Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tume ya uchaguzi Kenya IEBC ilitumia seti ya pili ya fomu za matokeo, ripoti ya mahakama yafichua
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) ilitumia seti ya pili ya fomu za upeperushaji matokeo ambayo ilikubaliana na vyama vya kisiasa kuzifunga katika bahasha zisizoweza kuguswa kabla ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022, ripoti ya Mahakama imefichua.
Mahakama iliamuru kuhesabiwa upya kwa kura katika vituo 15 vya kupigia kura kufuatia ombi la wagombeaji wa Azimio la Umoja Raila Odinga na Martha Karua.
Timu za kiufundi kutoka kwa Idara ya Mahakama zilipewa jukumu la kuandaa ripoti kuhusu kuhesabiwa upya kura, na uchunguzi wa seva za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Kamishna wa IEBC katika hati yake ya kiapo amemkashifu Mwenyekiti Wafula Chebukati kwa kuchapisha kwa siri seti ya pili ya fomu za uwasilishaji matokeo, ambazo zinaonyesha kura alizopata kila mgombeaji katika vituo vya kupigia kura.
Vyama vya kisiasa mnamo Julai vililalamika wakati wa uchapishaji wa seti ya pili ya fomu, na kusababisha IEBC kuwaita kwa mkutano wa mashauriano.
Katika mkutano huo, iliamuliwa kuwa seti ya pili ya fomu hazitatumika katika uchaguzi bali zimefungwa katika bahasha zisizoweza kufunguliwa .
Katika ripoti yake, timu ya Mahakama inasema ilipata vituo tisa ambako fomu za pili za matokeo zilitumika, baadhi zikiwa na hitilafu katika kujumlisha kura zao.
Vituo 15 vya kupigia kura viko katika kaunti za Nandi, Kericho, Mombasa, na Nyandarua. Baadhi ya hitilafu za kujumlisha zilibainika baada ya kuhesabiwa upya kwa kura.
Kwa mfano, katika kituo cha Kericho Chepkutung kura moja ilichukuliwa kutoka kwa kura za Raila Odinga na kupewa William Ruto.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa vituo vingine sita vya kupigia kura vilishindwa kutoa seti zao za fomu 34A za kitabu cha pili.
“Baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walieleza kutokuwepo kwa fomu 34A za kitabu cha 2 kwa kuonyesha kuwa wasimamizi walizitumia badala ya fomu 34 za kitabu cha kwanza.
“Katika hali hiyo timu ilihakiki taarifa hizo kwa kutafuta fomu 34A za kitabu 1 ili kuthibitisha kama ni kweli kwa madhumuni ya uwajibikaji.Sababu iliyotolewa ni kwamba baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walikosea vitabu hivyo viwili kwa sababu hawakuvielewa na utaratibu uliofaa kufuatwa” inasema ripoti hiyo.
Picha ya uchunguzi
Katika uchunguzi wa seva za IEBC, ripoti inasema kwamba vifaa vya kuwatambua wapigakura vinavyotumiwa katika uchaguzi vina programu ambayo hubadilisha picha kuwa muundo wa PDF.
Kufikia wakati zoezi la uhakiki lilikamilika, IEBC ilikuwa haijatoa picha ya kitaalamu ya fomu 34C, hati ya mwisho ya utumaji matokeo ya kura za Urais, kwa timu ya Mahakama.
IEBC, hata hivyo, ilijitolea kuwasilisha picha ya uchunguzi. Picha ya uchunguzi imekusudiwa kusaidia katika kujua jinsi na wakati hati ilijazwa na matokeo.
Ripoti hiyo imewasilishwa kwa majaji wa Mahakama ya Juu ili ikaguliwe, na itajadiliwa siku ya Ijumaa.