Jinsi muswada tata wa fedha 2023 utakavyoathiri maisha ya Mkenya

Na Abdalla Seif Dzungu

Huku wabunge wakitarajiwa kupitisha muswada tata wa kifedha wa 2023, muswada huo umeendelea kuzua pingamizi na uungwaji mkono miongoni mwa Wakenya licha ya kamati ya bunge kuhusu fedha na mipango kudai kwamba mazuri ya msaada huo yanazidi mabaya.

Lengo la serikali kuwasilisha muswada wa sheria ya fedha ni kukusanya mapato zaidi ili kuendesha shughuli zake.

Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 ambao utaletwa bungeni kwa usomaji wa tatu siku ya Jumanne tarehe 20 mwezi Juni 2023, ambapo utajadiliwa na kupigiwa kura ya mwisho, unalenga kurekebisha sheria mbalimbali zinazohusiana na kodi.

Muswada huo pia unakuja kufuatia madai ya mafisa wakuu wa Serikali kwamba Serikali haina fedha kwasababu sehemu kubwa ilisimamiwa vibaya na Serikali iliyopita.

Hata hivyo huku serikali ya Kenya kwanza ikipanga kuvamia zaidi mifuko ya walipa kodi, inabidi ifanye uamuzi kati ya kuwakamua walipata kodi wake ambao iliwaahidi kutowatoza ushuru zaidi lakini wakati huo huo ikihakikisha kwamba inatii ahadi iliyowapa Wakenya wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Haya yanajiri huku muungano wa upinzani Azimio ukisema kuwa utaleta marekebisho kadhaa wakati muswada huo utakapowasili bungeni.

Lakini je serikali inalenga vipi kujipatia mapato kutoka kwa walipa kodi?

Tozo ya Makazi

Wafanyikazi wanaweza kupoteza pesa zao katika Hazina ya Makazi yenye utata ikiwa Bunge litaidhinisha pendekezo jipya la kufuta kifungu kinachoitaka Serikali kuwarejeshea wachangiaji ambao watakosa nyumba za bei nafuu baada ya miaka saba.

Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango imependekeza marekebisho katika Muswada wa Sheria ya Fedha, 2023 ili kubadilisha mfuko wa nyumba kuwa tozo, jambo ambalo lina maana kwamba fedha hizo hazitarejeshwa baada ya kukusanywa.

Maafisa wa serikali, akiwemo Rais William Ruto, wamesisitiza kuwa mapato ya nyumba za bei nafuu sio ushuru bali ni mchango sawa na ule wa Hazina ya Kitaifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Ili kuwaridhisha walipa ushuru, kamati ya bunge imepunguza mchango huo kutoka asilimia 3.0 iliyopendekezwa hadi asilimia 1.5, lakini ikaubadilisha kuwa ushuru, ambao sasa utakusanywa na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) pamoja na ushuru mwingine.

Serikali ya Rais William Ruto inataka kujenga nyumba kama sehemu ya mtindo wake wa kiuchumi kutoka chini kwenda juu, ikisema kuwa mpango huo utatoa nyumba kwa wanaoishi katika vitongoji duni na kutoa ajira kupitia ujenzi wa nyumba 250,000 kila mwaka.

Wakosoaji, hata hivyo, wanasema kwamba tozo hiyo itapunguza mshahara wa wafanyikazi ambao tayari wanakabiliana na shinikizo la mfumuko wa bei.

Katibu Mkuu wa chama cha Orange Democratic Edwin Sifuna alikashifu mswada huo akisema Serikali inashughulikia vipaumbele visivyofaa kwa Wakenya.

Sifuna ambaye alikuwa akizungumza katika kituo kimoja cha habari nchini alisema kuwa serikali ilifaa kuboresha mishahara ya Wakenya kabla ya kuwatoza ushuru zaidi.

Bwana Sifuna aliongezea kwamba tozo hiyo ya nyumba ya 1.5% itaathiri ajira kwani waajiri watalazimika kupunguza idadi ya wafanyikazi huku wengine ambao hawawezi kudhibiti ushuru huo wakilazimika kufunga virago na kuhamia mataifa yanayotoza ushuru wa kadri .

Kupanda kwa VAT kwenye Mafuta

Pendekezo la Rais William Ruto la kurejesha ushuru wa asilimia 16 wa ongezeko la thamani kwa bidhaa za petroli limefichua tofauti kati ya ahadi zilizotolewa dhidi ya hatua zinazochukuliwa huku Wakenya wakionesha ghadhabu zao.

Hazina ya Kitaifa imependekeza kuwa kuanzia Julai 1, bei ya VAT kwa bidhaa za petroli itapanda kutoka asilimia 8 ya sasa iliyopitishwa wakati wa uongozi wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta hadi asilimia 16.

Hata hivyo, wakati wa kampeni za Rais Ruto, aliahidi kushughulikia gharama ya juu ya maisha badala ya kuwatoza ushuru mkubwa Wakenya ambao alisema walikuwa wanatozwa ushuru kupita kiasi.

Sekta ya uchukuzi nchini ndiyo inayoongoza kwa matumizi makubwa ya mafuta ya petroli ikichukua takriban asilimia 68.7 ya ujazo wote wa mafuta ya petroli.

Kuongezeka kwa VAT kwenye mafuta kutasababisha moja kwa moja kuongezeka kwa gharama zote zinazohusiana na uzalishaji, usindikaji na usafirishaji wa bidhaa za chakula.

Hii itaathiri bei za bidhaa za kimsingi kama vile chakula na hivyo kuathiri kila makaazi nchini.

Hivi majuzi serikali ya Kenya Kwanza ilifutilia mbali ruzuku ya petroli siku chache tu baada ya Rais William Ruto kusema ruzuku hazikuwa endelevu.

Katika hotuba yake baada ya hafla ya kuapishwa mnamo Septemba 13, Ruto alisema ruzuku imekuwa ya gharama kubwa na inaweza kutumika vibaya, ikiwa ni pamoja na kusababisha upungufu bandia wa bidhaa za ruzuku.

Waundaji wa maudhui ya kidijitali

Asilimia 5 ya malipo yatakayotolewa kwa waundaji wa maudhui ya kidijitali yatachukuliwa na serikali kama tozo baada ya serikali kukubali kupunguza ushuru huo kutoka asilimia kumi na tano iliyokuwa imependekezwa awali.

Mswada huo pia unatoa ufafanuzi mpana zaidi wa uundaji wa maudhui ya kidijitali kwa kueleza uchumaji wa mapato wa maudhui ya kidijitali kama toleo la nyenzo za burudani, kijamii, za kisanii au za elimu kwa madhumuni ya malipo.

Asilimia 35 ya ushuru kwa watu wanaopata mapato zaidi ya Sh500,000- Mswada umependekeza tozo la juu zaidi kutoka kwa watu wa kipato cha juu kwa kuanzisha bendi mpya ya ushuru ya asilimia 35 ya watu ambao mapato yao ya kila mwezi yanazidi Sh500,000 au Sh6 milioni kila mwaka.

Mswada huo utaongeza chandarua cha PAYE kutoka kwa watu wa kipato cha juu huku mapato yao ya mwezi yakipungua ikilinganihswa na Mkenya wa kipato cha chini ya fedha hizo.

Ushuru wa bidhaa

Mswada huo unalenga kuipa mamlaka ya kutoza ushuru KRA kulazimisha baadhi ya makampuni katika sekta fulani kulipa ushuru mara moja.

Washikadau katika sekta ya michezo ya kubahatisha kwa mfano wanatakiwa kutuma ushuru ndani ya saa 24.

Hivi majuzi, serikali ilisema halmashauri hiyo ina mpango wa kuajiri maafisa 6,604 zaidi katika kipindi cha miaka mitatu ili kuongeza mapato ya ziada ya Sh1 trilioni kutoka kwa walaghai wa kodi kama vile wakwepaji ushuru na wamiliki wa nyumba.

Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) inafanya jaribio lingine la kuongeza wafanyikazi wake hadi kufikia viwango vya wafanyikazi 14,555 kutoka wafanyikazi 7,955 wa sasa.

Hii ina maana kwamba wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wamekuwa hawalipi kodi kama vile mama mboga na hustlers watalazimika kulipa kodi.

Hii ni kinyume na ahadi ya serikali ya kuyawezesha makundi hayo katika kipindi cha kampeni za uchaguzi

Vipodozi- Nywele za binadamu, mawigi, ndevu , nyusi, kope na kucha bandia pia zitaanza kuvutia ushuru kwa kiwango cha asilimia tano.