Fahamu kwanini Iran inashirikiana na Urusi na China

Muda wa kusoma: Dakika 2

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi anasema nchi yake inashirikiana na China na Urusi kuzuia kurejeshwa kwa vikwazo vya Ulaya dhidi ya mpango wa nyuklia wa Tehran.

Maoni yake yanakuja siku moja baada ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kukataa hoja ya Bw. Araqchi kwamba hakuna msingi wa kisheria wa kurejesha vikwazo.

Araqchi alisafiri hadi Karbala kushiriki katika sherehe za Arbaeen alisema katika kipindi cha "Jarian" kwenye Televisheni ya Iran ya Channel One: "Tunashirikiana na China na Urusi kuzuia hatua hiyo. Hili lisipofaulu na wao kulitekeleza, tuna zana za kujibu. Tutazijadili kwa wakati ufaao."

Bw. Araqchi pia alikiri kwamba ikiwa vikwazo hivyo vitawekwa , "hakika ni jambo baya na hatuna shaka kwamba tutajaribu kulizuia hadi dakika ya mwisho.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeuambia Umoja wa Mataifa kwamba zitatumia "trigger mechanism" ikiwa suluhisho la kidiplomasia la mpango wa nyuklia wa Iran halitapatikana ndani ya siku 15.

Utaratibu huo unaojulikana kama "kichochezi" ulikuwa sehemu ya makubaliano ya JCPOA na Iran na pia umejumuishwa katika azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama.

Kwa mujibu wa utaratibu huo ambao unamalizika tarehe 18 Oktoba mwaka huu, mhusika yeyote katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA iwapo hataridhika na ushirikiano wa Iran, anaweza kukumbuka maazimio ya Baraza la Usalama dhidi ya Iran ambayo yana vikwazo.

Bwana Araqchi anasema: "Katika barua ndefu na yenye hoja kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, nilisema kwamba kwa sababu wengi wao si wanachama tena wa JCPOA. Bila shaka, wanaweza pia kujaribu njia nyengine."

Amesisitiza kuwa: "Suala hili lina matatizo mengi ya kisheria. Tumekuwa tukifanya mikutano ya mara kwa mara ya wataalamu na China na Urusi kuhusu suala hili kwa miaka kadhaa.

Bila shaka, suala hilo linapofikishwa kwenye Baraza la Usalama, uamuzi wa mwisho unatolewa huko, na Iran si mwanachama wa Baraza la Usalama; hii inafanya kazi yetu kuwa ngumu zaidi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza: Sasa ni wakati wa Iran kuamua hatma yake

Uingereza ilisema jana kwamba kwa muda mrefu imekuwa ikiweka wazi kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa na kwamba Tehran imeshindwa kutoa hakikisho la kuaminika kuhusu asili ya mpango huo.

Waziri wa Mambo ya Nje David Lemmy alisema kuwa, pamoja na wenzetu wa Ufaransa na Ujerumani, tumejitahidi mara kwa mara kutafuta suluhu la kidiplomasia ili kushughulikia maswala haya.

"Tumeiongezea Iran muda mdogo wa kuondolewa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, mradi tu masharti ya wazi yatatimizwa, ikiwa ni pamoja na Iran kuanza tena mazungumzo na Marekani na kuhakikisha ushirikiano kamili na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Dunia."

Kwa mujibu wa Bw. Lamy, "Iran bado ina chaguo la kurejesha diplomasia, na tunaitaka Iran ifanye hivyo. Mpira sasa uko kwa Iran kufanya uamuzi."

Iran na nchi tatu za Ulaya zilikutana mara moja katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje na mara moja katika ngazi ya manaibu waziri wa mambo ya nje baada ya shambulio la Israel.

Iran inasema bado haijawekwa tarehe ya duru ijayo ya mazungumzo.

Nchi hizo tatu pamoja na Marekani, China na Urusi, zilitia saini mpango kamili wa utekelezaji wa pamoja (JCPOA), makubaliano ambayo yaliipa Iran motisha ya kupunguza kasi ya kurutubisha madini ya uranium.

Rais Donald Trump alijiondoa katika makubaliano hayo wakati wa muhula wake wa kwanza na kuiwekea Iran vikwazo vipya.

Lakini nchi tatu za Ulaya zilisema zitashikilia makubaliano hayo.