Mambo manne yanayochochea mzozo wa Israel na Palesitina

WESD

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Hamas wanasema kuna sababu kadha za shambulio hilo

Shambulio lililoanzishwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba lilikuwa kubwa na limekuja ghafla, lakini limetokea kutokana na miongo kadhaa ya mvutano kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Hamas inasema kuna sababu kadhaa nyuma ya shambulio hilo. Kwa miaka mingi Israel na Palestina zimekuwa katika mzozo, maeneo manne ambayo yanafanya mzozo huo uzidi kuwa mkali:

Gaza

RTHFG
Maelezo ya picha, Kukatika kwa umeme hutokea kila siku katika ukingo wa Gaza

Ukanda wa Gaza una urefu wa kilomita 41 na upana wa kilomita 10 na unapatikana kati ya Israel, Misri na Bahari ya Mediterania. Ni makazi ya takriban watu milioni 2.3, ni eneo lenye msongamano mkubwa zaidi wa watu duniani.

Takriban asilimia 80 ya wakazi wa Gaza wanategemea misaada ya kimataifa, kulingana na Umoja wa Mataifa, na takriban watu milioni moja wanategemea msaada wa chakula kwa kila siku.

Hii ina maana kwamba maisha ya kila siku ya watu wanaoishi huko ni magumu, na kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, mwaka 2021 umeme hupatikana Gaza kwa masaa 13 tu kwa siku.

Shirika la Afya Duniani linasema kila mtu anahitaji lita 100 za maji kwa siku kwa ajili ya kunywa, kuosha, kupika na kuoga, wakati wastani wa matumizi ya maji Gaza ni lita 88 kwa mtu.

Israel inadhibiti anga ya Gaza na ukanda wake wa pwani, na imeweka vikwazo kwa bidhaa zinazoruhusiwa kuingia na kutoka kupitia vivuko vya mpaka wake. Kadhalika, Misri inadhibiti kinachoingia na kutoka katika mpaka wake na Gaza, kwa sababu za kiusalama.

Katika kukabiliana na shambulio la wikendi, serikali ya Israel imetangaza "kuizingira Gaza na kuzuia upatikanaji wa chakula, maji na mafuta.

Gaza imekuwa chini ya udhibiti wa Hamas tangu mwaka 2007, wana mgambo hao waliwafukuza wanajeshi waliokuwa watiifu kwa mamlaka iliyokuwa ikitawala wakati huo ya Palestina.

Mwaka wa 2014, kufuatia mzozo mfupi na Hamas, Israeli ilitangaza kulitenga eneo la Gaza ili kujilinda kutokana na mashambulizi ya roketi na uvamizi wa wanamgambo.

Msikiti wa Al-Aqsa

EWDS
Maelezo ya picha, Msikiti wa Al-Aqsa ni moja ya eneo takatifu katika Uislamu
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Msikiti wa Al-Aqsa kwa muda mrefu umekuwa chanzo cha mvutano kati ya Waisraeli na Wapalestina huko Jerusalem Mashariki.

Katika rekodi ya sauti iliyotolewa wakati wa shambulio la hivi sasa, Muhammad al-Deif, kamanda wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi ya Al-Qassam, alisema mapigano hayo yamekuja kujibu kile alichokiita "mashambulio ya kila siku dhidi ya Al-Aqsa" na Waisraeli ambao humtukana Mtume wetu ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa."

Katika miaka ya hivi karibuni, wahafidhina wa Israel wameongeza ziara zao kwenye eneo la misikiti, jambo ambalo limewatia wasiwasi Wapalestina. Msikiti huo mara nyingi hushuhudia mapigano kati ya waumini wa Kipalestina na vikosi vya usalama vya Israel.

Aprili mwaka jana, polisi wa Israel walivamia msikiti huo kwa kutumia maguruneti na risasi za mpira baada ya mzozo kuhusu shughuli za kidini. 2021 uvamizi wa Israeli ulizusha mzozo mkubwa wa siku 11 kati ya Israeli na Hamas.

Osama Hamdan, mwakilishi mkuu wa Hamas nchini Lebanon, aliambia BBC kwamba walikuwa na wasiwasi kuhusu nia ya serikali ya Israel juu ya eneo hilo, akisema mabadiliko yoyote yatamaanisha "kuvuka mstari mwekundu."

Makaazi ya Walowezi

WEFDFC
Maelezo ya picha, Makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo yanayozozaniwa ni chanzo cha mvutano wa Israel na Palestine

Tangu Israel iikalie kwa mabavu ardhi yaPalestina baada ya vita vya mwaka 1967, idadi ya makaazi ya walowezi wa Kiyahudi yameendelea kuongezeka, na Umoja wa Mataifa unakadiria - takriban Wayahudi 700,000 wanaishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu hadi 2022.

Umoja wa Mataifa na nchi nyingi zinachukulia makaazi hayo kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel haikubaliani na hilo.

Mwaka huu kumekuwa na ongezeko la ghasia zinazofanywa na walowezi wa Israel wenye itikadi kali dhidi ya raia wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi, huku matukio zaidi ya 100 yakiripotiwa kila mwezi kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Kulingana na Osama Hamdan wa Hamas, Wapalestina wanahofu Israel "inapanga kuwafukuza kutoka Ukingo wa Magharibi."

Mahusiano ya Waarabu na Israeli

TRFG

Chanzo cha picha, DPA

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (mwenye suti nyeusi)

Israel inadumisha uhusiano wa kidiplomasia na majirani zake wawili wa Kiarabu, Misri na Jordan, baada ya kusaini mikataba ya amani 1979 na 1994. Lakini katika miaka ya hivi karibuni imefungua mazungumzo na nchi nyingine za kikanda kama vile UAE.

Septemba iliyopita, Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman aliiambia runinga ya Fox News ya Marekani - nchi yake inapiga hatua kila siku kurekebisha uhusiano na Israel.

Ingawa Saudi Arabia hapo awali ilieleza makubaliano yoyote yatahitaji maendeleo kuelekea kuanzishwa kwa taifa la Palestina, Hamas inapinga hatua hiyo, ikisema kurekebisha uhusiano na Israel kutapunguza shinikizo la kutambua madai ya Wapalestina.

Katika hotuba ya televisheni Oktoba 7, Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas, alikosoa nchi za Kiarabu kuchukua msimamo wa maridhiano na taifa la Kiyahudi.

Alisema: "Mikataba yote ya ushirikiano ambayo mataifa hayo yamesaini na Israel hayawezi kutatua mzozo huu."