Israel-Hamas: Zijue silaha mpya za teknolojia ya hali ya juu za Israel zinazotumiwa Gaza

    • Author, Amira Mhadhbi
    • Nafasi, BBC News Arabic

Vikosi vya jeshi la Israel au IDF, ni mojawapo ya majeshi yenye uwezo mkubwa duniani. Vita vya Gaza vimeshuhudia matumizi ya silaha mpya za teknolojia ya hali juu zilizoundwa na Israel.

Ujasusi wa kutumia akili mnembe au bandia unachukua sehemu kubwa katika silaha za Israel na utambuzi wa shabaha - ingawa uamuzi wa kuua unabaki kwa askari, kulingana na IDF.

Idadi ya waliofariki Gaza imepita watu elfu 22, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Ukanda wa Gaza, inayoendeshwa na Hamas.

IDF inasema inafuata sheria za kimataifa na inachukua tahadhari ili kupunguza majeruhi kwa raia.

Je! ni silaha gani mpya zinazotumiwa na Israel?

Vifaru vya Barak

Vifaru vya Barak vinaelezewa kuwa ni toleo la tano la vifaru vya Merkava. Vinatumia akili bandia. Vinamwezesha kamanda alieoko ndani kuona nje - hata kama funiko la juu limefungwa.

Vifaru hivi vipya viliwasilishwa kwa vikosi vya Israel mapema Septemba 2023, baada ya miaka mitano ya kutengenezwa.

Barak pia ina mfumo wa kujilinda. Huunda kinga ya digrii 360 kuzunguka kifaru. Mfumo huo hutambua mara moja tishio lolote na hurusha kombora na hulipua kombora linalokuja.

Droni za Spark

Droni za Spark zimeundwa kama sehemu ya mpango wa Jeshi la Anga la Israel. Zimeundwa na kampuni za Rafael Advanced Defence Systems na Aeronautics Group.

IDF haijafichua mengi kuhusu ndege hizi mpya. Imesema zitaboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi na uwezo wa askari wanaoendesha mashambulizi, kulingana na taarifa wanazopokea kutoka katika droni hizo.

Lakini IDF haielezi droni hizo zinafanyaje kazi.

Droni ya Kilo Tatu

Hizi ni katika toleo la ndege zisizo na rubani za Kamikaz, zina uzani wa kilo 3 tu na uwezo wa kubeba kombora moja.

Kulingana na mtengenezaji, hutumiwa zaidi katika maeneo askari wasiyoweza kuona. Inamaanisha zinaweza kuruka katika maeneo ya adui ambayo askari anayefanya kazi chini hawezi kuona.

Ndege hiyo isiyo na rubani ina uwezo wa kubaki hewani kwa hadi dakika 30 na kuwapa wanajeshi ufahamu wa hali ya mambo hadi kilomita 1.5.

Inakusanya taarifa na kuonyesha shahaba kwa amri ya askari ambaye anaidhibiti kwa kompyuta. Inaweza kurudi kambini - au ikiwa na kichwa cha kombora inaweza kushambulia shabaha.

Kombora la Iron Sting

Hutumia mionzi na GPS – limeundwa na kampuni ya ulinzi ya Elbit. Limetumika kwa mara ya kwanza Gaza Oktoba 2023, kwa mujibu wa IDF.

Kama ilivyoelezwa na mtengenezaji, Iron sting lina urefu wa milimita 120 – ni kombora linaloongozwa na hushambulia shabaha kwa usahihi. Linaweza kushambulia shabaha ya umbali wa kilomita 1-12.

Kombora hilo linaweza kupenya kuta nene za zege na kulipua, kulingana na Elbit.

Akili bandia katika vita (AI)

Matumizi ya akili bandia katika vita yanaelezwa - huifanya silaha kushambulia kwa usahihi zaidi na hivyo kupunguza uharibifu usiohitajika na mauaji ya wasio na hatia.

Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), wameelezea wasiwasi wao kuhusu matumizi ya akili bandia.

ICRC imesema, katika ripoti iliyotolewa mapema mwaka jana, "wajibu wa kisheria na wajibu wa kimaadili katika vita hayapaswi kutolewa na mashine na programu."

Wasiwasi huu unahusiana na mifumo ya silaha zinazojiendesha; mifumo ambayo mara inapoachiliwa hufanya kazi kwa uhuru kulingana na programu zake.

Mwaka 2023 IDF imetumia akili bandia kukusanya taarifa za kijasusi na kushambulia shabaha. Mifumo ya akili bandia ilikuwa inatumiwa tayari na Israel katika vita vya siku 11 huko Gaza, 2021.

Katika mahojiano na tovuti ya habari ya Israel ya Ynet News mwezi Juni 2023, mkuu wa zamani wa vikosi vya ulinzi vya Israel, Aviv Kochavi alitaja kitengo cha Targeting Directorate "kinajumuisha mamia ya maafisa na wanajeshi, wanaofanya kazi kwa kutumia mfumo wa akili mnembe."

"Ni mifumo ambayo huchakata kiasi kikubwa cha data haraka na kwa ufanisi zaidi kuliko binadamu yeyote, na kuzitafsiri katika malengo yanayotekelezeka," alisema.

"Katika siku za nyuma, tungegundua shabaha 50 huko Gaza kwa mwaka mmoja. Sasa, mifumo hii huonyesha shabaha 100 kwa siku moja," alielezea, akimaanisha operesheni ya 2021.

Mfumo wa Gospel

Mfumo wa Gospel umeundwa nchini Israel kwa kutumia akili bandia – unaendeshwa na Targeting Directorate na unafanya kazi masaa 24, kama ilivyoelezwa na IDF katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti yao tarehe 2 Novemba 2023.

Mfumo huu huonyesha shabaha kwa kuchakata kiasi kikubwa cha data zilizokusanywa na mashirika ya kijasusi ya Israeli katika ukanda wa Gaza. Hata hivyo, uamuzi wa utekelezaji unasalia mikononi mwa maafisa, kulingana na IDF.

Siku ya 27 ya vita, IDF ilisema kulikuwa na shabaha zaidi ya 12,000 katika Ukanda wa Gaza.

Yuval Abraham, mwandishi wa habari wa uchunguzi wa Israel anayeishi Jerusalem amekuwa akichunguza matumizi ya akili bandia katika vita vya Gaza.

Ripoti ya Abraham "Mass assassination factory” iliyoandikwa katika gazeti la +972 - gazeti huru la mtandaoni la waandishi wa habari wa Palestina na Israel.

Ripoti hiyo inatokana na mazungumzo na maafisa saba wa sasa na wa zamani wa mashirika ya kijasusi ya Israel, wakiwemo maafisa wa kijasusi wa kijeshi na wanajeshi wa anga ambao walihusika katika operesheni za Israel.

Abraham aliiambia BBC, “mfumo wa Gospel hutoa taarifa kuhusu wanaotaka kushambuliwa na nyumba zao pamoja na idadi ya raia ambao IDF huenda ikawauwa.”

IDF iliiambia BBC kuhusu madai hayo: "Katika kukabiliana na mashambulizi ya kikatili ya Hamas, IDF inafanya kazi ya kuharibu uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas. IDF inafuata sheria za kimataifa na huchukua tahadhari zinazowezekana ili kupunguza madhara ya raia.”

Kwanini idadi kubwa ya raia wanauwawa?

Kwa mujibu wa Yuval Abraham, vyanzo vyake vitatu ambavyo kwa sasa viko katika jeshi la Israel - vilizungumza kuhusu mamia ya raia wa Palestina waliouawa katika kila shambulio la kulenga kile wanachokitaja kama mwanachama mkuu wa Hamas.

Anasema chanzo chake kilimwambia "siku za nyuma wangeweza kuuwa makumi ya raia ili kuuwa kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Hamas. Lakini sasa idadi ya raia wanaoruhusiwa kuuawa ni mara 10 hadi 20 ya siku zilizopita."

Yuval aliiambia BBC, vyanzo vyake vilidai maafisa wanaoongoza operesheni ya kijeshi ya sasa huko Gaza "waliacha itifaki zote za hapo awali ambazo zinaweza kuzuia kushambuliwa raia."

IDF haikujibu maswali ya +972 lakini ilisema kwa ujumla: "IDF hutoa maonyo kabla ya mashambulizi kwa njia mbalimbali, na hali inaporuhusu, pia hutoa maonyo kwa mtu binafsi kwa njia ya simu kwa watu waliokuwa karibu na walengwa."

Kwa ujumla, IDF inafanya kazi ya kupunguza madhara kwa raia katika mashambulizi kadri inavyowezekana, licha ya changamoto ya kupambana na kundi la kigaidi linalotumia raia wa Gaza kama ngao.’’

Kanali wa zamani wa ujasusi wa jeshi la Uingereza, Philip Ingram ameiambia BBC "ikiwa Hamas itaweka vifaa vya kijeshi kwenye au karibu na miundombinu ya kiraia, itaigeuza sehemu hiyo kuwa shabaha halali ya kijeshi. Ilimradi lengo la kushambulia sehemu hiyo ni kuharibu shabaha hiyo, basi ni shabaha halali.”

"Israel ina jukumu la kufanya kila wawezalo kupunguza idadi ya majeruhi wa kiraia lakini hilo halimaanishi hawatouwa kabisa raia” amesema.

Mabomu yanayoongozwa na yasiyoongozwa

Tathmini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa Marekani iliyotolewa Disemba 2023, ikafichuliwa na CNN inasema, karibu 40-45% ya mabomu 29,000 ambayo Israel iliangusha Gaza, hayakuwa mabomu ya kuongozwa.

“Mabomu yasioongozwa yanaweza kukosa shabaha kwa hadi mita 30," Marc Garlasco, mchambuzi wa zamani wa kijasusi wa Pentagon na mchunguzi wa zamani wa uhalifu wa kivita wa Umoja wa Mataifa, meiambia BBC.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi