Nchi 10 bora kwa usawa wa kijinsia: Afrika ipo moja

aszx

Chanzo cha picha, Chad Case/Alamy

Maelezo ya picha, Maendeleo ya usawa wa kijinsia yakoje ulimwenguni?
    • Author, Amanda Ruggeri
    • Nafasi, BBC

Maendeleo ya usawa wa kijinsia yakoje ulimwenguni? Kwa mujibu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF), mambo yanasonga katika mwelekeo sahihi kulingana na ripoti yake ya hivi karibu ya Pengo la Usawa wa Kijinsia Ulimwenguni.

Kwa kiwango cha sasa cha maendeleo, ripoti imegundua kuwa itachukua miaka 131 kufikia usawa kamili wa kijinsia. Na hakuna nchi ambayo imefikia usawa huo kikamilifu.

Ingawa nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini zina mwelekeo wa kufanya vizuri zaidi kuliko nchi nyingine ulimwenguni. Marekani, kwa mfano, inashika nafasi ya 43, huku pengo la usawa wa kijinsia likiwa chini ya asilimia 75, nyuma ya nchi zikiwemo Colombia, Belarus, Liberia na Cabo Verde.

Nchi nyinginre ni Australia imeziba pengo hilo kwa 77.8% ikishika nafasi ya 26, nyuma ya Msumbiji na Chile. Canada 77% imeshika nafasi ya 30, nyuma ya Slovenia na Barbados.

Ripoti inazingatia vipengele kama vile ushiriki wa wanawake kiuchumi - ikiwa ni pamoja na mapato, ajira na majukumu ya uongozi, elimu, viwango vya kusoma na kuandika na uandikishaji katika mashule.

Vilevile masuala ya afya na maisha - kama vile umri wa kuishi na uwezeshaji wa kisiasa, yaani uwakilishi wa wanawake katika bunge, nafasi za uwaziri na mkuu wa nchi mwanamume au mwanamke.

Nchi 10 bora kwa usawa wa kijinsia - 2023

1. Iceland imeziba pengo kwa 91.2%

2. Norway kwa 87.9%

3. Finland kwa 86.3%

4. New Zealand kwa 85.6%

5. Sweden kwa 81.5%

6. Germany kwa 81.5%

7. Nicaragua kwa 81.1%

8. Namibia kwa 80.2%

9. Lithuania kwa 80%

10. Belgium kwa 79.6%

Iceland

SZX

Chanzo cha picha, New Zealand Transition/Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa mwaka wa 14 mfululizo, Iceland inachukua nafasi ya juu katika viwango vya WEF
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mwaka wa 14 mfululizo, Iceland inachukua nafasi ya juu katika viwango vya WEF, huku pengo la kijinsia likikadiriwa kudhibitiwa kwa 91.2%. Ni nchi pekee iliyoziba zaidi ya 90% ya pengo lake.

Iceland inashika nafasi ya kwanza katika suala la uwezeshaji wa kisiasa, kutokana na ukweli kwamba kaŕibu miaka 25 kati ya 50 iliyopita imeshuhudia mkuu wa nchi mwanamke na asilimia 48 ya wabunge wake ni wanawake.

Lakini iko katika nafasi ya 79 katika ufaulu wa elimu na ya 128 kwa afya ya wanawake na makadirio ya wanawake kuishi. Katika pengo la mishahara nchi hiyo inafanya vizuri. Pengo la mishahara kati ya jinsia ni dogo kuliko nchi nyingine nyingi.

Hii ni kutokana na sheria ya 2018 iliyotangaza kwamba makampuni yenye wafanyakazi zaidi ya 25 lazima yatoe malipo sawa kwa kazi sawa (au yatapigwa faini).

Bado, wanawake wa nchi hiyo wanasema, kuna mengi ya kufanyika. Mke wa Rais wa nchi hiyo Eliza Reid, m-Canada aliyehamia Iceland, anakubali kwamba nchi ina safari ndefu na sio "pepo ya kijinsia." Anaamini, ni "jamii ambayo wanawake wanatendewa sawa na wanaume, au angalau, nia ya kufanya hivyo ipo."

Miongoni mwa mambo mengine nchi hiyo, imeorodheshwa kama mojawapo ya nchi zenye furaha zaidi na zenye amani zaidi.

Norway

az\

Chanzo cha picha, Jordan Siemens/Getty Images

Maelezo ya picha, Norway inashika nafasi ya pili katika viwango vya WEF vya 2023

Norway inashika nafasi ya pili katika viwango vya WEF vya 2023, imefanikiwa kuliziba pengo la usawa kijinsia kwa 87.9%. Pia ilishika nafasi ya kwanza katika Fahirisi ya Amani na Usalama wa Wanawake ya 2021.

"Usawa wa kijinsia unaonekana kabisa nchini Norway," anaeleza Thea Ringseth, mzaliwa wa Norway. "Kuna wanawake wengi zaidi katika nyadhifa ambazo kwa kawaida walikuwa wapo wanaume, kama waziri mkuu, ambaye kwa miaka minane iliyopita alikuwa mwanamke, na kuna viongozi wengi wa kike serikalini na nyadhifa nyingine muhimu."

Nje ya siasa, Norway inafanya vyema katika masuala ya ujuzi wa kusoma na kuandika wa wanawake - inachukua nafasi ya kwanza. Idadi ya wafanyakazi wa kike kitaaluma na kiufundi pia ya kwanza na usawa wa mapato iko nafasi ya sita.

Bila shaka, Norway haijafikia 100% usawa wa kijinsia - na hilo linaonekana katika mitazamo ya watu. "Inatarajiwa kwamba ikiwa mtoto wako ni mgonjwa, kwa mfano, kwa kawaida ni mama ambaye anabaki nyumbani," Ringseth anasema.

Wakati huo huo, kuna uhuru na uwezeshaji kwa raia wote wa Norway ambao Ringseth anauthamini sana. "Kama jamii, haikuzuii kuendeleza mahitaji yako kama elimu, fani, mahitaji yako ya kijamii, kiuchumi [kama mwanamke]," anasema.

New Zealand

EDSAXZ

Chanzo cha picha, Jordan Siemens/Getty Images

New Zealand inashika nafasi ya nne kwenye ripoti ya WEF. Inafanya vizuri katika masuala ya uwakilishi wa kisiasa, huku asilimia 50 ya wabunge wake wakiwa wanawake, wakati uandikishaji wa wanawake katika elimu ya msingi na sekondari unakaribia kuwa sawa na wanaume.

Jessica Redenburg, m-Canada anayeishi New Zealand tangu 2016, ni profesa wa masoko katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Auckland.

"Kwa uzoefu wangu, angalau katika taaluma ya biashara, mgawanyiko wa kijinsia ni sawa kabisa. Katika idara yetu ya masoko, tunaweza hata kusema wanawake ni wengi kuliko wanaume. Mkuu wangu wa kitivo ni mwanamke. Wenzangu wengi ni wanawake."

Lakini kwa usawa wa mishahara inashika nafasi ya 37. WEF iligundua kuwa wanawake wanapata wastani wa dola za kimarekani 33,620 kwa mwaka ikilinganishwa na 52,370 kwa wanaume.

Pia inafanya vibaya kwa umri wa kuishi wa wanawake. Ipo katika nafasi ya 109 duniani. Jamii ya Wamaori wako katika hatari fulani, takwimu zinaonyesha umri wa kuishi wa wanawake wa Māori ni mfupi kwa miaka saba kuliko ule wa wanawake wasio Wamaori.

Namibia

sdfxc

Chanzo cha picha, Keren Su/Alamy

Maelezo ya picha, Nchi pekee ya Kiafrika katika 10 bora, pengo la usawa kijinsia linakadiriwa kuzibwa kwa 80.2%

Nchi pekee ya Kiafrika katika 10 bora, pengo la kijinsia la Namibia linakadiriwa kuzibwa kwa 80.2%, na kuiweka katika nafasi ya nane. Hiyo ina maana kwamba inazishinda nchi nyingi katika sehemu nyingine za dunia, ikiwa ni pamoja na Uingereza ya 15 kwa 79.2%, Uhispania ya 18 kwa 79.1%, Canada ya 30 kwa 77% na Marekani ya 43 kwa 74.8%.

Nafasi ya nchi hiyo ina maana kubwa kwa Penohole Brock, mkufunzi wa masuala ya jinsia katika Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano.

"Mawaziri wetu wengi ni wanawake. Mabalozi wetu wengi ni wanawake. Na wafanyakazi wenzangu, naweza kusema, hawakumbani na ubaguzi linapokuja suala la mwelekeo wa kazi - kuna mazingira mazuri ya kazi."

"Usawa wa kijinsia ni hatua kubwa katika mwelekeo sahihi. Lakini kwa upande wa unyanyasaji wa kijinsia bado tuna safari ndefu."

Fahirisi ya Amani na Usalama ya Wanawake ya mwaka 2021, iliiweka Namibia ya 95, nyuma ya nchi nyingine za Kiafrika zikiwemo Mauritius, Rwanda, Afrika Kusini na Ghana.

Brock ambaye pia ameishi Afrika Kusini na Paris, anasema asingependa kuwa popote pengine. "Watu, muziki, furaha – naipenda hii nchi. Namibia ni mahali pazuri."