Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unaweza kujifunza nini kimaisha kutokana kazi ya muziki ya Burna Boy?
Na Dinah Gahamanyi
BBC News Swahili
Akifahamika kwa jina la usanii kama Burna Boy, Damini Ebunoluwa Ogulu ni muimbaji na mtunzi wa nyimbo Mnigeria anayefahamika hasa kwa mtindo wake wa kipekee wa Afrobeat, R & B, na mitindo mingineyo.
Binafsi anauelezea muziki wake kama Afro-fusion, aina ya muziki ambao unajumuisha midundo ya kiafrika -Afrobeat, dancehall riddims, reggae, rap ya Marekani, na R & B.
Burna Boy ambaye alizaliwa Julai 2 1991 katika Port Harcourt, Jimbo la Rivers, nchini Nigeria ni miongoni mwa wanamuziki wachache wa Nigeria na nje yake ambao wameweza kung’ara kwenye fani ya muziki.
Burna Boy ni muimbaji na mtunzi wa muziki ambaye miondoko yake ni ya kipekee hususan, mtindo wake ukidhihirika tatika albamu yake ya nne “African Giant.” Iliyoachiliwa Julai, 26, 2019 na spaceship Entertainment, bad Habit , Atlantic Records na Warner Music- nembo kubwa katika fani ya muziki duniani.
Albamu yake ni mchanganyiko wa Afrobeat, dancehall riddims, reggae, rap ya Marekani, na R & B.
Sawa na wanamuziki wenzake wa Nigeria kama Kizz, Davido na Naira Marley, Burna Boy ameweza kujinadi kwa aina yake ya ladha ya muziki katika sekta ya muziki ya Nigeria. Hii imemuwezesha kujishindia tuzo mbali mbali za kitaifa na kimataifa kama Tuzo ya Grammy kitengo cha Albamu ya muziki bora duniani, mwaka 2021.
lakini je ni mambo gani unayoweza kujifunza ya kimaisha na ya kimuziki kwa Burna Boy?
Kufanya mambo ya kipekee na kuyaendeleza
Burna Boy anafahamika kwa mtindo wake wa kipekee wa Afrobeat. Anafananishwa Mfalme wa Afrobeats, Fela Anikulapo Kuti, ambaye alikuwa na aina yake ya muziki wa wa mapigo ya kiafrika ambao ulikuwa ni utambulisho wake. Ndivyo ilivyo kwa Burna Boy unaposikia mapigo na sauti yake bila shaka utagundua ni Burna Boy hata kama haujamtizama.
Anafahamika kwa kuendeleza mtindo wake katika mapigo ya Afrika-Afrobeat na pia kwa kushikilia aina fulani ya kasi ya mapigo na hilo huifanya kazi yake kuwa ya kipekee.
Ukweli ni kwamba hakuna mwanamuziki mwingine Mnigeria ambaye anacheza mtindo wake wa muziki, na hilo limejenga upekee wake kimuziki.
Katika moja ya nukuu za Burna Boy kuhusu maisha , alisema : “kwangu mimi, kila mradi ninaoufanya ni tofauti, unastahili lengo tofauti .”
Hii inadhihirika kwenye kila kazi anayoifanya Burna Boy.
Kuwa mkweli, na uwe halisi
Hii pia inaweza kumaanisha ‘’kuwa halisi’’ – au uasilia. Burna Boy anafahamika kwa tungo za maneno yake yenye ukweli.
Huwasilisha ukweli kuhusu jamii katika kazi yake, hata katika colabo anazozifanya, mfano ni ile aliyoifanya na DJDS ‘’Steel and Cooper’’
Kuwa na shauku ya kile unachokifanya na kukifanya kwa ufasaha
Tofauti na wasani wengine, Burna Boy amechagua kutozungumzia mapenzi, mahusiano au pesa.
Sio kwamba mambo hayo ni mabaya kabisa, bali aliipeleka Afrobeat katika kiwango tofauti. Hutupeleka katika katika safari ambapo hutupa hadithi, au picha au kutatua matatizo mfano ya kijamii, kisiasa na mengineyo, hilo ni jambo ambalo analipenda sana.
Kuwa na malengo ya juu
Katika kuendeleza shauku ya mambo unayoyapenda, azma ya utekelezaji wake pia inakufanya uyafanye mambo hayo kwa kiwango bora zaidi hata wakati unapokuwa huwezi kufanya vyema zaidi.
Burna Boy hakufanya kazi yake kwa lengo la kushinda tuzo za nchini Nigeria; aliteuliwa kwa Tuzo ya Grammy kabla ya wasanii wengine maarufu wa muziki. Ingawa Tuzo hiyo ilimwendea mwanamuziki mkongwe Angeliue Kidjo, mtindo wake wa muziki ulikuwa unafahamika tayari kimataifa.
Katika mojawapo ya nyimbo zake ulioitwa ‘’Dangote’’, alimsaidia kila mtu kuangalia uwezekano wa kufanya mambo na kuwa na malengo hata ya juu zaidi. Shauku husaidia kurejesha imani.
Kuleta mabadiliko yenye athari
Hakuna yeyote anayeweza kuzungumzia kuhusu muziki nchini Nigeria na athari zake kwa jamii bila kumtaja Burna Boy.
Hii ni kwasbaabu mwanamuziki huyu si nyota tu bali ni nyota mwenye kuleta athari kwa kutumia muziki wake. Hutumia mtindo wake wa muziki kuwaleta watu hususan Wanigeria wanaoishi ughaibuni nyumbani… kwenye asili yao. Alifanya hivyo na kuweza kutambuliwa kwa kiwango cha kimataifa.
Mawasiliano
Mawasiliano ni jambo muhimu sana inapokuja katika suala la mafanikio ya nyanja zote maishani. Nyimbo za Burna Boy kila mara huwa na ujumbeambao anataka kuufikisha kwa wanaomsikiliza.
Katika wimbo wake ‘’Africa giant’’ anaelezea matatizo yanayoisumbua nchi yake na kuwasiliana na serikali kujaribu kutafuta suluhu.
Ingawa sio wa kwanza kuimba kuhusu masuala hayo, ni yeye aliyeweza kutambuliwa. Kila unanolifanya tafuta njia ya kuwasiliana kwa undani zaidi na hadhira yako.
Jiamini kwa kile unachokifanya na ikibidi jisifie unapofanya kazi yako vyema
Ingawa watu wengi hawapendi kujisifia, ni hulka ya binadamu kupenda kusifiwa wakati mwingine anapofanya vyema. Wakati mwingine si vibaya kusema mbele ya wale unaowahudumia au unaowatumbuiza kwamba una imani uko vizuri katika jambo unalolitenda.
Kujisifu kunasaidia kuinua ari ya mtu ya kufanya kazi. Na hili limedhihirishwa na Burna Boy ambaye amekuwa akiwaambia mashambiki wake hasa awapo jukwani kwa kuwauliza ni nani anayeimba vizuri kulingana na midundo au beats - kati yake na pruducer?