Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani na China zaahidi kuimarisha uhusiano wao baada ya mazungumzo
Marekani na China zimeahidi kuimarisha uhusiano wao ambao umekuwa na mvutano kufuatia ziara ya siku mbili ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mjini Beijing.
Bw Blinken alikutana na Rais Xi Jinping wa China kwa mazungumzo siku ya Jumatatu, na kuanzisha upya mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya mataifa hayo yenye nguvu.
Bw Xi alisema wamepiga hatua, huku Bw Blinken akidokeza kuwa pande zote mbili ziko tayari kwa mazungumzo zaidi.
Lakini mwanadiplomasia wa juu wa Marekani aliweka wazi kuwa bado kuna tofauti kubwa.
"Nilisisitiza kwamba... mawasiliano endelevu katika ngazi za juu ndiyo njia bora ya kudhibiti tofauti kwa uwajibikaji na kuhakikisha kwamba ushindani hauingii kwenye migogoro," Bw Blinken aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo wa dakika 35 katika Ukumbi Mkuu wa Watu wa Tiananmen Square.
"Nilisikia vivyo hivyo kutoka kwa wenzangu wa China," alisema.
"Sote wawili tunakubali hitaji la kuimarisha uhusiano wetu."
Lakini Bw Blinken, 61, alisema yuko "macho wazi" juu ya China na kulikuwa na "maswala mengi ambayo hatukubaliani nayo kabisa kabisa".
Uhusiano kati ya Beijing na Washington umedorora kutokana na vita vya kibiashara vya enzi ya Trump, madai ya Beijing dhidi ya Taiwan na kutunguliwa kwa puto linalodaiwa kuwa la kijasusi la China juu ya Marekani mapema mwaka huu.
Lakini baada ya ziara ya Bw Blinken - ya kwanza kwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani nchini China katika takriban miaka mitano - Bw Xi alisema kuwa uhusiano unaweza kuwa na mwelekeo mzuri.
"Pande hizo mbili pia zimepiga hatua na kufikia makubaliano juu ya baadhi ya masuala maalum," alisema, katika nakala ya hotuba yake iliyotolewa na idara ya serikali ya Marekani. "Hivi ni vizuri sana."
Mkutano na Bw Xi haukuwa kwenye ratiba ya Bw Blinken na ulitangazwa saa moja tu kabla ya kufanyika.
Kama haungefanyika, wengi wangechukulia kama upuuzi hasa tangu mwanzilishi mwenza wa Microsoft Bill Gates kukutana na Bw Xi huko Beijing mapema wiki hii.
Badala yake, Wamarekani wataweza kuashiria ziara ya katibu huyo - ambayo pia ilijumuisha mikutano na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi na Waziri wa Mambo ya Nje Qin Gang - kama mafanikio ya ushirikiano na serikali ya China baada ya miezi ya mahusiano yaliyozorota.
Bw Xi pia alikuwa akituma ujumbe kwa watu wake kwamba serikali yake ilikuwa inafanya mazungumzo na Marekani.
Alimwambia mgeni wake kwamba jumuiya ya kimataifa ilikuwa na wasiwasi kuhusu mahusiano ya China-Marekani, ambayo yangekuwa muhimu kwa "hatma ya baadaye ya wanadamu".
Bw Blinken alikubali ni "muhimu kabisa" kwamba nchi hizo mbili ziendelee kuwasiliana.
"Hili ni jambo ambalo tutaendelea kulifanyia kazi," alisema.
Rais wa Marekani Joe Biden na maafisa wa Washington wamesema wanawaona Wachina kama washindani na sio wapinzani.
Ni tofauti ndogo sana iliyopo, hata hivyo, mashindano yanapopamba moto – ya kijeshi na kiuchumi.
Taiwan ndio eneo kubwa la mzozo kati ya nchi hizo mbili na ambalo lina uwezo wa juu zaidi wa kuongezeka.
Bw Wang alisema ni suala ambalo "hakuna fursa ya kulijadili na kuafikiana", huku Bw. Gang akilitaja kuwa "suala muhimu zaidi katika uhusiano wa China na Marekani na lenye uwezo wa kuwa hatari zaidi".
China inaiona Taiwan inayojitawala kama jimbo lililojitenga na Bw Xi amedokeza kwamba anataka kuiweka Taiwan chini ya udhibiti wa Beijing katika kipindi chake cha uongozi - ikiwa ni lazima, kwa nguvu.
Hata hivyo, Taiwan inajiona kuwa tofauti na bara la China na katiba yake na viongozi.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema mwaka jana kwamba Marekani itailinda Taiwan endapo kutatokea shambulizi kutoka China, hatua iliyoshtumiwa na Beijing.
Lakini Marekani pia imesisitiza sera yake ya China Moja, ikimaanisha kuwa kuna serikali moja tu ya China.
"Sera hiyo haijabadilika," Bw Blinken alisema Jumatatu. "Hatuungi mkono uhuru wa Taiwan."