BBC yaingia ndani ya hospitali ya Al-Shifa na jeshi la Israel

Tunapanda kwenye jengo la Hospitali ya Al-Shifa kukiwa na giza kupitia ukuta uliopinda kwa ndani baada ya kugongwa na tingatinga la kivita siku ya Jumanne ili kuruhusu ufikiaji salama kwa vikosi vya Israeli.

BBC na wafanyakazi wengine wa televisheni walikuwa waandishi wa habari wa kwanza walioalikwa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kutazama kile Israel inasema imekipata kwenye eneo hilo.

Mwangaza wowote wa ziada hapa ni hatari kwa hivyo tunapapasa , tukifuata askari wenye silaha nzito waliotumwa kutusindikiza - kuzunguka mahema ya muda, vifusi na watu waliolala.

Madaktari katika hospitali hiyo wanasema wamekuwa wakifanya kazi bila umeme, chakula au maji kwa siku nyingi sasa - na kwamba wagonjwa mahututi wamekufa kutokana na hilo, wakiwemo watoto wachanga. Watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano huko Gaza wamekuwa wakipata hifadhi katika hospitali hiyo.

Lakini Israel inasema Hamas pia inaendesha mtandao wa njia za chini ya ardhi, ikiwa ni pamoja na chini ya Hospitali ya Al-Shifa.

Vikosi maalum vilivyofunika nyuso vinavyotuongoza ndani ya jengo juu ya vifusi na vioo vilivyovunjika ni ishara ya jinsi hali bado ilivyo. Uwepo wetu, siku moja tu baada ya Israeli kuchukua udhibiti wa hospitali, unazungumzia mengi juu ya Israeli kuonyesha ulimwengu kwa nini wako hapa.

Katika korido zenye mwanga wa kitengo cha MRI, Luteni Kanali Jonathan Conricus anatuonyesha picha tatu ndogo za Kalashnikovs, risasi na fulana za kuzuia risasi - anasema wamepata karibu bunduki 15 kwa jumla, pamoja na baadhi ya mabomu.

Lt Kanali Conricus pia anatuonyesha baadhi ya vijitabu vya kijeshi, na ramani ambayo anasema imewekwa alama ya njia za kuingia na kutoka hospitalini.

Inachotuambia, anasema, ni kwamba Hamas hutumia hospitali kwa madhumuni ya kijeshi. "[Na] tuligundua kompyuta nyingi na vifaa vingine ambavyo vinaweza kutoa mwanga juu ya hali ya sasa, kwa matumaini kuhusu mateka pia."

Kompyuta hizo, anasema, zina picha na video za mateka, waliochukuliwa baada ya kutekwa nyara hadi Gaza. Pia kuna picha zilizotolewa hivi karibuni, zilizoshirikiwa na polisi wa Israel, za kuwahoji wapiganaji wa Hamas waliokamatwa baada ya mashambulizi ya Oktoba. BBC haikuonyeshwa kilichokuwa kwenye kompyuta za mkononi.

Hii, Luteni Kanali Conricus anasema, inaonesha Hamas walikuwa hapa "katika siku chache zilizopita".

"Mwisho wa siku, hu ni mfano tu," alisema. "Hamas hawapo hapa kwa sababu waliona tunakuja. Hii labda ndicho walilazimika kuwacha nyuma kabla ya kuondoka. Tathmini yetu ni kwamba kuna mengi zaidi."

Jeshi la Israel limetumia wiki kadhaa kupigana hadi kwenye lango la hospitali hiyo. Mitaa inayozunguka imeshuhudia mapigano makali zaidi huko Gaza katika siku chache zilizopita.

Ziara yetu ilidhibitiwa vikali; tulikuwa na wakati mchache sana na hatukuweza kuzungumza na madaktari au wagonjwa huko.

Safari yetu ya kuelekea Gaza, tukiwa ndani ya shehena ya kivita iliyozibwa, ilifuatilia njia ya mashambulizi ya kwanza ya ardhini ya Israeli kuingia Gaza wiki zilizopita.

Kwenye skrini ndani ya gari la kijeshi, ardhi ya kilimo ilibadilika polepole katika mitaa iliyotawanyika na vipande vikubwa vya uchafu, na majengo yaliyovunjwa.