Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mambo ya kutisha yalitokea'-Ndani ya kanisa la TB Joshua lenye simulizi za kuogofya
- Author, Na Charlie Northcott na Helen Spooner
- Nafasi, BBC News, Africa Eye
TB Joshua, kiongozi wa Nigeria mwenye mvuto wa moja ya makanisa makubwa zaidi ya kiinjili duniani, alitenda uhalifu wa kingono kwa siri kwa kiwango kikubwa, uchunguzi wa BBC katika mabara matatu umegundua. Ushuhuda kutoka kwa watu kadhaa walionusurika unaonyesha kuwa Joshua alikuwa akiwanyanyasa na kuwabaka wanawake vijana kutoka kote ulimwenguni mara kadhaa kwa wiki kwa karibu miaka 20.
Onyo: Ina simulizi za mateso, ubakaji na kujidhuru
Mwanzoni mwa 2002, katika kina cha msimu wa baridi nchini Uingereza , Rae mwenye umri wa miaka 21 alitoweka.
Mara ya mwisho marafiki zake wengi walimwona alikuwa chuo kikuu huko Brighton. Alikuwa akisomea usanifu wa picha, akiishi katika nyumba ya pamoja dakika 25 kutoka baharini. Rae alikuwa mwerevu na maarufu.
"Kwangu mimi, ilikuwa kama alikufa, lakini sikuweza kumuomboleza " anasema Carla, rafiki mkubwa wa Rae wakati huo.
Carla alijua ni wapi Rae alienda. Lakini ukweli wa jambo hilo ulikuwa mgumu kueleza marafiki zao. Wiki chache zilizopita, yeye na Rae walikuwa wamesafiri kwenda Nigeria pamoja, kutafuta mtu wa ajabu ambaye angeweza kuponya watu kwa mikono yake. Alikuwa mchungaji Mkristo, mwenye ndevu nyeusi, katika mavazi meupe. Jina lake lilikuwa TB Joshua. Wafuasi wake walimuita “Mtume”.
Rae na Carla walipanga kutembelea kanisa lake, Synagogue Church of All Nations [Scoan], kwa juma moja tu. Lakini Rae hakuja nyumbani. Alikuwa amehamia katika boma la Joshua.
“Nilimwacha pale,” anasema Carla, huku machozi yakitiririka ."Sitawahi kujisamehe kwa hilo."
Kanisa linaonekana kama hekalu la kale juu ya kitongoji cha Ikotun huko Lagos, jiji kubwa zaidi la Afrika. Joshua alitengeneza ghorofa zote 12 za jumba lililopakana nayo, ambapo aliishi pamoja na wafuasi wake wengi. Alisimamia ujenzi wa ngazi nyingi za chumba chake cha kulala. Milango mitatu ya kuingia ndani ya chumba hicho, ndani na nje. Chumba cha maombi kilichofichwa kilichojaa vioo vidogo na "kliniki" ya chini.
Tumewahoji zaidi ya watu 25 waliokuwa wakiishi ndani. Wanatoa taswira ya picha ya jengo kubwa kama jitu; ulimwengu wa jinamizi ambapo ukweli ulipotea na mambo ya kutisha yakatokea.
Wanawake wengi wanasema walishambuliwa kingono na Joshua, huku baadhi wakidai kuwa walibakwa mara kwa mara wakiwa wamefungiwa. Wengine wanasema walilazimishwa kutoa mimba baada ya kupata ujauzito.
Leo, Rae amerudi Uingereza, akiishi katika kitongoji kizuri mashambani. Anatabasamu na anacheka kwa uhuru, lakini kuna jambo lisilotulia juu yake.
"Kwa nje anaonekana kawaida, lakini sivyo," anasema.
Wakati Rae anazungumza kuhusu miaka yake huko Lagos, midomo yake inabana. Anaongea akipumua. Wakati fulani, rangi inajitokeza kwa uso wake. Aliishi miaka 12 ndani ya boma la Joshua.
"Hadithi hii ni kama simulizi ya kutisha. Ni kama kitu unachokitazama kwenye tamthiliya, lakini ni kweli."
Uchunguzi huo wa miaka miwili, kwa ushirikiano na jukwaa la kimataifa la vyombo vya habari Open Democracy, umehusisha zaidi ya waandishi wa habari 15 wa BBC katika mabara matatu. Walikusanya kumbukumbu za rekodi za video, hati, na mamia ya saa za mahojiano ili kuthibitisha ushuhuda wa Rae na kufichua hadithi zaidi za kutisha. Zaidi ya mashahidi 25, kutoka Uingereza, Nigeria, Ghana, Marekani, Afrika Kusini na Ujerumani, wametoa maelezo ya jinsi ilivyokuwa ndani ya boma la Joshua, na matukio ya hivi karibuni zaidi katika mwaka wa 2019.
Kanisa la Synagogue Church of All Nations halikujibu madai hayo, lakini lilisema madai ya hapo awali hayana msingi.
Wafuasi wa zamani hapo awali walijaribu kuzungumzia unyanyasaji, lakini wanasema wamenyamazishwa au kudharauliwa na Scoan, na wawili wanasema walipigwa. Wakati kipindi cha BBC Africa Eye kilipokuwa kikipiga picha nje ya kanisa, mlinzi alipiga risasi juu ya vichwa vya wafanyakazi baada ya kukataa kutoa nyenzo zao.
Wengi wa waliohojiwa wameondoa haki yao ya kisheria ya kutokujulikana, mara nyingi wakiomba tu majina yao ya ukoo yaachwe. Wengine waliuliza kwamba utambulisho wao ubaki siri kwa kuogopa kulipizwa kisasi.
Mwanamume aliyeongoza Scoan anachukuliwa kuwa mmoja wa wachungaji wenye ushawishi mkubwa katika historia ya Afrika. Alikufa, ghafla mnamo Juni 2021, siku chache baada ya mahojiano yetu mengi ya kwanza kurekodiwa. Siku ya mazishi yake, shughuli za mji wa Lagos zilisimama huku umati wa waombolezaji ukifurika barabarani.
Takriban watu 50,000 walihudhuria ibada za Joshua kila wiki, na kanisa likawa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea Nigeria. Himaya yake ya kimataifa ya televisheni na mitandao ya kijamii ilikuwa miongoni mwa mitandao ya Kikristo yenye mafanikio zaidi duniani, huku mamilioni ya watazamaji wakienea Ulaya, Amerika, Kusini Mashariki mwa Asia na Afrika. Kituo chake cha YouTube kilikuwa na mamia ya mamilioni ya watazamaji .
Kanisa bado ni maarufu leo, likiongozwa na mjane wake Evelyn na timu mpya ya wanafunzi.
Mahojiano na bintiye Nelson Mandela mwaka 2013 yanaonyesha picha ya Joshua akiwa amekaa kwenye meza ya rais wa zamani wa Afrika Kusini. Katika maisha yake, Joshua alivutia wanasiasa na watu mashuhuri kwenye kanisa lake, wakiwemo magwiji wa michezo kama mshambuliaji wa Chelsea, Didier Drogba na takriban marais tisa wa Afrika.
Kwa usaidizi na taarifa kuhusu unyanyasaji wa kingono, tafadhali wasiliana na Mtandao huu waBBC Actionline nchini Uingereza. Na kwa habari zaidi juu ya madhehebu, tafadhali tazama The Family Survival Trust
Wafuasi wake wengi walivutiwa na ufadhili wake, lakini wengi wao walikuja kwa kile kinachoitwa miujiza yake. Joshua alirekodi kwa utaratibu "uponyaji" wa kuvutia katika maisha yake yote. Baada ya Joshua kuwaombea, watu binafsi kwenye kamera walitoa ushuhuda wa kuponywa magonjwa kama saratani na VVU/Ukimwi, kipandauso na upofu wa kudumu.
"Hatujawahi kuona kitu kama hicho hapo awali," anasema Solomon Ashoms, mwandishi wa habari anayeangazia dini ya Kiafrika.
"Siri alizokuwa nazo, siri alizobeba, [ndizo] ambazo watu walifuata."
Video kadhaa za Joshua zinaonyesha wanaume walioambukizwa vibaya sehemu za siri, ambazo zilipasuka na kupona kimiujiza anapoinua mkono wake katika maombi. Nyingine zinaonyesha wanawake wanaohangaika kuzaa, ambao huzaa watoto wao papo hapo Joshua anapokaribia. Baada ya kila tukio, wale waliohusika wangeshuhudia kuokolewa.
Kanda za video za uponyaji wa Joshua zilikuwa zikisambaa miongoni mwa makanisa ya kiinjilisti kote Ulaya na Afrika mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Rae, ambaye alikua na maadili ya Kikristo ya kihafidhina, alitiwa moyo kusafiri hadi Lagos baada ya kutazama video hizi, alizoonyeshwa na mtu anayefahamiana na Afrika Kusini.
"Nilikuwa nashikiriki mapenzi wa jinsia moja na sikutaka kuwa," anasema. "Nilifikiri: 'Vema, labda hili ndilo jibu la matatizo yangu. Labda mtu huyu anaweza kuninyoosha. Kama akiniombea, sitakuwa mpenzi wa jinsia moja tena."
Mwanamke mwingine wa Uingereza, Anneka, kutoka Derby, katika Midlands, anasema pia alivutiwa na video hizo.
"Chumba kizima kilitulia," anasema, akielezea wakati waumini wa kanisa lake walipokutana na kanda hizo kwa mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka 16.
“Hivi ndivyo Yesu angefanya,” anakumbuka akiwaza. Yeye, pia, aliendelea na safari hadi Nigeria.
Hakuna kati ya Rae au Anneka, wala vijana wengi walioondoka katika nchi zao ili kukutana na Joshua katika miaka ya mapema ya 2000, hawakulipia tikiti zao. Vikundi vya makanisa kote Uingereza vilichanga pesa za kutuma mahujaji huko Lagos kushuhudia miujiza hii - na Joshua alichangia pesa za Scoan mwenyewe, wadadisi wakuu wa zamani wa kanisa wanasema. Baadaye, mara tu kanisa lilipokuwa thabiti , alitoza bei za juu kwa mahujaji kuja kukaa.
Bisola, Mnigeria ambaye aliishi kwa miaka 14 ndani ya boma hilo, anasema kuwachumbia watu wa Magharibi ilikuwa mbinu kuu.
"Aliwatumia wazungu kuuza chapa yake," anasema.
Wadadisi wa zamani wanakadiria Joshua alitengeneza makumi ya mamilioni ya dola kutoka kwa mahujaji na njia zingine za pesa - kuchangisha pesa, mauzo ya video, na maonyesho ya uwanja nje ya nchi. Alijitoa kutoka kwa umaskini na kuwa mmoja wa wachungaji matajiri zaidi Afrika.
'Mtu huyo [alikuwa] gwiji," anasema Agomoh Paul, mwanamume aliyewahi kuchukuliwa kama namba mbili wa Joshua katika kanisa, ambaye aliondoka baada ya miaka 10 katika boma hilo.
"Kila kitu ... [alichofanya] kilipangwa."
Sehemu kubwa ya upangaji huu ilikuwa kughushi "miujiza" anasema Agomoh Paul, ambayo anasema aliisimamia.
Yeye na vyanzo vingine vinasema kwamba wale "walioponywa" mara nyingi walikuwa wakilipwa kufanya au kutia chumvi dalili zao kabla ya uponyaji wao unaodhaniwa kufanyika. Katika baadhi ya matukio, wanasema, watu walikuwa wamenyweshwa dawa bila kujua au kupewa dawa za kuboresha hali zao wakiwa kanisani, na baadaye kushawishiwa kutoa ushuhuda kuhusu kupona kwao. Wengine walidanganywa kuwa walikuwa na VVU/UKIMWI na kwamba, kutokana na huduma za Joshua, sasa walikuwa hawana virusi.
Rae alipotua kwenye joto kali la Lagos, aliona miujiza pia. Makumi ya watu walikuja na kushuhudia kuwa wameponywa magonjwa makubwa.
"Nilikuwa na majibu ambayo sikutarajia. Nilibubujikwa na machozi," anasema.
Hapo ndipo Rae alipochaguliwa. Joshua alimteua kuwa "mwanafunzi" - kundi la wafuasi waliomtumikia na kuishi naye ndani ya boma lake.
Rae alifikiri angesoma chini ya Joshua, ili "kutibu" jinsia yake, kujifunza jinsi ya kuponya watu.
Ukweli ulikuwa tofauti sana.
"Sote tulifikiri tuko mbinguni, lakini tulikuwa jahanamu," anasema. "Na katika jahanamu mambo ya kutisha hutokea."
Kumi na sita kati ya wanafunzi wa zamani tuliowahoji, akiwemo Rae, walitoa ushuhuda wa moja kwa moja wa unyanyasaji wa kingono au ubakaji na Joshua. Wengi wanasema ilitokea mara kwa mara - kama vile mara mbili hadi nne kwa wiki - kwa muda wao katika boma lake. Baadhi walielezea ubakaji wa kikatili ambao uliwaacha wakihangaika kupumua au kuvuja damu.
Wengi waliamini ni wao tu ndio walikuwa wanashambuliwa na hawakuthubutu kushiriki kile kinachowapata na wanafunzi wengine, kwani wote walitiwa moyo kuripoti kila mmoja.
Kulingana na Victoria, ambaye alituomba tubadilishe jina lake kwa sababu za usalama, na ambaye aliishi kwa zaidi ya miaka mitano katika boma hilo, waathiriwa wengine wa unyanyasaji wa kingono mara nyingi walichaguliwa na Joshua kutoka kanisani.
Anasema alichaguliwa akiwa anahudhuria shule ya Jumapili ya kanisa hilo, na anasema alibakwa katika nyumba ya kibinafsi ya Joshua miezi michache baadaye, baada ya wazazi wake kumweka chini ya uangalizi wake. Kisha aliajiriwa kama mwanafunzi mkazi.
Victoria anasema Joshua aliamuru baadhi ya wanafunzi wake wa Nigeria walioaminiwa kusaidia kutambua waathiriwa wapya. Kikundi hiki kilijulikana kwa njia isiyo rasmi kama "idara ya uvuvi" na anasema hatimaye ilimlazimisha kujiunga.
Mwanafunzi mwingine aliyehusika katika uandikishaji kama huo alikuwa Bisola.
"TB Joshua aliniomba nimtafutie mabikira... Ili aweze kuwaleta kwenye kundi la wafuasi wake wa karibu waliokuwa kama wanafunzi wake na kuvunja ubikra wao', anasema.
Alishiriki kwa sababu ya "mafunzo" na vitisho vya vurugu, anasema, akiongeza kuwa yeye mwenyewe alibakwa mara kwa mara na Joshua.
Baadhi ya wanawake wanasema walikuwa na umri wa chini ya umri wa idhini ya kisheria - ambayo ni 18 katika jimbo la Lagos - wakati waliponajisiwa au kubakwa. Kosa hili linaweza kusababisha hukumu ya kifo nchini Nigeria.
Jessica Kaimu, ambaye sasa ni mwandishi wa habari nchini Namibia, anasema alikuwa na umri wa miaka 17 tu na bikira wakati Joshua alipombaka kwenye bafu la nyumba yake ya kifahari, ndani ya wiki chache baada ya kuwa mfuasi.
"Nilikuwa nikipiga kelele na alikuwa akininong'oneza sikioni kwamba niache kujifanya kama mtoto... niliumia sana, sikuweza kulia," anasema.
Jessica anasema mkutano kama huu ulirudiwa tena na tena, katika muda wote wa miaka mitano aliyokaa kama mfuasi. Simulizi yake inaakisi ya wanawake wengine waliozungumza na BBC, na pia simulizi za watumishi wanne wa kiume wa Joshua ambao walipewa kazi ya kuondoa ushahidi wa kimwili wa unyanyasaji huu.
Maelezo mengi ya simulizi za waliohojiwa ni ya kutisha sana kuweza kuchapishwa. Ni pamoja na simulizi nyingi za moja kwa moja za wanawake waliovuliwa nguo, na kubakwa kwa vitu - ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja ambaye anasema ilimtokea mara mbili kabla ya umri wa miaka 15.
"Ilikuwa uchungu sana, alinidhulumu," mwanamke huyo, ambaye aliomba kutotajwa jina, anasema. "Maneno hayawezi kueleza ipasavyo. Ilinitia makovu maishani."
Baadhi ya waliohojiwa ambao wanasema walibakwa na kupewa mimba na Joshua, wanaeleza jinsi walivyopewa pia mimba za kulazimishwa kuzitoa ndani ya boma - katika eneo linalojulikana kama "idara ya matibabu" au "kliniki".
"Yote yalifanywa kwa usiri," anasema Sihle, mfuasi wa zamani wa Afrika Kusini, ambaye anasema alitoa mimba mara tatu kwa lazima kanisani.
"Unapewa mchanganyiko wa kunywa na unaugua. Au wanaweka vipande hivi vya chuma kwenye uke wako na kutoa chochote. Na hujui kama [kwa bahati mbaya] vinatoa mfuko wako wa uzazi."
Sihle alilia katika mahojiano yake yote, kama vile Jessica ambaye anasema alipewa mimba tano za kulazimishwa.
Bisola anasema alishuhudia "dazeni" za utoaji mimba katika miaka yake 14 ndani ya kanisa. Wakati fulani, anasema angepanda hadi orofa ya juu zaidi ya boma na kulia, akimsihi Mungu amwokoe.
Wanafunzi walimhudumia kila haja yake. Walimfanyia masaji, wakamsaidia kuvaa, wakapuliza manukato alipoingia chumbani. Walimwekea glavu za plastiki mikononi mwake ili aweze kula chakula chake bila kugusa hata chembe.
Badala ya kumwita kwa jina lake, wote walitiwa moyo kumwita "daddy". Sio jambo geni kwa mchungaji wa Kinigeria katika mila ya Kipentekoste kuitwa hivi, lakini wanafunzi wanasema lilikuwa jina ambalo Joshua alisisitiza.
"Akili yangu ilikuwa kama imetikisika," anasema Anneka. "Hakukuwa na uwazi wa utambuzi hata kidogo... Ukweli ulipotoshwa kabisa."
Muundo wa kimaumbile wa kiwanja cha jengo hilo ulizidisha kuchanganyikiwa kwao.
"Ilikuwa msururu wa ngazi," anasema Rae.
Mnamo 2014, ujenzi ulisababisha maafa. Nyumba ya wageni ya ghorofa sita iliyojengwa kwa ajili ya wageni wa kimataifa iliporomoka na kusababisha vifo vya takriban watu 116.
Ripoti ya serikali ya mtaa iliyofuata ilipata kushindwa kwa muundo na kazi duni ya ujenzi kuwa sababu ya kuporomoka. Hakuna mtu aliyewahi kufunguliwa mashitaka.
Baadhi ya waliohojiwa walituambia wanaamini kuwa idadi ya waliofariki ni kubwa zaidi kuliko ilivyoripotiwa, wakieleza kwamba idadi ya raia wa Nigeria ambao walikuwa wakifanya kazi kwenye nyumba hiyo ya wageni hawakuorodheshwa kama waathiriwa na kwamba washiriki wa kanisa walishindwa kujaribu kuokoa na kuficha miili usiku. .
Wanasema Joshua pia alizuia huduma za dharura kusaidia juhudi za uokoaji mara moja, akijali jinsi sifa yake ingevyoonekana machoni pa umma.
Mshiko wake kwenye mawasiliano ulikuwa mkali kila wakati, vyanzo vyetu vinasema.
Rae anasema ni baada tu ya kuondoka ndipo alipogundua kuwa familia yake na marafiki walikuwa wakimtumia barua pepe. Hakuwahi kuzipokea.
Joshua alizuia wanafunzi na wafuasi kufikia simu na akaunti za barua pepe, waliohojiwa wanasema.
"Alitaka kudhibiti kila mtu, kila kitu," anasema Agomoh Paul. "Kile alichokuwa akitafuta sana [ilikuwa] udhibiti wa akili za watu."
Wanafunzi wanasema walilazimishwa kufanya kazi, bila malipo, kwa saa nyingi kila siku - wakiendesha mambo yote ya kanisa kuu. Wote wanasema kuwanyima usingizi lilikuwa jambo la kawaida, huku taa zikiwashwa kwenye mabweni usiku.
Anneka anasema hawakuwahi kulala zaidi ya saa nne kwa wakati mmoja.
Ikiwa mtu yeyote angekamatwa akilala bila ruhusa, au kuvunja sheria nyingine zozote za Joshua, angeadhibiwa. Wanafunzi kumi na tisa wa zamani walielezea kushuhudia mashambulizi ya kikatili au mateso ndani ya boma, yaliyotekelezwa na Joshua au kwa amri yake.
Wanafunzi wengine walielezea kuvuliwa nguo na kuchapwa wenyewe, kwa nyaya za umeme na mjeledi wa farasi unaojulikana kama koboko. Miongoni mwa wale wanaodaiwa kulengwa kwa njia hii ni wanafunzi waliofunzwa wenye umri wa miaka saba.
Kiwanja huko Lagos kilikuwa na kuta zenye urefu wa futi 3.7 na walinzi wenye silaha. Lakini kilichowaweka wanafunzi pale ni uaminifu-mshikamanifu aliouzalisha, na woga wenye mizizi iliyopandikizwa na Joshua juu ya kile ambacho kingewapata ikiwa wangetoroka.
"Ilikuwa gereza la kisaikolojia," anasema Rae. "Ni vigumu sana kuelewa jinsi mtu anaweza kupitia unyanyasaji wa kisaikolojia hadi kupoteza mawazo yake muhimu."
"Scoan inaafikia vigezo vya kuitwa dhehebu lenye itikadi kali' anasema Dk Alexandra Stein, msomi katika Chuo Kikuu cha Sussex na mwanachama wa The Family Survival Trust, ambayo huongeza ufahamu wa umma wa vikundi kama hivyo.
Amekumbana na manusura wengi wa Scoan, na anasema Joshua aliwatenga waathiriwa wake, na kuwaweka katika "michakato ya kudhibiti kwa nguvu ya dhiki, hofu, hatia na aibu". Anaongeza hii ilimaanisha kuwa waliogopa sana kuondoka. Wahojiwa wote wa BBC walizungumza juu ya "kuosha ubongo", "kufundishwa" na "kudhibiti akili" - na wengi walielezea maisha kama mwanafunzi chini ya Joshua kama kuwa katika "ibada".
Rae anasema kwake, ni mateso ya kisaikolojia ambayo yameacha makovu makubwa zaidi. Anasema Joshua alimpa adhabu ijulikanayo kama "adobe" kwa miaka miwili, ambapo alikatazwa kutoka nje ya boma, na hakuna mtu ndani aliyeruhusiwa kuzungumza naye.
"Kimsingi nilikuwa nimetengwa kabisa ... nilikuwa na shida kamili," anasema. "Nilijaribu kujiua mara tano."
Katika kusukumwa ukingoni, kuna kitu kilipasuka akilini mwa Rae. Miaka kumi na miwili ya kufundishwa ilianza kufunguka.
"Alifanya makosa makubwa, alishindwa kunidhibiti," anasema.
Alipokuwa akisafiri na kanisa katika ziara ya kwenda Mexico, Rae alitoroka kutoka kwa wanafunzi. Yeye kamwe hakurudi nyuma.
Maisha yake sasa ni tofauti sana. Lakini anapaswa kuishi na hali ya kukata tamaa kwamba hakuna njia ya kumwajibisha Joshua.
"TB Joshua akifa kabla ya kukabiliwa na haki kwa ukatili aliofanya, imekuwa ya kufadhaisha sana. Imeongezwa tu na hisia mbaya ya ukosefu wa haki inayohisiwa na sisi sote kama waathiriwa wake."
Tuliwasiliana na Scoan na madai hayo katika uchunguzi wetu. Hawakuwajibu, lakini walikanusha madai ya awali dhidi ya TB Joshua.
"Kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Nabii TB Joshua si jambo geni... Hakuna madai yoyote yaliyowahi kuthibitishwa," waliandika.
Ripoti ya ziada ya Maggie Andresen, Yemisi Adegoke na Ines Ward
End of Unaweza Pia Kusoma
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah