Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
BBC yafichua uharibifu wa vituo vya maji vya Gaza
Mamia ya vituo vya maji na mifereji ya maji taka vya Gaza vimeharibiwa au kuangamia kabisa tangu Israel ilipoanza kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Hamas, uchunguzi wa satelaiti na BBC Verify umegundua.
Uharibifu wa bohari kuu ya vifaa pia umetatiza sana ukarabati.
Ukosefu wa maji safi na mtiririko wa maji taka ni tisho kubwa kwa afya, yanasema mashirika ya misaada.
Jeshi la Israel limeiambia BBC kuwa Hamas hutumia vibaya miundo mbinu ya raia kwa malengo ya kigaidi.
Uharibifu huo unakuja licha ya wajibu wa Israel kulinda miundombinu muhimu chini ya sheria za vita, isipokuwa kama kuna maeneo ya ushahidi yanayotumiwa kwa sababu za kijeshi, wanasema wanasheria wa haki za binadamu.
Maji safi daima yamekuwa rasilimali ndogo huko Gaza na eneo hilo kwa kiasi kikubwa linategemea mfumo wa visima na mimea ya kuondoa chumvi kwa usambazaji wake.
Uchambuzi wetu uligundua kuwa zaidi ya nusu ya vituo hivi muhimu vimeharibiwa au kuharibiwa tangu Israel ilipoanzisha kulipiza kisasi huko Gaza baada ya Hamas kushambulia tarehe 7 Oktoba.
Pia tuligundua kuwa mitambo minne kati ya sita ya kutibu maji machafu - muhimu katika kuzuia mkusanyiko wa maji taka na kuenea kwa magonjwa - imeharibiwa au kuharibiwa. Wengine wawili wamefunga kwa sababu ya ukosefu wa mafuta au vifaa vingine, kulingana na shirika moja la misaada.
Mitambo hiyo ilikuwa kati ya zaidi ya vifaa 600 vya maji na usafi wa mazingira ambavyo tulichanganua, kwa kutumia orodha ya maeneo yaliyotolewa na Shirika la Maji la Manispaa ya Pwani ya Gaza (CMWU).
Katika picha moja ya satelaiti, ya Khan Younis kusini mwa Gaza, matangi mawili makubwa ya kuhifadhia maji yaliyoharibika yanaweza kuonekana.
Uharibifu wa vifaa vya maji na usafi wa mazingira umesababisha "matokeo mabaya ya kiafya kwa idadi ya watu", alisema Dk Natalie Roberts, mkurugenzi mtendaji wa Medecins Sans Frontiers nchini Uingereza.
"Viwango vya ugonjwa wa kuhara vimepanda kwa kasi kubwa," alisema.
Katika hali mbaya sana, ugonjwa huo unaweza kuua watoto wadogo na wale walio katika mazingira magumu. Viwango vya homa ya ini A - inayopatikana katika maji machafu na hatari hasa kwa wanawake wajawazito - pia ni vya juu, kulingana na shirika hilo la misaada.
"Hii inaua watu," Dk Roberts alisema.
Kuna ongezeko fulani la ugonjwa huko Rafah kusini ambako watu wengi wa Gaza wamekimbilia, Dk Roberts aliongeza, na hatari ya kipindupindu.
Kumekuwa na uharibifu mkubwa kwa majengo kote Gaza tangu Hamas ilipoishambulia Israel tarehe 7 Oktoba.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban nyumba 69,000 zimeharibiwa na nyingine 290,000 kuangamia kabisa
Nyumba kwa sasa "hazina uwezekano mkubwa" wa kuwa na maji ya bomba, kulingana na wafanyakazi wa misaada tuliozungumza nao.
Uchunguzi wa satelaiti ya BBC
Ili kufanya uchambuzi huu tuliomba ushauri kutoka kwa wataalamu katika Umoja wa Mataifa na shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch kuhusu mbinu bora zaidi ya kutathimini hali.
Kwa kila eneo, tulipata picha za hivi karibuni za ubora wa juu za satelaiti na tukailinganisha kila picha yetu na picha iliyopigwa kabla ya tarehe 7 Oktoba.
Kisha tulitia alama kituo kuwa kimeharibiwa au kuangamia iwapo mfumo wa maji karibu zaidi wa viwianishi vilivyotolewa ulionekana kubakia kuwa vifusi, kuporomoka kwa kiasi au kuonyesha dalili nyingine za uharibifu.
BBC Verify haijatofautisha kati ya vifaa "vilivyoharibiwa" na "vilivyoangamizwa". Hii ni kwa sababu bila kujua muhtasari sahihi wa kila kituo, hatuwezi kusema ikiwa kimeharibiwa kwa kiasi au kuharibiwa kabisa.
Visima vya maji kwa kawaida huwa na kisima cha chini ya ardhi na pampu ya umeme, pamoja na chumba kidogo cha kudhibiti maji juu ya ardhi.
Lakini kwa kuwa chumba cha kudhibiti hakionekani kila wakati au kutambulika kwa urahisi tulilazimika kutegemea kuchambua majengo yaliyo karibu zaidi wakati wa kutathmini uharibifu.
Tulichobaini
Kati ya vituo 603 vya maji tulivyochanganua, 53% kati yake vilionekana kuharibiwa au kuangamizwa tangu tarehe 7 Oktoba.
Vituo vingine 51 vilikuwa katika maeneo ambayo yalionyesha kuwa na uharibifu fulani au ambapo mitambo ya nishati ya jua ilikuwa zimeondolewa, lakini hatukuweza kubaini kama kituo cha maji chenyewe kilikuwa kimeharibiwa kwa hivyo haya hayakujumuishwa katika uchambuzi wetu.
Picha za hivi punde za setilaiti zinazopatikana ni za mwezi wa Machi na Aprili, na uchanganuzi wetu umekuwa ukiendelea tangu Aprili.
Maeneo mengi yaliyotambuliwa kuwa yameharibiwa au kuangamizwa kabisa yapo kaskazini mwa Gaza au katika eneo karibu na mji wa kusini wa Khan Younis.
Katika kituo kimoja cha maji machafu huko Bureij, katikati mwa Ukanda huo, mitambo ya nishati ya jua ambayo nguvu yake ilikuwa imefunikwa na matanki ya kusafisha maji taka ilionekana kuwa na mwani unaomea juu yake.
Sio uharibifu wote unaoonekana kwa picha za setilaiti, kwa hivyo uchanganuzi wetu unaweza kuwa umekosa baadhi ya vifaa vilivyoathiriwa. Baadhi ya mifumo ya maji pia huenda haifanyi kazi kikamilifu kwa sababu ya ukosefu wa mafuta.
Kwa mfano, kiwanda cha kuondoa chumvi kwenye maji cha Unicef huko Deir al-Balah - mojawapo ya vituo vitatu vikubwa vya maji ya bahari huko Gaza - kinaweza kufanya kazi kwa asilimia 30 tu kwa sababu ya ukosefu wa mafuta, Unicef iliiambia BBC.
Huku watu wengi wa Gaza sasa wakihama makwao, na kuishi katika kambi za mahema, kuongezeka kwa maji taka mitaani ni tisho zaidi.
"Pampu za maji taka hazifanyi kazi na mitaa imejaa [maji hayo]," alisema Muhammad Atallah, ambaye anafanya kazi katika Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina.
Uharibifu wa bohari muhimu ya ukarabati
Mgogoro huo tayari umefanya ukarabati wa vituo vya maji kuwa mgumu kwa mamlaka ya maji ya Gaza, lakini shambulio kwenye ghala kuu la ukarabati umeifanya hali kuwa ngumu zaidi.
Jengo la bohari lililo katika kitongoji cha al-Mawasi, liliharibiwa vibaya katika shambulio la kombora tarehe 21 Januari. Watu wanne walifariki na wengine 20 kujeruhiwa, kulingana na CMWU.
mkurugenzi mkuu wa CMWU, Monther Shoblaq, aliiambia BBC kuwa ghala hili, ambalo lilifanya kazi kama bohari ya CMWU na Unicef, lilikuwa na zaidi ya vfaa 2,000 vilivyotumika kwa matengenezo, na lilikuwa kitovu cha huduma za maji na vyoo huko Gaza.
Uharibifu wake umepunguza sana uwezo wa CMWU wa kukarabati na kudumisha vifaa muhimu kama mabomba ya maji, alisema.
Jeshi la Israeli- IDF, ilisemabohari hiyo haikulengwa, lakini magaidi wa Hamas waliokuwa wakiendesha shughuli zao karibu walipigwa na "inawezekana kwamba sehemu za zake zilipata uharibifu kutokana na shambulio hilo".
Tuliipa IDF sampuli ya maeneo mengine matano ya maji yaliyoharibiwa au kuangamia kutoka kwa uchanganuzi wetu. Katika kesi moja, IDF ilikanusha kuwa kulikuwa na shambulio la anga, katika matukio mengine manne ilisema wapiganaji wa Hamas au mahandaki yao ndio waliokua walengwa halisi wa mashambulio yao.
"Hamas huhifadhi silaha na risasi ndani ya majengo haya ya kiraia, hujenga miundombinu ya ugaidi chini yao, na kutoka kwenye mahandaki ya chini ya majengo, hufanya mashambulizi yake ... IDF inatafuta na kuharibu miundombinu hii ya ugaidi, ambayo imegunduliwa, miongoni mwa maeneo mengine, ndani na karibu na maji na vifaa vinavyohusika."
Leila Sadat, mshauri maalum wa uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, aliiambia BBC kwamba vituo muhimu kwa maisha ya raia vinapaswa kulindwa isipokuwa pale ambapo chombo cha kijeshi kina ushahidi madhubuti wa kupendekeza vinginevyo.
Ili kutathmini vitendo vya vita katika suala la uhalali, unahitaji kuzingatia "mfano" wa hatua hizo, alisema.
"Huwezi tu kuangalia shambulizi... na kusema [ahaa [IDF] wamepiga mabomba ya maji, matanki, hifadhi, na miundombinu," alisema.
"Kuteka udhibiti wa nusu ya maji na usafi wa mazingira itakuwa vigumu sana bila kufanya hivyo kimakusudi. Kwa hivyo hatua hiyo ni ushahidi wa mbinu za kizembe au uharibifu wa kukusudia; haya yote hayakuwa makosa," aliongeza.
Katika kujibu matokeo yetu, mwanasheria wa kimataifa wa uhalifu na haki za binadamu,Sara Elizabeth Dill, alisema: "Tunachokiona kimsingi ni kuzingirwa kwa vita na uharibifu kamili wa Gaza, bila kujali maisha ya binadamu au utu wa binadamu, au majaribio yoyote ya kufuata sheria za kimataifa."
Ripoti ya ziada na Erwan Rivault, Joshua Cheetham, Benedict Garman na Deena Easa
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi