Je, Iran kukishambulia Kisiwa cha Diego Garcia, ambacho ni marufuku raia kufika?

m

Chanzo cha picha, Planet Lab

    • Author, Farzad Seifikaran
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya ripoti kwamba ndege sita za kivita za Marekani aina ya B-2 zimepelekwa kwenye kisiwa cha mbali, kisiwa tulivu, na kizuri katika Bahari ya Hindi ambacho ni marufuku mtu yoyote raia kufika.

Taarifa zinasema kwamba kisiwa hicho kinaweza kulengwa "kulengwa kwa makombora" kutoka kwa Iran iwapo mvutano kati yake na Marekani utaongezeka.

Diego Garcia ni makazi ya kituo cha kijeshi cha pamoja kati ya Uingereza na Marekani. Shirika la habari la IRNA lilisema kwamba kituo hicho kiko kwenye rada za "makombora na droni za Iran za masafa ya kati."

Siku chache zilizopita, Rais wa Marekani Donald Trump alisema katika mahojiano kwa njia ya simu na NBC kwamba Iran itashambuliwa ikiwa haitafikia makubaliano mapya ya nyuklia na Marekani. Alisisitiza: "Kama hawatufikii makubaliano, watashambuliwa. Watashambuliwa kwa njia ambayo hawajawahi kuona hapo awali."

Sasa, BBC Persian imebaini kupitia uchunguzi wa picha za setilaiti kwamba kati ya Machi 22, 2025, na Aprili 2, ndege sita za B-2 na ndege sita za B-52 zimepelekwa katika kituo cha kijeshi cha Diego Garcia.

Maafisa wa Marekani hawajatangaza rasmi kupelekwa kwa ndege hizi huko Diego Garcia au sababu ya kufanya hivyo, na Kamandi ya Kistratejia ya Jeshi la Marekani pia imesema kwamba haizungumzii kuhusu mazoezi au operesheni zake.

a

Chanzo cha picha, Planet Lab

Maelezo ya picha, Ndege za kivita za B-52 zimepelekwa kwenye kambi ya Diego Garcia, Machi 25, 2025

Kwa kuchunguza zaidi picha za setilaiti, BBC imebaini kuwa kupelekwa kwa ndege za kivita huko Diego Garcia ulianza Machi 25, ambapo ndege kumi na moja za B-52 zilipelekwa kituoni hapo.

Jumamosi iliyopita, Machi 29, idadi ya ndege za B-52 ilipungua hadi kufikia sita, lakini wakati huo huo, ndege nne za B-2 zilikuwa zimewasili kwenye kituo hicho.

Karibu wakati huo huo na ripoti za kupelekwa kwa ndege za B-2 na B-52 hadi kituo cha kijeshi cha Diego Garcia, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilizindua kituo chake kipya cha chini ya ardhi cha makombora, ambacho kiliibua maoni mengi.

Katika kituo cha makombora kilichozinduliwa, makombora kama Khyber-Shakan, Haj Qasim, Emad, Sejjil, Qadr-H, na kombora la mwelekeo wa Paveh yaliwekwa wazi.

Je, Iran inaweza kukishambulia Kisiwa cha Diego Garcia?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jibu la swali hili si rahisi na linahitaji utafiti wa kitaalamu kuhusu uwezo wa kijeshi wa Iran katika nyanja za makombora na droni.

Kisiwa cha Diego Garcia kiko umbali wa kilomita 3,800 kutoka eneo la kusini zaidi la Iran, katika bandari ya Pasabandar.

Hii ni wakati ambapo masafa ya makombora ya masafa marefu na makombora ya mwelekeo wa kijeshi yanayomilikiwa na Iran yanasemekana kuwa na uwezo wa kwenda umbali wa kati ya kilomita 2,000 na 2,500.

Baadhi ya makombora ya balistiki ya Iran, kama Sejil na Shahab-3B, yanadaiwa kuwa na masafa ya "kilomita elfu mbili," na kulingana na walinzi wa mapinduzi, masafa halisi ya kombora la Somar la mwelekeo wa kijeshi ni "kati ya kilometa 2,000 na 2,500."

Masafa halisi ya makombora haya hayawezi kuthibitishwa kwa uhakika, lakini bado hayajawahi kutumika kwa oparesheni ya masafa ya kilomita 2,000.

Umbali mkubwa zaidi ambao makombora ya Iran yameweza kufika hadi sasa ulikuwa wakati wa Operesheni Vashti Sadeq, ile uya kwanza na ya pili katika shambulio dhidi ya Israel.

Umbali kutoka sehemu ya magharibi kabisa ya Iran hadi Israel ni karibu kilomita 1,200.

.

Chanzo cha picha, IMA MEDIA

Maelezo ya picha, Uzinduzi wa kwanza wa ndege isiyo na rubani ya Shahed-136B

Masafa ya droni za Iran pia yameripotiwa kwenda umbali karibu "kilomita 2,500." Hata hivyo, mnamo Oktoba 2014, Kikosi cha Anga cha IRGC kilizindua droni ya Shahed-136B, ambayo inasemekana kuwa na uwezo wa kwenda "masafa ya kilomita 4,000."

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Iran kutangaza kuwa na silaha za kijeshi zilizo na masafa zaidi ya "kilomita elfu mbili."

Kwa mujibu wa Jeshi la Iran, matamshi ya Kiongozi Mkuu Ali Khamenei kwamba masafa ya makombora ya Iran hayapaswi kuzidi kilomita 2,000 kwa sasa yamesababisha kutengenezwa kwa makombora ya masafa marefu zaidi. Khamenei alisema kuwa kuna "sababu" ya uamuzi huu, lakini hakuitaja wazi.

Iwapo masafa ya droni ya Shahed-136B ni sahihi, Iran itaweza kukilenga Kisiwa cha Diego Garcia, lakini kuna njia nyingine za kukishambulia kisiwa hicho; kwa mfano, kuboresha masafa ya makombora na droni, au kutumia meli inayobeba droni ambayo IRGC ilizindua hivi karibuni.

Kwa kutumia meli hii, kuna uwezekano kwamba Iran inaweza kuwa karibu zaidi na kisiwa cha Diego Garcia kijiografia na kushambuliwa kwa droni kutokea hapo.

Lakini haya si rahisi kutekelezwa kwa muda mfupi.

Wakati mvutano kati ya Tehran na Washington unazidi kuongezeka, msemaji wa Pentagon Sean Parnell alisema jana: "Ikiwa Iran au mawakala wake watatishia wafanyakazi wa Marekani na maslahi yetu katika eneo hilo, Marekani itachukua hatua kali kulinda watu wetu."

Tunachojua kuhusu ndege za mashambulizi za B-2 na kwa nini ni tishio kwa Iran?

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege ya kivita ya B-2 katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Andersen

Umuhimu wa ndege za mashambulizi za B-2 Spirit unatokana na uwezo wake wa kushambulia kwa nguvu vituo vya ardhini vilivyo chini ya ulinzi mkali.

Ndege hizo na mabomu yake hutengenezwa na kampuni ya Northrop Grumman na linaweza kupenya mifumo ya ulinzi ya hali ya juu zaidi na kushambulia maeneo lengwa yenye ulinzi mkubwa.

Ndege hii ina uwezo wa kufikia umbali wa kilomita 9,600 kwa kujaza mafuta mara moja, na kutokana na muundo wake wa anga, inaweza kuruka kwa urahisi kwenye urefu wa juu sana.

Ndege za B-2 zina uwezo wa kubeba mabomu mazito, yakiwemo mabomu ya nyuklia. Miongoni mwa silaha zake ni bomu la kupenya ardhini la GBU/57AB lenye uzito wa kilo 14,000.

Ndege hii inadaiwa kuwa na uwezo wa kuruka kwa kasi karibu na kasi ya sauti na kufikia urefu wa futi 50,000.

Jeshi la Anga la Marekani linadaiwa kuwa na ndege 20 za B-2.

Tangu Donald Trump aingie madarakani, uwezekano wa kushambuliwa kwa vituo vya nyuklia vya Iran umeongezeka, na kupelekwa kwa idadi kubwa ya ndege hizi kumewatia wasiwasi maafisa wa Iran.

Ndege hii ina uwezo wa kuepuka mifumo ya ulinzi na rada, na mabomu yake yanaweza kuharibu vituo vya kijeshi vilivyo chini ya ardhi.