Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini viatu hutundikwa kwenye nyaya za umeme mitaani?
- Author, MARIAM MJAHID
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa vijana wengi nchini Kenya, hasa wale wanaoishi katika mitaa ya mabanda, kupata nafasi ya pili, fursa ya kurekebisha makosa ya zamani na kurejea kwenye njia sahihi, ni changamoto kubwa.
Kwa muda mrefu, jamii imekuwa ikiwatenga vijana hawa, ikiwaita wale waliokosa mwelekeo na kutowapa nafasi ya kujirekebisha.
Ni mtindo wa maisha ulioenea kwa miaka mingi – njia rahisi ya kuelewa matatizo na kuyakabili – lakini ambao sasa umefanya vijana katika mitaa duni ya jiji kuu la Nairobi kuwa na hamu ya kurekebisha maisha yao yaliyovurugika kutokana na uhalifu.
Katika kutafuta uthibitisho wa uwezo wa kujirekebisha, na kuaminisha jamii msemo wa Mui huwa Mwema vijana hawa wamejenga picha ya matumaini kwa kuchagua alama moja, kitu cha kawaida kilichojificha kwa muda mrefu, lakini kimekuwa kikiashiria mapambano, ustadi, na kujitolea.
Utamaduni wa kutundika viatu
Viatu vinavyotundikwa kwenye nyaya za umeme na nyaya za simu vimekuwa na utata mkubwa duniani kote.
Vimezungukwa na siri na wasiwasi, na katika jamii nyingi, vinahusishwa na mambo ya uovu.
Nchini Marekani na sehemu za Amerika ya Kusini, viatu hivi mara nyingi vinahusishwa na magenge ya uhalifu, yakionyesha mipaka yao na maeneo yao au himaya wanayotawala.
Vilevile, katika sehemu nyingi, viatu hivi hutumika kama alama isiyo rasmi ya kumbukumbu ya mahali ambapo mwanachama wa genge aliuawa.
Hata hivyo, kwa vijana hawa wa Nairobi, kiatu si tu alama ya vurugu.
Badala yake, ni ishara ya nguvu na matumaini.
Viatu vinavyoning'inia kwenye nyaya za umeme katika mitaa ya mabanda iliyo viungani mwa jiji la Nairobi vimekuwa picha ya kawaida huku wengi wakipuuza viatu hivyo vimefikaje hapo na baadhi kutojisumbua kujua kiini cha viatu hivyo kuwa hapo.
Katika mtaa huu wa mabanda kilomita 6.6 magharibi kusini mwa jiji la Nairobi ni mtaa unaojulikana kama Kibra ambao una makazi ya Soweto.
Ni eneo ambalo limekuwa likishuhudia kadhia ya uhalifu na uvunjaji sheria.
Viatu hivi vilivyoning'inizwa katika nyaya za umeme ama stima zinakumbukumbu kwa wakaazi kuhusu wahalifu ambao waliangamia baada ya arubaini yao kutimia au wahalifu waliobadilika kuwa wema na kuamua kuchuma kihalali.
Kwao, kiatu kilichotundikwa juu ni zaidi ya alama ya zamani ya machafuko; ni ishara ya kuibuka kutoka kwenye maovu na kujenga mustakabali mpya.
Omondi amebahatika kuwa hai.
Wakati alipokuwa mui anaelezea alivyoamua kubadilika na jinsi kuning'iniza viatu kuna maana tofauti kwa sehemu mbalimbali.
Kwa mtaa huu wa Soweto desturi hii hutumika kama ukumbusho wa mara kwa mara kwa wahalifu waliobadilika katika uhalifu.
Ni kupitia jazanda ya kiatu ambapo wahalifu wanaweza kufuta maisha yao ya zamani.
''Kutundika mabuti (viatu) ni alama ya ushindi. Mimi mwenyewe ni shahidi. Wengi huitumia kutangaza wamebadilika kuwa wema na wameacha uhalifu. Mimi nililitundika buti yangu miaka 10 iliyopita na kila ikipita eneo hili na kuona buti langu inanikumbusha maisha yangu ya uhaifu,'' ananieleza Omondi.
Na kwa matukio tofauti mhalifu anayepatikana akitekeleza wizi na kuuliwa na raia huvuliwa kiatu chake na kuangikwa kwa nyaya za umeme iwe funzo kwa wengine wanaohangaisha wakaazi,
''Wakati mmoja wetu ameuawa, ilikuwa lazima tuchukue kiatu chake iwe nikama kumbukumbu kwetu kuhusu maisha yake. Na kama ana familia hasa watoto wangeonyeshwa viatu vya babake wakitimia umri muafaka'' Omondi anaeleza.
Kwa kuwa ni kawaida kula kiapo kwa kuinua Biblia, wao huning'iniza buti zao kwenye nyaya za umeme kuaminisha jamii wamebadilisha mienendo.
Vijana hawa waliodanganya kifo na kubadilika sasa wamechukua njia tofauti za kuchuma riziki huku wengine wakijikusanya kwa makundi na kuanzisha eneo la kuosha magari.
Nchi nyingine ambazo zina mtindo kama huu
Na sio Kenya pekee mabuti hutundikwa kwa nyaya za umeme au stima.
Katika taifa jirani la Tanzania kuna baadhi ya sehemu ambazo viatu vinatundikwa pia kwenye nyaya za umeme.
Lakini kwa eneo hili, ina maana tofauti na ile ya Kenya.
Kuna mitizamo inayokinzana kidogo Tanzania, kuna wale wanaosema yanaashiria kuwa eneo hili kuna biashara haramu ya uuuzaji wa dawa za kulevya.
'Inasemwasemwa kwamba ukiona viatu vimetundikwa mahali kwenye nyaya za umeme ujue inapatikana ngada (dawa za kulevya) katika eneo hilo, lakini hakuna mwenye uhakika', anasema Aziz Charles mkazi wa Salala
BBC haiwezi kuthibitisha maoni hayo. Lakini kuna wale wanaosema kutundika viatu hivyo hakuna maana yoyote.
'Hutokea tu labda mtu kavirusha tu juu vimekwama, sidhani kama inamaana yoyote me sijawahi kusikia', Selemani Mayala
Kwanini mtindo huu unakosolewa?
Hata hivyo ikiwa ni alama ya maisha ya zamani ya uhalifu kwa baadhi ya wakaazi wa Soweto katika mtaa wa Kibera hawafurahishwi na mtindo huu.
Zaina Abdallah ambaye sio jina lake halisi anasema huwa inaamsha kumbukumbu mbaya huku wakichora taswira mbaya kuhusu mtaa huu.
Iwapo angekuwa na ujasiri na usaidizi, Zainab Abdallah angetetea dhidi ya viatu vinavyoning'inia katika nyaya za umeme ambapo ni hatari hasa mvua inaponyesha.
"Kando na kufanya eneo hilo kutoonekana vizuri kwa sababu ya viatu vilivyoning'inia, viatu hivyo ni bomu linalosubiri kulipuka wakati nyaya za umeme zinagusana," anasema Zaina huku akizitaka mamlaka kuchukua hatua dhidi ya tabia hiyo.
Iwe ni kwa nia njema ama kwa nia mbaya, bado kutundika viatu kwenye nyaya za umeme ni hatari.