Wairan wanaosherehekea Pasaka kisiri

    • Author, Na Sara Monetta
    • Nafasi, BBC News

Juu ya meza sebuleni, Tina - si jina lake halisi - amefanya onyesho na miali ya chai, mayai ya rangi, mishumaa na msalaba mdogo wa mbao. Ni njia yake mwenyewe, ya karibu ya kuashiria Pasaka.

Yeye na mume wake walibadili dini na kuwa Wakristo miaka mingi iliyopita, jambo ambalo katika nchi yao ya Iran, limekatazwa kisheria.

Wanaweza kukamatwa wakati wowote.

Katiba ya Iran inatambua dini ndogo ndogo. Wakristo wa Armenia na Ashuru wanaweza kufuata dini zao, lakini wamepigwa marufuku kuwahubiria Wairan wengine au hata kuwaruhusu kuingia makanisani mwao.

Wale walioachana na Uiisilamu na kugeukia Ukristo, wanaweza tu kuzingatia imani yao kwa siri, katika yale yanayoitwa makanisa ya nyumbani. Tina ni mmoja wao.

Mamlaka zimekuwa zikiimarisha mashambulizi dhidi ya makundi hayo, kuwakamata baadhi ya watu na kuwapa vifungo virefu zaidi, hivyo washiriki wa makanisa wanalazimika kuchukua tahadhari zaidi.

"Tunakutana katika vikundi vidogo na kila wakati katika sehemu tofauti," Tina anasema. "Inaweza kuwa nyumbani kwa mmoja wa wanachama wetu au wakati mwingine hata kwenye bustani au kwenye gari wakati wa kuendesha gari. Ni salama zaidi ikiwa kila kikundi kinafahamu machache iwezekanavyo kuhusu wengine, kwa hiyo ikiwa kikundi kimoja kitajipata mashakani, wengine wasihusishwe."

Kuishi na tishio la mara kwa mara la kugunduliwa na kufungwa, ni changamoto, anasema. Wkati mwingine, watoto wake wanasema shuleni au kuwaambia marafiki zao kwamba wazazi wao ni Wakristo.

Tina amewahi kuitwa na shuleni na kukaripiwa mara kadhaa kuhusiana na hilo.

Anasema pia mume wake, ambaye anafanya biashara, amelaghaiwa na watu ambao wamejua kuhusu dini yake.

Na bado, anajihesabu kuwa na bahati - hawajakamatwa hadi sasa. Lakini wengine wengi wamejipata mashakani.

Mehdi - sio jina lake halisi - amekamatwa mara mbili. Mara ya kwanza, alikuwa na miaka 20.

Anasema aliwekwa katika kifungo cha upweke, akihojiwa mara kwa mara na kutishiwa.

Lakini hatawahi kusahau kukamtwa kwa mara ya pili akiwa na umri wa miaka 24, kwani ilimuathiri sana.

"Nilikuwa katika kifungo cha upweke kwa zaidi ya mwezi mmoja," ananiambia.

"Mahojiano yalikuwa makali zaidi, na yalikuwa yakiendana kila jambo. Hatukuweza kuiona familia yetu na hatukujua ni kwa muda gani tutakuwa pale. Kila tukiwauliza walicheka tu na kusema 'usijali kuhusu hilo, utakuwa hapa kwa muda'."

Mehdi alizuiliwa gerezani kwa miaka mitatu, tukio ambalo anasema lilimtatiza mara kwa mara.

Alishtakiwa kwa mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na 'kutishia usalama wa taifa' - uhalifu wa kisiasa ambao ulimaanisha kwamba alipoachiliwa, hangeweza kurejelea maisha yake ya zamani.

"Unapokabiliwa na shutuma hizi za kisiasa, moja kwa moja unakuwa raia wa daraja la pili au la tatu," anasema. "Popote unapotaka kwenda kufanya kazi au kusoma, una lebo ya kisiasa, ambayo inafanya maisha kuwa magumu sana kwako.''

Anasema alikuwa chini ya uangalizi wa karibu kila mara, na alihofia kukamatwa tena wakati wowote.

"Ilikuwa ngumu sana kwa familia yangu," anasema. "Kila wakati nikienda nje hata kununua kitu kwa mfano, waliogopa kwamba sitarudi."

Mwishowe, familia yake ilimshawishi kuikimbia Iran na kuomba hifadhi katika nchi jirani ya Uturuki.

Kulingana na shirika lisilo kiserekali Kifungu cha 18, ambacho kinatetea Wakristo nchini Iran, watu wasiopungua 166 walikamatwa mwaka jana, ongezeko kutoka 2022, wakati 134 walikamatwa.

Dhamana zimekuwa ghali zaidi, na mara nyingi hazipatikani. Na hukumu za jela zimekuwa ndefu zaidi.

Mehdi ananiambia kwamba alipopewa kifungo chake cha miaka mitatu, ndicho kilikuwa kifungo kirefu zaidi ambacho Mkristo yeyote katika jiji lake aliwahi kupata. Lakini sasa, anasema, vifungo vya miaka 10 au hata 15 vinatolewa kwa Wakristo.

"Ukandamizaji mkali dhidi ya upinzani wowote ni sera ambayo serikali imeendelea kutekeleza licha ya ukosoaji mkubwa," anaelezea Mansour Borji, mwanzilishi na mkurugenzi wa Ibara ya 18.

Mamlaka ya Iran iliongoza msururu wa kukamatwa kwa Wakristo katika miezi kadhaa kabla ya kumbukumbu ya kifo cha Mahsa Amini - msichana aliyekufa akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili wa Iran ambao walikuwa wamemshtaki kwa kutovaa hijabu yake ipasavyo.

Mwezi Machi, ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa uligundua kwamba kifo chake kilisababishwa na unyanyasaji wa kimwili aliofanyiwa na kwamba taifa la Iran liliwajibika kwa hilo.

Wakati wa kifo chake, maandamano ambayo hayajawahi kutokea yaliikumba nchi. Vijana wa kike walichoma hijabu zao barabarani huku wengine wakipiga makofi, kuimba na kucheza.

Takriban waandamanaji 551 waliuawa katika msako wa polisi. Maelfu walikamatwa. Wanaume tisa waliuawa na kunyongwa, na wengine sita kwa sasa wanakabiliwa na hatima kama hiyo.

Katika hali hii, dini ndogo pia hazikusazwa, lakini Mansour anasema kwamba - licha ya yote hayo - watu wengi wamesalia kuwa wakaidi. Na hiyo pia inamaanisha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaobadili dini.

"Idadi ya wale wanaojitambulisha kuwa Wazoroastria ni kubwa," Mansour anaeleza, akimaanisha mojawapo ya dini kongwe zaidi ulimwenguni iliyoanzishwa miaka 3,000 iliyopita huko Uajemi, ambayo sasa inajulikana kama Iran.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi