Afrika Kusini inamsaka mtuhumiwa aliyesimamia shughuli za uchimbaji haramu wa madini

    • Author, Mayeni Jones
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Hakuna mtu nchini Afrika Kusini anayeonekana kujua alipo Tiger. Mwanaume mwenye umri wa miaka 42 kutoka nchi jirani ya Lesotho, ambaye jina lake halisi ni James Neo Tshoaeli, anasakwa na polisi kwa muda wa miezi minne sasa.

Polisi wanasema, alitoroka kizuizini baada ya kutuhumiwa kuendesha shughuli haramu katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa karibu na mji wa Stilfontein nchini Afrika Kusini, ambapo maiti 78 zilipatikana ndani ya mgodi huo mwezi Januari.

Polisi wanne, wanaodaiwa kumsaidia kutoroka, wako nje kwa dhamana na wanasubiri kufikishwa mahakamani.

Tulikwenda Lesotho ili kujua zaidi kuhusu mtu huyu na kusikia kutoka kwa wale walioathiriwa na vifo katika mgodi.

Pia unaweza kusoma

Familia ya Tiger

Nyumba ya Tiger iko karibu na jiji la Mokhotlong, umbali wa saa tano kwa gari kutoka mji mkuu, Maseru, kwenye barabara inayopita katika milima ya taifa hilo.

Tunamtembelea mama yake, Mampho Tshoaeli, na kaka yake mdogo, Thabiso. Tofauti na Tiger, Thabiso aliamua kukaa nyumbani na kufuga kondoo kwa ajili ya kujipatia riziki, badala ya kujiunga na wachimba migodi haramu, wanaojulikana kama zama zamas, nchini Afrika Kusini.

Hawajamuona Tiger kwa miaka minane sasa.

"Alikuwa mtoto rafiki kwa kila mtu," anasema Bi Tshoaeli.

"Alipenda amani hata shuleni, walimu wake hawakuwahi kulalamika kuhusu yeye. Kwa ujumla, alikuwa mtu mzuri," anasema.

Thabiso, mdogo wa Tiger kwa miaka mitano, anasema wote wawili walikuwa wakichunga kondoo wa familia walipokuwa watoto.

"Wakati tunakuwa alitaka kuwa polisi. Hiyo ilikuwa ndoto yake. Lakini haikuwahi kutokea kwa sababu, baba yetu alipoaga dunia, ilibidi awe mkuu wa familia."

Tiger, aliyekuwa na umri wa miaka 21 wakati huo, aliamua kufuata nyayo za baba yake na kuelekea Afrika Kusini kufanya kazi katika mgodi - lakini sio katika sekta rasmi.

Alikuwa akirudi akipata likizo au Krismasi. Na katika kipindi hicho cha kwanza cha uchimbaji madini – Tiger alikuwa ndiye mlezi mkuu wa familia.

"Kwa kweli alituhudumia sana. Akinipa kila kitu, hata ndugu zake. Alihakikisha wanapata nguo na chakula."

Mara ya mwisho familia yake kumuona au kusikia kutoka kwake ilikuwa mwaka 2017 alipoondoka Lesotho na mke wake wa wakati huo. Muda mfupi baadaye, wanandoa hao walitengana.

"Nilidhani labda ameoa tena, na mke wake wa pili hakuwa akimruhusu kurudi nyumbani," anasema mama yake kwa huzuni.

"Nimekuwa nikiuliza: 'Mwanangu yuko wapi?'

"Mara ya kwanza niliposikia ni mchimbaji madini huko Stilfontein, niliambiwa na mwanangu, alikuja nyumbani akiwa ameshika simu na akanionyesha habari hizo kwenye mitandao ya kijamii na kunieleza kuwa wanasema, ametoroka polisi."

Kweli ni kiongozi mkuu?

Polisi wanasema wachimba migodi haramu walimtaja kama mmoja wa viongozi huko Stilfontein.

"Kwa kweli inaniuma sana, labda atafia huko, au labda tayari amekufa, au akibahatika kurudi nyumbani, labda sitakuwepo tena. Nitakuwa miongoni mwa waliokufa," anasema mama yake.

Rafiki wa Tiger kutoka Stilfontein, kwa jina la Ayanda, ananiambia walikuwa wakila pamoja na kuvuta sigara kabla ya mahitaji hayo kupungua.

Pia anatilia shaka kwamba Tiger ndio "kiongozi mkuu," anasema Tiger alikuwa akifanya usimamizi wa kati zaidi.

"Alikuwa bosi wa chini, lakini si bosi mkuu. Alikuwa kama msimamizi, mtu ambaye akitusimamia sisi tuliokuwa tukifanya kazi."

Mtafiti wa madini Makhotla Sefuli anaamini Tiger hakuwa ndio kiongozi mkuu shughuli haramu za uchimbaji madini huko Stilfontein. Anasema wakuu hasa wa shughuli hizo, kamwe hawafanyi kazi ya kuwa chini ya migodi.

“Biashara haramu ya uchimbaji madini ni sawa na piramidi yenye safu nyingi, huwa tunatazama tu safu ya chini kabisa ambayo ni ya wafanyakazi. Lakini kuna safu ya pili... wanaopeleka pesa kwa wachimbaji haramu.

"Halafu kuna wanunuzi...wananunua [dhahabu] kutoka kwa wale wanaopeleka fedha kwa wachimbaji haramu."

Juu kabisa kuna "watu wenye nguvu sana," na "wenye ukaribu na wanasiasa wakubwa." Watu hawa hupata pesa nyingi zaidi, lakini hawachafui mikono yao kwenye migodi.

Waliofariki

Supang Khoaisanyane alikuwa mmoja wa wachimbaji waliolifariki. Mwili wa kijana huyo mwenye umri wa miaka 39 ni miongoni mwa miili iliyopatikana mwezi Januari. Yeye, kama wengine wengi walioangamia, alikuwa ni muhamiaji Afrika Kusini. Anatokea Kijiji cha Bobete, katika wilaya ya Thaba-Tseka.

Baada ya kuvuka daraja dhaifu, kuna safari ndefu ya kupanda milima katika barabara isiyo na vizuizi vya usalama. Kuna mandhari safi huko. Makumi ya vibanda vidogo vilivyoezekwa kwa nyasi, kuta zake zimejengwa kwa mawe, vimezungukwa na vilima vya kijani kibichi.

Karibu kabisa na nyumba ya familia ya marehemu Supang, kuna nyumba ambayo haijakamilika aliyokuwa akijenga kwa ajili ya mke wake na watoto watatu.

Tofauti na makazi mengi katika kijiji hicho, nyumba hiyo ni ya tufali, lakini bado haina paa, madirisha na milango.

"Aliondoka kijijini kwa sababu alikuwa akihangaika," anasema shangazi yake Mabolokang Khoaisanyane.

Mke wake Supang na mmoja wa watoto wake wamejilaza kwenye godoro sakafuni, wakitazama angani kwa huzuni.

"Alikuwa akitafuta pesa huko Stilfontein, kuilisha familia yake, na kuezeka nyumba yake," anasema Bi Khoaisanyane.

Nyumba hiyo ilijengwa na Supang kwa pesa alizozipata kutokana na safari ya awali ya kikazi nchini Afrika Kusini - safari ambayo wengi wa watu kutoka Lesotho wameifanya kwa miongo kadhaa kutokana na fursa katika nchi jirani ya Afrika Kusini.

Shangazi yake anasema, aliondoka mara ya pili, miaka mitatu iliyopita.

Nchi hii isiyo na bandari - imezungukwa na nchi ya Afrika Kusini - ni moja ya nchi maskini zaidi duniani. Ukosefu wa ajira umefikia 30% lakini kwa vijana umefikia 50%, kulingana na takwimu rasmi.

Familia ya Supang inasema haikujua kuwa alikuwa akifanya kazi kama mchimbaji haramu wa madini, hadi jamaa yao mmoja alipowapigia simu na kusema amekufa chini ya ardhi.

Walidhani alikuwa akifanya kazi ya ujenzi na hawakuwahi kusikia kutoka kwake tangu aondoke Bobete 2022.

Bi Khoaisanyane anasema kupitia simu hiyo, waliambiwa kilichosababisha vifo vya watu wengi waliokuwa chini ya ardhi huko Stilfontein ni ukosefu wa chakula na maji. Wengine zaidi ya 240 waliookolewa wakiwa dhaifu sana.

Mgodi wa Stilfontein

Stilfontein iligonga vichwa vya habari duniani mwishoni mwa mwaka jana pale polisi walipotekeleza mkakati wenye utata wa kukabiliana na uchimbaji haramu wa madini.

Walizuia mtiririko wa chakula na maji ndani ya mgodi huo katika jaribio la kuwatoa wachimbaji hao.

Mwezi Januari, amri ya mahakama iliilazimisha serikali kuanzisha operesheni ya uokoaji.

Familia ya Supang inasema inaelewa sasa kuwa alichokuwa akikifanya ni kinyume cha sheria lakini hawakubaliani na jinsi mamlaka ilivyoshughulikia jambo hilo.

"Waliwatesa watu kwa njaa, bila kuruhusu chakula na dawa kuteremshwa. Inatusikitisha sana kwamba alikuwa chini ya ardhi bila chakula. Tunaamini hilo ndilo lilikatisha maisha yake," anasema shangazi yake.

Familia ya mchimba mgodi huyo aliyefariki hatimaye ilipokea mwili wake na kumzika karibu na nyumba yake aliyokuwa akiijenga.

Lakini mama na kakake Tiger bado wanangojea habari kuhusu Tiger. Huku Polisi wa Afrika Kusini wakisema msako unaendelea.