Waziri wa Israel azua mgogoro kwa kupendekeza ujenzi wa sinagogi katika msikiti wa al-Aqsa

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa siasa za mrengo wa kulia nchini Israel Itamar Ben-Gvir amezua mgogoro baada ya kupendekeza kujenga sinagogi katika ardhi ya msikiti wa al -Aqsa mjini Jerusalem.
Jordan, ambayo inashikilia usimamizi wa Jamii ya Wahashemite kwenye maeneo matakatifu ya Kiislamu huko Jerusalem chini ya Mkataba wa Wadi Araba wa 1994, ilijibu kwa kusema kwamba "Msikiti uliobarikiwa wa Al-Aqsa/Al-Haram Al-Sharif na eneo lake lote la dunam 144 ni mahali pa ibada kwa ajili ya Waislamu pekee.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan ilisema kupitia msemaji wake, Sufyan Al-Qudah, kwamba "Utawala wa Wakfu wa Jerusalem na Utawala wa Masuala ya Msikiti wa Al-Aqsa, wenye mafungamano na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Jordan na Maeneo Matakatifu, ndio chombo cha kisheria chenye mamlaka ya kipekee kusimamia mambo yote ya eneo hilo takatifu udhibiti kuhusu ni nani anayefaa kuingia eneo hilo.”
"Kama ningeweza kufanya chochote ninachotaka, ningeweka bendera ya Israel kwenye eneo hilo," Ben-Gvir alinukuliwa akisema na Agence France-Presse katika mahojiano na kituo cha redio cha jeshi la Israel Gali, akizungumzia kuhusu uwanja wa Msikiti wa Al-Aqsa.
Wapalestina na Israel walaani kauli za Ben Gvir
Katika kujibu swali ambalo mwandishi wa habari alimuuliza Ben-Gvir zaidi ya mara moja kuhusu kama angejenga sinagogi kwenye eneo la msiki ti wa Al- aqsa kama angeweza, waziri huyo wa mrengo wa kulia alijibu, "Ndiyo.
Taarifa hii iliifanya ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kujibu tena kwa kusema, "Hakuna mabadiliko katika hali iliyopo kwenye Mlima wa Hekalu."
Wengine pia walikosoa kauli za Ben-Gvir.
Waziri wa Ulinzi Yoav Galant alichapisha kwenye akaunti yake ya X kwamba "kupinga hali iliyopo kwenye Mlima wa Hekalu ni kitendo cha hatari, kisicho cha lazima na cha kutowajibika."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliongeza: "Vitendo vya Ben Gvir vinahatarisha usalama wa Taifa la Israel."
Kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid alisema kwenye jukwaa la X kwamba matamshi ya mara kwa mara ya Ben Gvir yanaonyesha kuwa "Netanyahu amepoteza udhibiti wa serikali yake."
Wayahudi wanaita eneo ambalo Msikiti wa Al-Aqsa upo "Mlima wa Hekalu" na wanalichukulia kuwa eneo takatifu zaidi la kidini. Vikosi vya Israel vinadhibiti viingilio kwenye msikiti huo ambao unasimamiwa na Idara ya Wakfu ya Kiislamu ya Jordan.
Chini ya "hali ilivyo," wasio Waislamu wanaweza kutembelea Msikiti wa Al-Aqsa kwa nyakati maalum bila kufanya sala na ibada za kidini huko, ambazo baadhi ya Wayahudi wa Orthodox wakati mwingine hukiuka.
Wapalestina na Wizara ya Wakfu ya Jordan wanachukulia ziara za Wayahudi katika Msikiti wa Al-Aqsa kama "uchokozi" wa hisia za Waislamu.
Wakati wa mahojiano, Ben-Gvir alisema, "Waarabu wanaweza kuomba wakati wowote wanataka, hivyo Wayahudi wanapaswa pia kuwa na uwezo wa kuomba wakati wowote wanataka."
Kulingana na Ben-Gvir, "sera ya sasa inaruhusu Wayahudi kusali kwenye eneo hilo," kama ilivyoripotiwa na AFP
Kwa upande wake, msemaji wa Ikulu ya Palestina, Nabil Abu Rudeineh, alizitaja kauli za Ben Gvir kuwa ni hatari sana na kusema kuwa Al-Aqsa na maeneo matakatifu ni mstari mwekundu, na hatutakubali kuguswa hata kidogo."
Hamas ilisema kauli za Ben-Gvir ni "tangazo la hatari."
Kwa mujibu wa taarifa ya vuguvugu hilo, "ukiukaji" wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Jerusalem si lolote bali ni "sera inayomwaga mafuta zaidi kwenye moto."
Jordan ilitoa wito wa "msimamo wazi wa kimataifa wa kulaani na kukabiliana naye (Ben Gvir)."

Chanzo cha picha, AFP
Jordan na Misri zatoa kauli yao
Taarifa hiyo ilimnukuu msemaji rasmi wa wizara hiyo, Safia Al-Qudah, akisema, "Jordan itachukua hatua zote zinazohitajika kukomesha mashambulizi kwenye maeneo matakatifu, na kwamba inatayarisha nyaraka muhimu za kisheria kuchukua hatua katika mahakama za kimataifa dhidi ya mashambulizi kwenye maeneo matakatifu, ambayo yanajumuisha ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na ongezeko la hatari ambalo Jordan itakabiliana nalo kwa njia zote zinazowezekana."
Misri kwa upande wake imelaani vikali matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel kuhusu mpango wa kujenga sinagogi la Kiyahudi ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa, na ikaongezea kuwa ni "kutowajibika," kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri.
Katika mazungumzo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdel Aati na mwenzake wa Jordan Ayman Safadi walionya juu ya hatari ya kuendeleza kile walichokitaja kuwa "ukiukaji wa Israel" wa maeneo matakatifu mjini Jerusalem.
Mawaziri hao wawili wamesisitiza, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, haja ya kuheshimu hali ya kisheria na kihistoria iliyopo katika maeneo matakatifu.
Mawaziri hao wawili walishutumu vikali kauli walizozitaja kuwa za itikadi kali ,wakichukulia kuwa ni "ukiukaji" wa sheria za kimataifa, na "haukubaliki."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, "mawaziri hao wawili walionyesha kupinga sera hizi za itikadi kali zinazotaka kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya Jerusalem na maeneo yake matakatifu.
Mawaziri hao wawili walisisitiza, katika wito huo, kwamba kufikia usitishaji vita mara moja ili kupunguza ongezeko la hatari katika eneo hilo, ambalo linaweza kusababisha vita vya kikanda.
Imatafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












