Raia 120,000 wa Israel waomba bunduki kwa mara ya kwanza

Tangu shambulio la Oktoba 7, ambapo zaidi ya watu 1,400 waliuawa na wanamgambo wa Hamas, zaidi ya maombi 120,000 mapya ya leseni ya silaha yamewasilishwa na raia wa Israel.

Harakati za kupata bunduki kihalali zinafanyika kote nchini. Masafa ya upigaji risasi yana shughuli nyingi na idadi isiyokuwa ya kawaida ya Waisraeli wanaotaka kuboresha ujuzi wao. Nje ya maduka ya bunduki, foleni kubwa za watu wanaosubiri kununua silaha yao ya kwanza inaongezeka.

Kufuatia tangazo la serikali ya Israel kwamba italegeza sheria zake za umiliki wa bunduki, wale ambao hawana rekodi ya uhalifu au matatizo ya kiafya, sasa wanaweza kupata leseni ya bunduki ndani ya wiki moja. Watu binafsi pia wataruhusiwa kumiliki hadi risasi 100, kutoka 50.

"Sasa, ni rahisi kupata bunduki, kwa sababu waliondoa vikwazo vyote" anasema Omri Shnaider, wakili mwenye umri wa miaka 41 kutoka Kibbutz nje kidogo ya mji wa Jerusalem.

Lakini Bw Schnaider licha ya kufurahia uamuzi wake, ana wasiwasi kuhusu athari za maelfu ya silaha zinazotolewa kwa raia.

"Kuna faida, lakini pia hasara. Tunaona kile kilichotokea Marekani. Sio uamuzi rahisi. Lakini hili ndilo ninahisi nahitaji kufanya, ili kuwafanya watu wa Israeli wajisikie salama."

Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa Mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir, mtetezi wa muda mrefu wa umiliki wa bunduki za kibinafsi, amekuwa akizuru nchi akitoa maelfu ya silaha.

Alisema silaha hizo mpya ni maalum kwa ajili ya wale wanaoishi karibu na mpaka na Gaza au katika miji yenye mchanganyiko wa Wayahudi na Waarabu na kuzihimiza jumuiya hizo zote za Kiyahudi kuunda makundi ya usalama za raia.

Bw Schnaider anaishi Kibbutz ambako ni nyumbani kwa familia 200. Anaunga mkono wazo hili la "hatua ya kiraia".

"Kwa sababu ya hali hiyo, hapa Kibbutz tuliamua kuwa bunduki na kuunda makundi ya walinzi wa kitongoji. Kikosi hiki cha watoa huduma za dharura kitaingilia kati ikiwa kutakuwa na mashambulizi, Mungu apishe mbali."

Lakini wakati idadi kubwa ya Wayahudi wakitafuta njia za kuimarisha usalama wao, Waarabu wa Israel, ambao ni zaidi ya asilimia 20 ya watu wote, wanasema hawajawahi kuwa na hofu.

Matukio ya ubaguzi, matusi na unyakuzi mtandaoni yameripotiwa kwa BBC na raia wa Israel Waarabu kutoka kote nchini.

Mji wa Lod katikati mwa Israel una historia chungu ya unyanyasaji na ubaguzi wa rangi kati ya Wayahudi na Waarabu.

Suhair Hamdouni, mwalimu wa watoto wenye ulemavu, ameishi Lod maisha yake yote. Upande mmoja wa barabara kuna nyumba za Wayahudi, upande mwingine za Waarabu.

Anasema tangu mashambulizi hayo, haendi tena kununua mboga katika eneo la Wayahudi lakini hutembea umbali mrefu hadi kwenye maduka ya Kiarabu, kwa kuhofia kushambuliwa.

"Tumevamiwa katika nyumba zetu hapo awali. Tayari tunapambana na kiwewe."

Raia wa Kiarabu wa Israel, ambao sana sana hujitambulisha kama Wapalestina, kwa ujumla hawalazimiki kujiunga na na mafunzo ya kijeshi kwa lazima. Bila mafunzo haya, ni vigumu zaidi kwao kupata leseni ya bunduki.

"Nina wasiwasi kwamba wakati Waisraeli wanatumia haki yao ya kujitetea, ninaweza kuishia kufa. Mimi na wanangu.

"Si kwa sababu nilifanya kosa lolote. Lakini kwa sababu mimi ni Mwarabu. Ikiwa Wayahudi katika mtaa wangu wana haki ya kupata bunduki, basi mimi pia nipate au pande zote mbili zisipate bunduki."

Tangu shambulio la Hamas, miji yenye mchanganyiko wa wakazi nchini Israel, ambayo hapo awali ilishamiri na watalii wa ndani, imesalia mahame. Maduka yamefungwa na migahawa yote imefungwa.

"Zaidi ya 60% ya wateja wangu walikuwa Wayahudi," anasema mmiliki wa mgahawa wa Lod, Abu Amir.

"Lakini sasa, hawaji. Hakuna anayekuja. Hakuna anayeita. Waarabu wanaogopa kwenda katika vitongoji vya Wayahudi na Wayahudi wanaogopa kwenda katika miji ya Waarabu."