Kipi kinachotokea miilini mwetu tunapokataliwa na jinsi ya kukabiliana nacho

Makala moja ya New York Times yadokeza kwamba kizazi cha sasa cha vijana wakubwa kinakabiliwa na kukataliwa kuu zaidi katika historia, na matatizo ya kupata kazi, mkopo, na elimu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Makala moja ya New York Times yadokeza kwamba kizazi cha sasa cha vijana wakubwa kinakabiliwa na kukataliwa zaidi katika historia, na matatizo ya kupata kazi, mkopo, na elimu.
    • Author, Daniel Gallas
    • Akiripoti kutoka, BBC News Brazil
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Je, inawezekana kuwa kizazi cha sasa cha vijana ni "kizazi kilichokataliwa zaidi katika historia"?

Wazo hili lilitolewa na mwandishi wa habari wa Marekani, David Brooks, kupitia makala katika The New York Times, baada ya mazungumzo na vijana waliokumbana na kukataliwa katika maeneo mbalimbali ya maisha — kuanzia maombi ya kujiunga na vyuo vikuu, nafasi za ajira, mahusiano ya kimapenzi, hadi kupata mikopo ya nyumba.

Kwa mujibu wa Brooks, dunia ya leo imejaa ushindani mkubwa zaidi kuliko wakati wowote ule.

Vijana wanaohitimu shule za sekondari hulazimika kutuma maombi kwa vyuo vingi, kati ya 20 hadi 30, lakini wengi wao hukataliwa na kubahatika kukubaliwa na kimoja au viwili tu.

Hali hii ya kukataliwa inaendelea katika hatua nyingine za maisha, huku rasilimali zikiwa chache na mahitaji yakiwa makubwa zaidi katika kila sekta.

Lakini tatizo la kukataliwa si la kijamii pekee, lina athari kubwa kiakili na kihisia.

Tafiti za mwanasaikolojia Roy Baumeister, mmoja wa watafiti wa mwanzo wa athari za kukataliwa, zinaonesha kuwa kukataliwa humfanya mtu awe na hasira zaidi, ashindwe kudhibiti hisia zake, apunguze uwezo wa kufikiri kwa utulivu, na pia apoteze huruma kwa wengine.

Katika majaribio ya kimaabara aliyofanya, Baumeister aliwafanyia watu majaribio ya kukataliwa kwa njia mbalimbali, na kufuatilia mabadiliko ya tabia zao.

Aligundua kuwa athari ya kwanza huwa ni hali ya "kupoteza hisia," kana kwamba mwili unajilinda dhidi ya maumivu kwa kuzima hisia kwa muda.

Lakini hali hiyo ya kupotea kwa hisia huleta matatizo mengine makubwa: kupungua kwa huruma, kuongezeka kwa uchokozi, na kushuka kwa udhibiti wa nafsi.

Soma pia:

Je, kizazi cha sasa ndicho kinachokataliwa zaidi?

BBC News Brazil ilizungumza na Baumeister kuhusu kazi yake kuelewa madhara ya kukataliwa sio tu kwa watu binafsi, lakini pia kwa jamii kwa ujumla.

Hii ni sehemu ya mahojiano.

Ni jambo linalowezekana, hasa katika baadhi ya maeneo.

Kwa mfano, vyuo vikuu vikuu havijaongeza nafasi kwa kiasi kikubwa, lakini idadi ya wanaotuma maombi imeongezeka mno. Hili linalazimu watu kuomba vyuo vingi zaidi, na matokeo yake ni kukataliwa mara nyingi.

Kuna pia tatizo la "grade inflation" — ambapo walimu huongeza alama za wanafunzi bila kuakisi ubora halisi wa kazi zao ili kuwasaidia kufuzu.

Nimesoma kitabu kipya cha Peter Turchin kuhusu "uzalishaji mkubwa wa wasomi," ambacho kimenishawishi kuwa tunazalisha wasomi wengi zaidi kuliko nafasi zilizopo.

Mwaka 1960, ni sehemu ndogo tu ya watu waliomaliza vyuo vikuu, lakini leo idadi ni kubwa zaidi huku nafasi za ajira zikiwa zile zile. Hii inaongeza ushindani na kukataliwa, hasa katika soko la ajira.`

Vijana wanapaswa kutuma maombi kwa vyuo vingi na kuishia kukataliwa na wengi wao.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vijana wanapaswa kutuma maombi kwa vyuo vingi na kuishia kukataliwa na wengi wao.

Hata katika mahusiano ya kimapenzi, majukwaa ya mitandaoni huunganisha watu kwa vigezo vya juujuu, jambo linaloleta uhusiano usiodumu na kuongeza idadi ya waliokataliwa.

Madhara ya kisaikolojia ya kukataliwa

Utafiti wangu ulianza na hoja kwamba hitaji la kuunganishwa na watu wengine ni moja ya misukumo ya msingi ya binadamu.

Kukataliwa huzuia na kuvuruga kabisa msukumo huu.

Kazi yako inaeleza kile kinachotokea kwa watu wanapokataliwa. mahitimisho yako yalikuwa yapi? Je, watu hubadilika?

Tulidhani athari ya kwanza itakuwa huzuni au mshtuko wa kihisia. Lakini katika majaribio yetu mengi ya kimaabara, hatukupata ushahidi wa moja kwa moja wa huzuni hiyo. Badala yake, tulibaini mabadiliko ya tabia.

Baumeister anasema kuwa kukataliwa kunawafanya watu kutopenda jamii zaidi na kukabiliwa na uchokozi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baumeister anasema kuwa kukataliwa kunawafanya watu kutopenda jamii zaidi na kukabiliwa na uchokozi.

Kwa kawaida, mtu hukumbwa na hali ya "kupotea kwa hisia" hali ambapo mtu hajisikii kitu chochote. Ni sawa na jeraha la mwili, ambapo mwili hutoa kemikali zinazopunguza maumivu kwa muda mfupi. Vivyo hivyo, kukataliwa kunaweza kupelekea kutolewa kwa opioidi za asili zinazozuia maumivu ya kihisia.

Hali hii huathiri mfumo mzima wa kihisia.

Mtu hupoteza uwezo wa kuonesha au kuhisi huruma kwa wengine. Badala ya kutafuta ushirikiano tena, mtu aliyekataliwa huwa na tabia ya kujitenga, kuchukia, na hata kuwa na hasira au tabia za uhasama.

Watu ambao wanakabiliwa na kukataliwa wameona utendaji wao wa kiakili ukiathiriwa, kulingana na Baumeister.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu ambao wanakabiliwa na kukataliwa wameona utendaji wao wa kiakili ukiathiriwa, kulingana na Baumeister.

Utafiti mwingine ulionyesha kuwa watu waliokataliwa utotoni hupata maumivu zaidi wanapopata magonjwa au majeraha, ikilinganishwa na wale wasio na historia hiyo.

Inaonekana mifumo ya mwili ya kukabiliana na maumivu inadhoofika zaidi baada ya kukataliwa mapema maishani.

Uvumilivu wa maumivu pia hupungua wakati watu wanakataliwa.

Huenda mifumo ya mwili wako inapungua unapokataliwa utotoni, na hivyo kukufanya ushindwe kustahimili maumivu unapokuwa mtu mzima.

Je, kukataliwa kwa wingi kunaweza kuathiri jamii?

Kwa kuwa watu wengi zaidi wanakataliwa kwa kiwango cha mtu binafsi, hii inaweza kuwa na athari kwa jamii kwa ujumla? Ikiwa watu waliokataliwa watakuwa wakali zaidi na wasio na huruma, je, jamii inaweza kuishia kuiga sifa hizi?

Ndiyo. Tulipokuwa tukichapisha tafiti hizi, baadhi ya wanajamii walituambia kuwa makundi ya kijamii yanayohisi yamekataliwa huonesha tabia kama zile za mtu mmoja aliyekataliwa: yanakuwa ya fujo zaidi, yasiyo na mshikamano, na yasiyo tayari kushirikiana kwa manufaa ya pamoja.

Tulifanya pia vipimo vya kiwango cha akili yaani IQ na kugundua kuwa watu waliokataliwa walifanya vibaya zaidi baada ya kukataliwa.

Inawezekana kwamba kukataliwa hudhoofisha uwezo wa kufikiri na kusoma.

Aidha, makundi yanayohisi yamekataliwa hayaoneshi motisha ya kujifunza, kushiriki au kufanikisha malengo ya kielimu.

Jinsi ya kukabiliana na kukataliwa

Unashughulikaje na kukataliwa, kwani athari zake nyingi hata hazionekani kwa watu?

Changamoto kubwa ni kwamba watu hawatambui mabadiliko haya hawagundui kuwa mfumo wao wa kihisia haupo sawa.

Ikiwa umekataliwa, jaribu tena mahali pengine, Baumeister anapendekeza.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ikiwa umekataliwa, jaribu tena mahali pengine, Baumeister anapendekeza.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nimeandika kuhusu mahusiano ya kimapenzi yasiyolipiwa ambapo mtu mmoja anapenda lakini mwingine hampendi.

Hali hii huvunja sana kujiamini na huacha maswali mengi: "Sijatosha?" "Nimekosea wapi?" "Kwa nini hanipendi?"

Tuligundua pia kuwa sehemu ya maumivu haya hutokana na hofu kuwa kuna kasoro ndani yako ambayo inaweza kusababisha ukataliwe tena na mtu mwingine atakayekuja baadaye.

Ushauri wangu:

Jaribu tena mahali pengine. Katika utafiti wetu, tuliona kuwa mtu hujisikia vibaya mpaka pale atakapopata mtu mwingine wa kumpokea. Kukubalika mahali pengine hufuta maumivu ya awali.

Katika kazi yangu ya utafiti, nimetuma mamia ya makala. Nyingi hukataliwa. Lakini pale moja inapokubaliwa, unaendelea mbele na maumivu ya kukataliwa yanapotea.

Hali hii ya kukataliwa ni sehemu ya mchakato wa maisha, lakini bado haifanyi iwe rahisi.

Je, kukataliwa kunaweza kuwa tatizo la afya ya umma?

Je, kukataliwa kwa wingi kunaweza kuwa tatizo la afya ya umma?

Sina uhakika kamili, lakini naamini linaweza kuwa na athari mbaya kwa afya ya watu.

Utafiti unaonesha kuwa watu wanaoishi peke yao huugua zaidi.

Wagonjwa waliotembelewa mara kwa mara na ndugu na marafiki walipona haraka zaidi kuliko wale waliokosa msaada wa kijamii.

Wataalamu wa afya mwanzoni waliona hili kama jambo lisilo la kisayansi, lakini ushahidi ni mzito na wa kueleweka.

Watu waliokataliwa huwa na uwezo mdogo wa kujidhibiti.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu waliokataliwa huwa na uwezo mdogo wa kujidhibiti.

Vidudu husababisha magonjwa, mifupa huvunjika kwa sababu za kimwili. Idadi ya wanafamilia wanaokuambia wanakupenda na kukukumbatia haipaswi kuathiri uponyaji. Lakini data ni ya kulazimisha sana na yenye kushawishi.

Kadri tunavyoendelea kuishi katika jamii yenye watu wengi wanaoishi peke yao, tutaona ongezeko la changamoto za afya ya umma.

Je, ni janga? Labda bado halijawa janga, lakini kuna dalili zinazotia hofu.

Vijana wanachelewa kuoa/kuolewa, wana uhusiano wachache wa maana, na hata tendo la ndoa limepungua.

Hii inaongeza idadi ya watu wanaoishi pekee na hii, kwa tafiti nyingi, huhusishwa na matatizo ya afya ya akili na mwili.

Lakini hatupaswi kufikiria kizamani pia. Watu wengi waliishi katika familia na nyumba zisizo na furaha na walikaa huko kwa sababu tu hawakuwa na uwezo wa kuondoka. Watu matajiri zaidi sasa wanaweza kumudu kuishi peke yao, na kuishi peke yao kuna faida zake.

Kitu gani kilichokushangaza zaidi katika utafiti wako?

Kilichonishangaza zaidi ni kutokuwepo kwa hisia kali mara moja baada ya kukataliwa.

Tulidhani tulikuwa tunapima vibaya. Lakini baada ya kufanya majaribio kwa njia mbalimbali, tuligundua kuwa badala ya huzuni ya haraka, watu hupata ongezeko la hisia chanya za ndani zisizotambulika moja kwa moja. Hili lilikuwa jambo la kushangaza sana.

Tuliwauliza watu watabiri matokeo ya majaribio, lakini hakuna hata mmoja aliyedhania kuwa kukataliwa kungesababisha kuibuka kwa hisia nzuri hata kama kwa muda mfupi.

Hii inaweza kuwa ni sehemu ya mfumo wa kujilinda wa kisaikolojia: unapopitia jambo gumu, akili yako ya ndani (subconscious) huanza kutafuta mawazo chanya kama njia ya kujifariji.

Kwa hiyo, mtu aliyekataliwa huingia kwenye hali ya kutohisi kitu chochote, lakini ndani ya nafsi yake, akili inaanza kujielekeza kwenye fikra nzuri zisizo za moja kwa moja.

Ni sawa na jeraha la mwili wakati mwingine unaweza kucheza mchezo mgumu bila kuhisi maumivu yoyote. Usiku ukifika, unashangaa mguu au mkono unauma sana, ukijiuliza: "Nilijeruhiwa wapi?" Ndiyo maana watu hukumbwa na maumivu baadaye, si mara moja.

Kukataliwa ni hali kama hiyo: unaweza usihisi uchungu wake mara moja, lakini utaujua baadaye. Ikiwa katika kipindi hicho akili yako imeanza kujenga hisia chanya au matumaini, basi maumivu ya kukataliwa yanapokuja hayatakuwa makali sana kama yangekuwa yamekufikia papo hapo.

Hili lilikuwa jambo la kushangaza na lenye maana kubwa katika kuelewa jinsi binadamu hujihami dhidi ya maumivu ya kihisia.

Unafanya kazi gani kwa sasa?

Kwa sasa, ninafanyia kazi makala kuhusu mabadiliko kutoka mawasiliano ya ana kwa ana hadi mawasiliano ya kidijitali.

Tunachunguza jinsi teknolojia, hasa ujumbe wa maandishi na mitandao ya kijamii, inavyobadili namna watu wanavyowasiliana.

Tafiti zinaonesha kuwa mawasiliano ya kidijitali yanaposaidia mawasiliano ya ana kwa ana, yanaweza kuwa na athari chanya. Lakini pale teknolojia inapotumika badala ya mawasiliano ya ana kwa ana, ndipo matatizo huzuka: hisia hupungua, uhusiano unadhoofika, na matatizo ya afya ya akili huongezeka.

Kwa hivyo, uhusiano wa kweli wa binadamu wa uso kwa uso bado ni muhimu sana.

Kukataliwa kwa njia ya mtandao pia huongeza ukatili na upweke, kwa sababu huathiri sana jinsi tunavyohisi, kujiamini, na hata uwezo wa kujenga uhusiano wa kina.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid