Vita vya Ukraine: Jamii ya Tatars ya Crimea inayoisumbua Urusi

Tatars wa Crimea, kabila linalotoka katika rasi inayokaliwa na Warusi, wamekuwa mashuhuri katika vita vya Ukraine.

Harakati ya kijeshi ya Atesh, ambayo ina maana ya moto, imeapa kuendeleza vita visivyo na mwisho dhidi ya wavamizi wa Kirusi.

Kikundi hicho kilianzishwa mnamo Septemba 2022, kinataka kuvuruga vifaa, kuhujumu malengo muhimu ya wapinzani na kutoleta utulivu dhidi na ndani ya jeshi la Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mbinu za Atesh ni za kikatili, kama ilivyoshuhudiwa mauaji ya wanajeshi 30 wa Urusi katika hospitali za Simferopol mnamo Novemba 2022.

Mnamo Februari mwaka huu, kundi hilo lilidai kuwa zaidi ya wanajeshi 4,000 wa Urusi walikuwa tayari wamechukua kozi ya mtandaoni, katika "shule ya Atesh", ya jinsi ya kunusurika kwenye vita kwa njia za hujuma.

Mustafa Dzhemilev, kiongozi wa Tatar ambaye amepigwa marufuku huko Crimea ilipo asili yake hadi mwaka 2034, hivi karibuni alisema kwamba "Atesh inafanya kazi chinichini, lakini wanafanya kazi ndani ya Crimea."

Serhii Kuzan, mkuu wa Kituo cha Usalama na Ushirikiano cha Ukraine, taasisi ya wanafikra yenye makao yake makuu mjini Kyiv, anasema kuwa: "Wazo ni kwamba mvamizi daima atahisi uwepo wa wapiganaji na kwamba kamwe hawatajiona salama."

Wanaharakati, ikiwa ni pamoja na Atesh, wanatumia mbinu mbalimbali kudhoofisha Warusi huko Crimea na hata nje ya mipaka ya eneo hilo.

"Hatima ya askari wa Hitler inakusubiri"

Atesh ilipodai kuhusika na shambulio dhidi ya wanajeshi wa Urusi katika hospitali za Simferopol, alionya: "Kagua wodi, angalia vyumba vya kuhifadhia maiti... unaweza kuthibitisha ukweli huu mara 300 lakini ndio ukweli."

Kama ilivyo kwa matukio mengi katika vita hivi, na hii inatumika kwa vitendo vinavyofanywa na pande zote, kuthibitisha madai kama hayo ni kazi ngumu sana.

Tunachojua ni kwamba vikosi vya waasi katika maeneo ya Kharkiv, Zaporizhia na Kherson hivi karibuni vilianzisha kampeni iliyoratibiwa na mabango madogo na vipeperushi dhidi ya ulimwengu unaoitwa Urusi.

Zaidi ya hayo, ikiiga mbinu iliyotumiwa katika migogoro iliyotangulia, inaripotiwa kwamba Ukraine ilisambaza vipeperushi kwenye maeneo ya jeshi la Urusi vikiwa na ujumbe huu: “Askari wa Urusi, ikiwa hutaki kuwa Mnazi wa karne ya 21, basi ondoka katika ardhi yetu! Vinginevyo, hatima ya askari wa Hitler na Mahakama ya Nuremberg inakungoja."

Mbinu hiyo ya zamani ni ya kuvutia kwa Kyiv, kwani vita vya msituni vilichukua jukumu kubwa katika kushinda Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Urusi (1917-1923) na kile Urusi inakumbuka kama "Vita Kuu ya Uzalendo" (1941-1945).

Ulinganisho wa jeshi la sasa la Urusi na wavamizi wa Nazi katika Vita vya pili vya dunia haufanani kabisa na kinachoendelea sasa chini ya Putin.

Ikulu ya Kremlin inawashutumu wazalendo wa Ukraine kwa kushirikiana na kufanya mauaji makubwa wakati wa uvamizi wa Nazi.

Propaganda za Kirusi zinadai kwamba vita vya sasa vimeundwa "kuondoa ushawishi wa Nazi" Ukraine.

Tatars ni akina nani?

Tofauti na Warusi wa Slavic, Tatars wa Crimea ni kabila la Turkic linalotoka kwenye Peninsula ya Crimea.

Taifa la Tatars la Crimea liliundwa kwa zaidi ya karne nne (c.1200-c.1650) likijumuisha wahamiaji.

Tsarina Catherine alitwaa Crimea mnamo 1783, kabla ya mapinduzi ya mwaka 1917.

Chini ya utawala wa Joseph Stalin (1924-1953), Umoja wa Kisovyeti ulishiriki katika ukandamizaji mkubwa wa Tatars wa Crimea.

Hilo lilifanya Tatars kadhaa kushirikiana na Wajerumani kufuatia uvamizi wa Wanazi wa Juni 1941.

Stalin aliwashutumu Watatari wa Crimea kwa uhaini na kumfukuza jamii kwa wingi hadi Gulag.

Ingawa Watatari wengine wa Crimea walitetea nguvu za Axis, wengi zaidi walihudumu katika Jeshi Nyekundu.

Machungu ya zamani

Kuhamishwa kwa angalau watu 180,000 kwenda Asia ya Kati mnamo 1944 ilikuwa moja ya hatua chungu zaidi katika historia ya Tatars, inayokumbukwa kama Sürgün (uhamisho).

Katika miaka ya 1960, utafiti wa wanaharakati wa Tatars ulikadiria kuwa takriban watu 100,000 kati ya hao waliohamishwa walikufa (na hata rekodi za Soviet zinakubali kwamba Tatars 30,000 wa Crimea ndani ya miaka miwili baada ya kufukuzwa).

Ilikuwa hadi Septemba 1967 ambapo Baraza Kuu la Kisovieti, chombo cha juu zaidi cha kutunga sheria cha Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR), kilitambua kwamba shtaka la uhaini dhidi ya taifa zima la Tatars la Crimea lilikuwa jambo "lisilo na sababu".

Miaka kumi na tatu kabla, Baraza Kuu la Soviet lilipiga kura kuihamisha Crimea iwe sehemu ya Ukraine kutoka kwa Urusi.

Kitendo kama hicho hakikuwa na utata wakati huo, ikizingatiwa kwamba Mamlaka zote mbili zilikuwa sehemu za Muungano wa Sovieti.

Kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991 kulibadilisha yote hayo.

Tatars wengi waliruhusiwa tu kurudi Crimea mwaka wa 1989, chini ya kiongozi wa mageuzi wa Soviet Mikhail Gorbachev.

Tatars hawakupata fidia kwa kilichowakuta, na kurudi kwao nyumbani kulizua mvutano kati ya Warusi na Waukraine, ambao wengi wao walikuwa wamehamia Peninsula baada ya mwaka 1944.

"Watu bora wa Ukraine huko Crimea"

Baada ya Ukraine kuwa huru mwaka 1991, viongozi wa Tatars walidai kuwa mamlaka ya Kyiv iliwazuia kimakusudi watu wao kupata kazi za serikali, huku wakiruhusu kwa siri "unyakuzi wa ardhi."

Hatua kwa hatua, hilo likawaunganisha Tatars wa Crimea na Ukraine.

Tatars wa Crimea wakawa wafuasi wenye bidii wa taifa jipya la Ukraine na wakati mwingine walipewa jina la utani "Waukraine bora zaidi huko Crimea".

Mnamo mwaka 1897, Tatars wenye asili wa Crimea walikuwa wengi karibu asilimia 34.1% ya wakazi wote wa Peninsula hiyo.

Licha ya mabadiliko ya Stalin ya utakaso wa kikabila, mnamo 2001 Warusi wakawa asilimia 58% ya wakazi wote wa Crimea, wakati Tatars asilia walikuwa asilimia 12% tu.

Uvamizi wa Urusi huko Crimea mnamo 2014 ulirejesha kumbukumbu mbaya kwa Tatars wa Crimea.

Warusi mara moja walianza mpango wa udhalimu. Mateso haya yanaendelea hadi leo.

Bunge la Watu wa Tatars wa Crimea, linalojulikana kama Tatar Mejlis, ambalo rais wake alikuwa Mustafa Dzhemilev, lilipigwa marufuku.

Baada ya 2014, maelfu ya Tatars waliondoka Crimea iliyokaliwa na Urusi na kuelekea Ukraine.

Mwanaharakati wa Tatars na mwanasiasa Ilmi Umerov aliiambia Huduma ya Usalama ya Shirikisho la Urusi kwamba "hakuona Crimea kama sehemu ya Shirikisho la Urusi."

Kwa kauli hiyo alipelekwa hospitali ya magonjwa ya akili.

Kuonyesha mshikamano wa Ukraine na Tatars, mnamo Novemba 2015 Verkhovna (Bunge la Ukraine) lilipitisha hoja ya kushutumu uhamishaji wa watu wa mwaka 1944 kama "mauaji ya kimbari." Ilikuwa ni mfano ambao ulihimiza Latvia, Lithuania na Canada kufanya vivyo hivyo mnamo 2019.

Mnamo 2021, Bunge hilo lilipitisha sheria inayotambua Tatars wa Crimea kama moja ya watu asilia wa Ukraine.

Wakati vita vya sasa vinaendelea, na kwa kuzingatia mchango mkubwa wa kijeshi wa Tatars wa Crimea, Kyiv italitazama suala la kujitawala vyema na vizuri kwa taifa la Tatars wa Crimea.

Msomi wa masomo ya Kiukreni Rory Finnin anasema kuwa mustakabali wa Crimea ni msingi wa mpango wowote ambao unaweza kufuata vita vya sasa.

Ukraine ilipoteza udhibiti wa Crimea mwaka 2014, lakini juhudi za Tatars wa Crimea katika mzozo wa sasa zinachangia kwa kiasi kikubwa uwezo wa Kyiv kuepuka kushindwa vita na Urusi.