasi, BBC News Accra
- Muda wa kusoma: Dakika 10
Mwanamume mmoja kutoka Ghana aliambia BBC jinsi alivyotekwa na wanamgambo wa nchi jirani ya Burkina Faso ,na kupelekwa katika kambi yao iliyo jangwani na kujua maisha yao yanavyokuwa -kuanzia watoto wao ambao wamepewa mafunzo ya kujitoa uhai kupitia kujilipua na mabomu, mahandaki waliochimba kujihami dhidi ya mashambulizi ya anga na vifaru wa kijeshi.
Katika mahojiano ya kwanza na chombo cha habari tangu kizaazaa kilichomkumba mwaka 2019 ,mwanamume huyo ambaye ni James sio jina lake halisi, anasimulia kuwa haikuwa rahisi kwake katika kambi hiyo kwani makundi ya wanamgambo walitoka vitani huku wakisherehekea kwa kufyatua risasi angani.
'nilidhani huo ndio mwisho wangu. Nilikuwa natiririkwa na jasho,''James anasema ,akiongeza kuwa alienda haja ndogo bila kutarajia baada ya wanamgambo kumgonga na mtutu wa bunduki kisha kumcheka.
James ambaye ana umri wa miaka 30 ,mwenye imani ya dini ya kiasili ya kiafrika ,anasema mamluki hao walijaribu kumshawishi ajiunge nao wakimhadaa kuwa atapata mamlaka na siku za usoni kuwa kamanda wa kikosi hicho cha wanamgambo.
''Wanamgambo walileta gunia.Ilikuwa na silaha za kila aina,AK-47, M16,na bunduki aina ya G3.
Kisha akaniuliza ni gani naweza itumia nikamjibu kuwa sijawahi kutumia silaha yoyote maishani.Akasema; tuna silaha kubwa zaidi,iwapo itatokea utakuwa kiongozi wa kundi moja la wanamgambo hakuna adui atakayekukaribia na kukuumizia,'' James anaongezea .
Aidha anasema ilikuwa ni bahati kuachiliwa huru wiki mbili baadaye baada ya kuwasihi wamuachilie , akidai kuwa aliacha mtoto mgonjwa nyumbani na kumuahidi kamanda kuwa atakuwa kinara wa kuwasajili watu katika harakati ya wanamgambo huko Ghana -ahadi anasema hakuitekeleza.
Tume ya kitaifa ya elimu kwa raia nchini Ghana, ambayo inatoa hamasa kwa vijana kutojiingiza katika kundi la wanamgambo , iliambia BBC kuwa walifahamu kilichomtokea James.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
''Nilikutana naye nikiwa katika pilka pilka za kuhamasisha vijana katika taasisi za anuwai,'' anasema Mawuli Agbenu ambaye ni mkurugenzi katika tume ya mkoa katika jiji la Aacra.
''Tutakuwa na njia ya kumhusisha ili awe balozi na mshawishaji katika jamii yake kuhusu athari za kujiingiza kwa kundi hilo haramu,'' anasema Agbenu.
Taifa la Ghana ambalo limekuwa halina mitikiso ya kundi lililona misimamo mikali ambapo wanamgambo wameongezeka hasa katika nchi jirani ya Burkina Faso na nchi za Afrika magharibi.
Wanamgambo ambao walimteka nyara James ni wa kundi la Jama'at Nusrat al- Islam wal-Muslimin (JNIM), au kundi la msaada kwa waislamu.
Ni wafuasi wa kundi la Al-Qaeda ambalo lilianzishwa mwaka 2017 kama mwavuli wa makundi ya wanamgambo katika eneo hilo.
Nchini Burkina Faso, ni kundi ambalo lina mashiko upande wa kaskazini ,ambapo wanasimamia maeneo makubwa na pia wameshikilia baadhi ya maeneo ya Kusini katika mpaka wa Ghana ulio na urefu wa kilomita 550.
Kwa mujibu wa mashirika ya misaada , zaidi ya watu 15000 kutoka Burkina Faso wamekimbia nchi yao na kutafuta hifadhi katika maeneo ya kaskazini mwa Ghana.
Kando na Burkina Faso , wanamgambo pia wametaka Niger na Mali,na wameshambulia Ivory Coast, Benin na Togo- zote zikiwa koloni za Ufaransa ikiibua wasiwasi kuwa wanaendelea kusogea katika pwani ya kusini .
Mwezi Aprili, afisa mkuu katika Umoja wa Mataifa anasema kuwa ''kitovu cha ugaidi kimehamia kaskazini mwa Afrika na mataifa ya uarabuni , yakizidi katika mkoa wa Sahel ambapo inajumuisha Burkina Faso, Mali na Niger''.
Wanamgambo ambao wanaukuruba na Al-Qaeda na Islamic State(IS) wanaendelea kutekeleza uhalifu wa kivita katika mkoa huo.

Chanzo cha picha, Thomas Naadi/BBC
Afisa wa usalama wa Ghana anayeshika doria mpakani Burkina Faso aliambia BBC kuwa wanamgambo wamekuwa wakivuka Ghana kujisuka upya baada ya kuanza kulemewa na wanajeshi wa Burkina Faso -na ilikuwa kivukio cha ulanguzi wa silaha, chakula na mafuta.
''Sio salama Ghana. Hujificha kwa miji kama vile Pusiga.Wakaazi wanaoishi mpakani wanahofia maisha yao kutokana na kudorora kwa usalama.''aliongezea.
Katika ripoti iliyowasilishwa mwezi Julai, Chuo cha Uholanzi masuala ya mahusiano ya kimataifa kinasema kuwa '; kutokuwa na mashambulizi halisi nchini Ghana ni kutokana na hesabu za Wanamgambo wa JNIM kutotaka kudororesha eneo ambalo huwasambazia bidhaa za kimsingi na pia kutochokoza jeshi ambalo linajivunia kuwa na mafunzo ya haiba ya juu.
Chuo hicho pia kinasema kuna wakati kundi hilo la JNIM lilijaribu kushawishi Jamii ndogo ya Fulani ya waislamu kutekeleza mashambulizi nchini Ghana.
JNIM ilidai kuwa wamekuwa wakiwanyanyapaa, lakini juhudi zao za kuwashawishi kulipua Ghana zilikuwa na "mafanikio madogo" kwani Wafulani walikuwa "wakiijua machafuko ambayo yameikumba Sahel kutokana na mitandao ya kifamilia" na hawakutaka hayo yatokee nchini Ghana, alisema taasisi ya tafiti.
Kiongozi wa kidini wa Kiislamu wa jamii ya Fulani kutoka Burkina Faso, Amadou Koufa, ni mwanzilishi mwenza wa JNIM na ndiye naibu wake mkuu. Anawaajiri wapiganaji wengi kutoka jamii ya Wafulani katika Burkina Faso.
Jeshi limekashifiwa na makundi ya haki za binadamu kwa kulipiza kisasi kwa kuwatuhumu Wafulani, na kufanya mashambulizi yasiyo na ubaguzi dhidi ya vijiji vyao katika Burkina Faso.
Mnamo mwaka 2022, shirika lisilo la kiserikali lililo na mizizi ya Ufaransa, Promediation, lilisema kwamba utafiti wake ulionyesha kuwa magaidi walikuwa wameajiri kati ya vijana 200 hadi 300 kutoka Ghana.
Ingawa baadhi yao walikuwa wakifanya operesheni katika nchi zilizoathiriwa na uasi kama Burkina Faso, wengine walirudishwa kwa vijiji vyao kaskazini mwa Ghana ili kuhubiri misimamo mikali", ilisema taarifa hiyo.
Hii inaweza hatimaye kupelekea magaidi kupata "msimamo endelevu katika maeneo ya mbali na pembezoni mwa kaskazini," ilisema taasisi hiyo.
Tangu 2022, Ghana imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuunda kikosi kipya cha kikanda kilichosaidiwa na Magharibi, chenye wanajeshi 10,000, kukabiliana na wanamgambo.
Tamale - mji mkubwa kaskazini mwa Ghana - ulipaswa kuwa makao makuu ya kikosi hicho.
Hata hivyo, makao makuu hayo hayajafunguliwa bado, na hatma ya mpango huo haijulikani baada ya eneo hilo kugawanyika kati ya nchi zinazounga mkono Magharibi na zile zinazounga mkono Urusi.
Burkina Faso - pamoja na Mali na Niger - zimegeukia Urusi.
Nchi tatu hizi zimeunda muungano wao wa kupambana na waasi, na pia zimetegemea msaada kutoka kwa wahusika wa Kirusi.
Ghana na nchi nyingine za kanda zimebaki katika muungano na Magharibi.
Jeshi la Ghana limeanzisha vituo vya kijeshi kaskazini, lakini vifaa vya uangalizi wa mipaka vilivyowekwa hivi karibuni bado havifanyi kazi, alieleza afisa wa usalama aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Chanzo cha picha, AFP
Baada ya kusafiri kwa kipande cha siku,James anatuelezea kuwa alikutana na wanamgambo wa kaskazini magharibi wa Burkina Faso alipokuwa akikaribia mpaka wa Mali.
Wanamgambo ambao waliokuwa kwa pikipiki walimsimamisha na kumpeleka katika kambi lao ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kina kubaini iwapo alikuwa jasusi na baadaye kumuachilia walipobaini sio mpelelezi,James anasema.
Anatueleza kuwa kitambaa alichofunikwa nacho macho ambacho ni bendera ya wanamgambo kiliondolewa.
James anasema aliwaona wanamgambo 500 ambao wengi wao ni vijana ikiwemo mmoja wao akijitambulisha kama daktari -anayeishi kwa kambi hiyo.
Kambi hiyo ambayo iko jangwani, ilikuwa imeezekwa na makuti, na kuekelewa paneli za nishati ya jua zinazozalisha umeme, alieleza.
Anasema kuwa kambi hiyo ilikuwa imegawanywa sehemu tatu-sehemu ya kamanda na familia zao, wanajeshi wa wanamgambo na sehemu ya tatu ni wanakijiji na wanajeshi waliotekwa nyara.
James anasema alikuwa amezuiliwa katika sehemu hiyo ya mateka lakini alianza kuwa na ukaribu na wanamgambo ndani ya wiki ya pili baada ya kuanza kujionyesha kuwa anaunga mkono wanachokifanya.
Walikuwa wakikaa kwa vikundi vya watu 5 au 10 , na kusikiliza nyimbo za muimbaji Seif Keita, ambaye ni wa kutoka Mali anayefahamika kama sauti ya dhahabu ya Afrika, James anasema.
Baadhi ya wanamgambo wamepiga marufuku muziki akisema kuwa ni haramu katika dini ya kiislamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
James anasema kuwa kambi hiyo ilikuwa na utulivu wa aina yake ,Kundi la wanamgambo hao kila uchao lilikuwa likienda kwa vita ,wakifyatua risasi za kusherehea kuwanyamazisha mahasimu wao wakidai kuwa wamefanikiwa katika mashambulizi yao.
James anasema ilikuwa mara ya kwanza kusikia mlio wa risasi na tangu hapo akafanya mazoea.
Anasema kuwa wanamgambo walikuwa wakiegesha magari yao aina ya pick up katika mahandaki hayo ili kuhakikisha hayajaharibiwa iwapo kulikuwa na mashambulizi ya anga ,ambao baadhi ya magari yalibaki nje ya kambi 'ili kutumika wakati wa dharura.
''Walikuwa wakiwauza wanawake waliowateka nyara.Wengine wanauza wake zao ambao wanahisi wamewachosha .Wale walikuwa wakipinga kuuza walikuwa wakibakwa na kundi,''James anaeleza lakini hakuwahi kushuhudia wazi hilo kufanyika.
James anasema kuwa bibi za wanamgambo walikuwa wanafanya majukumu ya nyumbani kama kupika na usafi huku wanawake waliokamatwa walikuwa wakibakwa na wangine kulazimishwa kuwa wanamgambo.
Anaendelea kutusimulia jinsi alivyoona wanawake waliojistiri mwili mzima wakiwa wamebeba Mabunduki aina ya AK 47 walioyaficha ndani ya nguo zao refu ,wakiondoka kuelekea kwa vijiji vilivyokaribu kuvamia na kuchukua mifugo ambayo ingefanywa vitoweo katika kambi au kuuza katika soko lililo jirani na kambi.
James pia anasema aliona watoto wengi ,ikiwemo wale wa wanamgambo wakipewa mafunzo ya kutumia silaha na vilipuzi.
''Ungeona mtoto mdogo akiwa amebeba bunduki akiniambia kuwa atakapokutana watu hivi ndio atawaua ,''James anasema.
Anasema kuwa si mara moja kuona watoto wanne wakichukuliwa na kupelekwa vitani na wanaporudi wamevalishwa fulana za kujilipua.
Fulana hizo zilikuwa refu kwao na walitoka kambini wakiwa wamebeba vibakuli vya kuombea msaada ,James anasema.
Wanamgambo wanasema kuwa wakitarajia mashambulizi makali wanakoenda huchukua watoto ambao hujitoa mhanga kwa kujilipua ili wawape fursa ya kuingia kukabiliana na maadui katika purukushani hizo.
Isitoshe wanamgambo ambao hutoa watoto wao chambo katika mashambulizi kama hayo hulipwa fidia bada ya kila shambuli,''lakini hawakumwekea wazi ni pesa ngapi kwa kila mtoto.
James anadokeza kuwa walijaribu kumshawishi kwa kumpa maneno ya kufuata misimamo mila; wakitangaza kuwa tamaduni za magharibi ni potofu na pia kumuonyesha video za propaganda kila jioni, ikiwemo moja ya uvamizi wa Marekani nchini Iraq na mauaji ya Wapalestina katika mzozo wa sasa na Israel.
James alisema aliweza kusema waasi wote walikuwa wanazungumza Kifaransa, lakini mmoja aliweza kuzungumza Kiingereza na lafudhi ya Ghana, na alificha uso wake ili asimuone.
Kama ishara pia wanamgambo walikuwa wanafuata nyayo ya muungano wa Afrika , James anasema alisikia wakitaja majina ya vigogo wa Burkina Faso Thomas Sankara na wa kutoka Ghana, Kwame Nkrumah na kumwambia kuwa watu wanapaswa kupinga uongozi mbaya na kujinasua katika unyanyasaji wa serikali.

Chanzo cha picha, AFP
James anasema wanamgambo walieleza kuwa iwapo Sankara na Nkrumah wangekuwa bado wako hai basi bara Afika lingekuwa tulivu -na hakuna muafrika angesafiri Ng'ambo kutafuta maisha mazuri.
James ambaye alikuwa hana bazi wala kazi kipindi hicho anasema kauli hiyo ilimuingia akilini na ni kutokana na uzaledo aliokuwa nao ambao ulimzuia kuingia katika kikosi hicho cha wanamgambo.
Na je ni vipi alitekwa nyara ?,James anasema kuwa marafiki zake wawili wa kiislamu walikuwa wakisafiri naye walimuahidi kumtambulisha kwa kiongozi wa kidini nchini Senegal ambao wangemuombea aimarishe kipato chake cha riziki.
Watatu hao walivamiwa na wanamgambo walipokuwa wakikaribia kufika mwisho wa safari, anasema.
James anasema mmoja wa rafiki yake alipigwa risasi na kuuawa alipojaribu kutoroka huku wenzake wakipelekwa kambini.
James anatuambia kuwa kamanda hakumuachilia rafiki yake na anahofia kuwa huenda alijiunga na wanamgambo hao au aliuawa.
''Kamanda aliniambia kuwa:Nitakuachilia urejee nyumbani iwapo utanihakikishia kuwa utasajili wanamgambo zaidi nchini humo,''James anasema.
Aidha alifikishwa katika ufuo wa mto ambapo alipatiwa nauli ya kurejea nyumbani ,wanamgambo wakimpa namba ya simu ya mtu watakayefanya kazikwa pamoja,lakini James anasema kuwa hakufuata maagizo hayo kwani alibadilisha laini ya simu na kurusha aliyokuwa nayo.
Kulingana na James ,wanamgambo pia walimpa hirizi ambazo walidai zina nguvu za kumkinga.
Hata hivyo wanamgambo wengi walikataa kuvaa hirizi wakisema kuwa ni kinyume cha dini ya kiislamu kushirikisha mungu.
James alituonyesha hirizi ambazo zimeundwa kwa kutumia unyoya , ngozi za wanyama na mitishamba ambazo zimefunikwa na kitambaa cha ngozi.
Ilijumuisha hirizi moja ambayo ilikuwa danganya toto kuwa ingemlinda dhidi ya risasi za adui.
James anasema hakupata ishara kuwa wanagambo walikuwa na nia ya kuvamia Ghana bali walipaona kama mahali salama pa kujificha wanapozidiwa na wanajeshi wa Burkina Faso.
Lengo lao kuu ni kushambulia mataifa ambayo yana raia wa Ufaransa na Marekani wakidai kuwa mataifa haya mawili yanatumia vibaya rasilimali za Afrika huku wakaazi wake wakiumia James anasema.
Hata hivyo hilo limepingwa vikali na mataifa hayo mawili.

Chanzo cha picha, AFP
Mchanganuzi wa masuala ya kijeshi ya Ghana Adib Saani alielezea wasiwasi wake ongezeko la wanamgambo Afrika magharibi na kusema hakuona suluhisho lolote la kijeshi.
''Tunapaswa kuenda zaidi ya utumizi wa majeshi. Tunapaswa kuziba pengo la kiuchumi na siasa mambo leo ambayo imekuwa ikijenga mazingira ya ukuaji wa ugaidi .'' anaiambia BBC.
Tume ya kitaifa ya elimu ya uraia imekuwa ikifanya kampeini za kuhamasisha umma kwa kauli mbiu "see something, say something" ili kuwasihi wakaazi kutoa ripoti kwa idara ya usalama shughuli inayotiliwa shaka.
Kampeni hiyo pia imepanuliwa hadi Accra, ili kuelimisha vijana kuhusu hatari za Ugaidi.
Bwana Agbanu kutoka tume hiyo aliambia BBC kuwa kampeni hiyo ni muhimu kwani Waghana wako katika hatari ya kuajiriwa na wanamgambo.
"Kuna kiwango kikubwa cha rushwa, maendeleo yasiyo sawa kote nchini, na ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana," alisema.
James, ambaye sasa ni mkulima mdogo wa kujikimu, alisema alifurahia kuwa hai kwani kamanda wa waasi alimwambia alikuwa akifanya uamuzi wa kipekee kwa kumwachilia kwa sababu kwa kawaida ilikuwa "au mwili wako uende nyumbani au hakuna atakayejua habari zako tena."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












