Kwa nini BBC haiwaiti 'magaidi' wanamgambo wa Hamas- John Simpson

Person holding gun standing on a tank

Chanzo cha picha, getty image

Mawaziri wa serikali, waandishi wa safu za magazeti, watu wa kawaida - wote wanauliza kwanini BBC haisemi wapiganaji wa Hamas waliotekeleza ukatili wa kutisha kusini mwa Israel ni magaidi.

Jibu linarudi kwenye kanuni za msingi za BBC.

Ugaidi ni neno lililosheheni, ambalo watu hutumia kuzingatia wasichokikubali kimaadili. Siyo kazi ya BBC kuwaambia watu nani wa kumuunga mkono na nani wa kumshtumu - ni nani wazuri na nani ni wabaya.

Mara kwa mara tunaeleza kwamba Uingereza na serikali nyinginezo zimeshutumu Hamas kama shirika la kigaidi, lakini hiyo ni biashara yao. Pia tunafanya mahojiano na wachambuzi na wachangiaji wanaotoa nukuu zao ambao wanaelezea Hamas kama magaidi.

Jambo kuu ni kwamba hatusemi kwa sauti zetu. Biashara yetu ni kuwasilisha kwa hadhira yetu ukweli, na kuwaruhusu wafanye maamuzi yao wenyewe.

Kama inavyotokea, bila shaka, watu wengi ambao wametushambulia kwa kutotumia neno Ugaidi wameona picha zetu, kusikia matangazo yetu kwa njia ya sauti au kusoma taarifa zetu, na kufanya maamuzi yao kwa msingi wa ripoti zetu, kwa hivyo, siyo kana kwamba tunaficha ukweli kwa njia yoyote – huo sio ukweli.

Mtu yeyote mwenye busara atashangazwa na aina ya kitu ambacho tumeona. Ni busara kabisa kuyaita matukio ambayo yametokea "ukatili", kwa sababu ndivyo ilivyo.

Hakuna anayeweza kutetea mauaji ya raia, hasa watoto na hata watoto wachanga - wala mashambulizi dhidi ya watu wasio na hatia, wapenda amani ambao wanahudhuria tamasha la muziki.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa muda wa miaka 50 nimekuwa nikiripoti matukio ya Mashariki ya Kati, nimejionea mwenyewe matokeo ya mashambulizi kama haya ya Israeli, na pia nimeona matokeo ya mashambulizi ya mabomu na mizinga ya Israeli dhidi ya raia huko Lebanon na Gaza. Hofu ya mambo kama hayo hukaa akilini mwako milele.

Lakini hii haimaanishi kwamba tuanze kusema kuwa shirika ambalo wafuasi wake wametekeleza ni shirika la kigaidi, kwa sababu hiyo itamaanisha kwamba tunaacha wajibu wetu wa kubaki katika malengo.

Na imekuwa hivi kila mara katika BBC. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, watangazaji wa BBC waliambiwa waziwazi kutowaita Wanazi kuwa waovu, ingawa tunaweza kuwaita "adui".

"Zaidi ya yote," ilisema nyaraka ya BBC kuhusu haya yote, "lazima kuwe hakuna nafasi ya kuwa na machungu". Toni yetu ilipaswa kuwa ya utulivu na yenye utaratibu.

Ilikuwa vigumu kudumisha kanuni hiyo wakati IRA ilipokuwa ikishambulia kwa mabomu Uingereza na kuua raia wasio na hatia, lakini tulifanya hivyo.

Kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa serikali ya Margaret Thatcher kwa BBC, na kwa waandishi binafsi kama mimi kuhusu hili - hasa baada ya shambulio la bomu la Brighton, ambapo aliepuka kifo na watu wengine wengi wasio na hatia waliuawa na kujeruhiwa.

Lakini tulishikilia taratibu zetu. Na bado tunafanya hivyo, hadi leo.

Hatuko upande wowote. Hatutumii maneno mazito kama vile "uovu" au "mwoga". Hatuzungumzii "magaidi". Na sio sisi pekee tunaofuata taratibu hii. Baadhi ya mashirika ya habari yanayoheshimiwa sana ulimwenguni yana sera sawa kabisa.

Lakini BBC inapata uangalizi maalum, kwa sababu tuna wakosoaji wenye nguvu katika siasa na vyombo vya habari, na kwa sehemu ni kwa sababu tunashikilia viwango vya juu sana katika kazi yetu.

Lakini sehemu ya kuendeleza kiwango hicho cha juu cha utendaji ni kuwa na malengo kadri inavyowezekana.

Ndiyo maana watu nchini Uingereza na duniani kote, kwa idadi kubwa, hutazama, kusoma na kusikiliza kile tunachosema, kila siku.

Awali, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Grant Shapps alisema sera hiyo "inaelekea kufedhehesha".

Hata hivyo, msemaji wa BBC alibainisha kuwa ni msimamo wa muda mrefu kwa wanahabari wake kutotumia neno hilo wenyewe isipokuwa kama wanalihusisha na mtu mwingine.

Mwandishi mkongwe wa BBC wa masuala ya kigeni John Simpson alisema "kumwita mtu gaidi ina maana unachukua msimamo".

Lakini Bw Shapps alisema BBC inahitaji kupata "dira yake ya maadili".

"Kwa kweli nadhani inaelekea kwenye aibu, wazo hili kwamba kuna aina fulani ya usawa, na watasema kila wakati, kuna pande mbili," aliiambia LBC.

Alisema Hamas, ambao "wameenda na kuwachinja watu wasio na hatia, watoto wachanga, wahudhuria tamasha, wastaafu", ni shirika lililopigwa marufuku nchini Uingereza - ikimaanisha kuwa serikali inaliona rasmi kama shirika la kigaidi ambalo ni kinyume cha sheria kuunga mkono.

"Hao sio wapigania uhuru, sio wanamgambo, kwa lugha rahisi kabisa ni magaidi na inashangaza kwenda kwenye tovuti ya BBC na bado unaona wakizungumza kuhusu watu wenye silaha na wapiganaji na sio kuwaita magaidi," Bw Shapps alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje James Cleverly na Waziri wa Utamaduni Lucy Frazer pia wamelitaka shirika la utangazaji BBC kurekebisha sera yake, huku kiongozi wa chama cha Labour Sir Keir Starmer akisema BBC "inahitaji kueleza kwa nini haitumii neno hilo."

"Nilisema 'ugaidi' na 'gaidi', na kwangu hilo ndilo tunaloshuhudia," Bw Starmer aliambia LBC.

Msemaji wa BBC alisema: "Siku zote tunachukulia matumizi yetu ya lugha kwa uzito sana.

“Yeyote anayetazama au kusikiliza matangazo yetu atasikia neno ‘gaidi’ likitumika mara nyingi – tunalihusisha na wale wanaolitumia, kwa mfano, Serikali ya Uingereza.

“Hii ni mbinu ambayo imekuwa ikitumika kwa miongo kadhaa, na inaendana na ile ya watangazaji wengine.

"BBC ni kituo huru cha utangazaji na kazi yake ni kueleza kwa usahihi kile kinachotokea ili watazamaji wetu waweze kufanya uamuzi wao wenyewe."

Je, miongozo ya BBC inasemaje?

Miongozo ya wahariri wa shirika hilo inasema neno "gaidi" linaweza kuwa "kizuizi badala ya msaada wa kuelewa".

Wanasema: “Tunapaswa kufahamisha hadhira yetu matokeo kamili ya kitendo hicho kwa kueleza kilichotokea.

"Tunapaswa kutumia maneno ambayo yanaelezea haswa mhusika kama vile 'mshambuliaji', 'mvamizi' 'mtumiaji wa bunduki', 'mtekaji nyara', 'muasi' na 'mpiganaji'.

"Hatupaswi kutumia lugha ya watu wengine kama yetu; jukumu letu ni kubaki na lengo na kuripoti kwa njia zinazowezesha watazamaji wetu kufanya tathmini zao wenyewe kuhusu nani anafanya nini na kwa nani."