Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kipi kiliwatokea wavulana wawili waliogundua mojawapo ya almasi kubwa duniani?
- Author, Swaminathan Natarajan
- Nafasi, BBC
Ilikuwa habari njema mwaka 2017. Vichwa vya habari kote ulimwenguni viliandika juu ya kugunduliwa kwa almasi kubwa huko Sierra Leone.
Katika taifa la Afrika ambako madini yamekuwa chanzo cha umwagaji damu na taabu, utajiri wa jiwe hili ulitarajiwa kutajirisha maisha ya watu wa eneo hilo.
Komba Johnbull na Andrew Saffea walikuwa wadogo zaidi katika kundi la vijana watano wachimbaji - pale walipopata jiwe hilo kubwa lenye kung’aa.
Ilionekana ndoto zao zote zimetimia. Lakini miaka sita baadaye, ugunduzi wao wa kimiujiza umewakatisha tamaa.
Kazi Ngumu ya Uchimbaji
Saffea alikuwa mwanafunzi lakini alilazimika kuacha shule kutokana na umaskini. Nayo familia ya Johnbull ilisambaratishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1991-2002.
Kwa pamoja, walijiunga na kikundi cha wachimbaji madini watano kilichofadhiliwa na mchungaji wa eneo hilo. Hawakulipwa, lakini walipewa vifaa na chakula kwa ajili yao na familia zao. Ikiwa almasi ingegunduliwa, mfadhili angepata sehemu kubwa ya almasi hiyo.
Wawili hao walikubali kazi hiyo ngumu - walifanya kazi kwenye shamba la mitende kabla ya kifungua kinywa, na kisha kwenda mgodini kuchimba kwa siku nzima. Matarajio yalikuwa kupata pesa za kurejea shuleni lakini ukweli kazi ilikuwa ngumu.
Johnbull anakumbuka jinsi walivyokabiliana na mvua kubwa na joto kali la kiangazi.
"Tulijipa maneno ya ujasiri ili kututia motisha. Pia tulianzisha utani. Tulikuwa na kifaa cha Bluetooth na tukicheza muziki."
Pia walielezana kile ambacho wangefanya ikiwa wangekuwa matajiri ghafla.
Johnbull alitaka nyumba ya ghorofa mbili na Toyota FJ Cruiser, huku Saffea akitaka kumaliza elimu yake.
Almasi Kubwa
Siku yao ya bahati ilianza kama siku nyingine, kwa kifungua kinywa cha ndizi zilizochemshwa na maombi, kabla ya kuelekea mgodini.
Ijumaa ya tarehe 13 Machi 2017, mpango wao ulikuwa kutayarisha mazingira ya uchimbaji madini - kuvunja ardhi, kuchimba kokoto na kukabiliana na mafuriko ya tangu mwanzo wa msimu wa mvua.
Ndipo jicho la Johnbull likakutana na jiwe lenye kung'aa.
"Niliona jiwe chini ya maji ya bomba likiburutwa. Kwa sababu sikuwahi kuona almasi hapo awali. Nilisimama kwa zaidi ya dakika moja nikilitazama lile jiwe. Kisha nikamwambia mjomba, 'Mjomba, hili jiwe linang'aa, ni jiwe la aina gani?'
Johnbull alinyoosha mkono na kulichomoa kutoka kwenye maji.
"Ni la baridi sana. Mara tu nilipoichukua, walininyakua, wakisema, 'Hii ni almasi!'
Jiwe hilo lilikuwa na uzito wa karati 709, na kulifanya kuwa la 14 kwa ukubwa kurekodiwa duniani.
Wachimbaji hao walimjuulisha mfadhili wao, Mchungaji Emmanuel Momoh, naye akaipeleka serikalini. Iliuzwa kwa mnada kwa dola milioni 6.5.
Utajiri wayeyuka
Maelfu ya watu wa Sierra Leone hufanya kazi za uchimbaji katika migodi isiyo rasmi kama vile Johnbull na Saffea. Ikiwa wana bahati, wanaweza kupata kipande kidogo cha almasi lakini ni vigumu kupata almasi nzima kama hii.
Ilikubaliwa kila mchimbaji apate sehemu ya pesa hiyo, na faida nyingine iende kwa serikali kwa maendeleo ya ndani.
Wachimbaji walipokea malipo ya awali ya dola za kimarekani 80,000 tu kila mmoja. Ilikuwa pesa nyingi kuliko Saffea na Johnbull walivyotarajia.
"Nilipopata pesa yangu, niliihifadhi kwa wiki nzima bila kuigusa. Kisha nilisafiri hadi Freetown kununua nyumba," anasema Johnbull.
Saffea alitaka kwenda Canada kusoma, na Johnbull alikuwa na shauku ya kujiunga naye.
Walilimpa wakala dola 15,000 kwa usafiri, malazi na ada za chuo kikuu. Walipelekwa Ghana ambako walikaa miezi sita na kutumia pesa nyingi.
Mpango wao ulisambaratika baada ya ombi la visa kukataliwa. Johnbull alirejea Sierra Leone, sehemu kubwa ya pesa yake ya almasi sasa imepotea, huku Saffea akianza safari mpya ya kutaka kwenda Canada.
Saffea amekwenda nchi ya tatu, ambayo hatuitaji kwa usalama wake, aliambiwa anaweza kufanya kazi ya udereva wakati wa mchana na kusoma jioni. Lakini alipofika, hali halisi ilikuwa tofauti sana.
"Ninachunga farasi kwenye zizi ambalo pia ninalala na kula. Wafanyakazi wengine walipewa malazi mimi nikabaki kulala zizini."
Sio maisha ya utajiri ambayo Saffea aliyatarajia - yuko katika mazingira magumu. Kando na nyumba aliyonunua nchini Sierra Leone, pesa zake za almasi zimeisha. Sasa, anataka tu kurudi nyumbani.
Hakuna kutambuliwa
Kinachowauma zaidi ni hisia za kutotambuliwa ipasavyo kwa ugunduzi wao.
Taarifa za vyombo vya habari kuhusu almasi zilimlenga mchungaji aliyewafadhili. Wachimbaji halisi hawakutajwa. Saffea alihisi kutengwa na kuachwa.
Johnbull anatamani angetumia pesa zake kwa njia tofauti.
"Nilipokuwa na pesa nilikuwa mdogo sana, nikitazama nyuma sijisikii vizuri, wakati huo nilikuwa najionyesha kwa kununua nguo, si unajua jinsi vijana wanavyofanya.
"Laiti nisingekuwa na azma ya kusafiri nje ya nchi kwa matumaini ningepata pesa zaidi huko, ningefanya mengi hapa bila pesa kupotea."
Huenda yasiwe maisha aliyoyatarajia - Johnbull kwa sasa ana maisha ya kutengeneza madirisha ya alumini huko Freetown. Saffea ana matumaini ya kuungana naye ikiwa matarajio yake nje ya nchi hayatatimia.
"Wazazi wangu hawakuwa na nyumba nilipozaliwa," anasema Johnbull.
"Watoto wangu wanakulia katika nyumba ya baba yao Freetown. Hilo ni jambo kubwa. Watoto wangu hawatateseka jinsi nilivyoteseka."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi