Hii ndiyo mashine ya ATM ya juu zaidi duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Huenda ikawa imewekwa kwenye sehemu isiyowezekana kuwekwa mashine ya pesa, lakini ATM ya Khunjerab Pass imekuwa ikihudumia idadi ndogo ya wakaazi na wafanyikazi wa mpakani - na watalii wajasiri - tangu 2016.
"Tunaenda mwisho wa Pakistan," niliwaeleza watoto wangu.
"Tutapanda juu au chini?" waliuliza, wakionyesha ufahamu mkubwa wa kijiografia.
"Juu," nilijibu, "Juu."
Tulikuwa tunaelekea kwenye mashine ya pesa ya urefu wa juu zaidi duniani, iliyoko kwenye mpaka wa Khunjerab Pass kati ya China na Pakistan katika mkoa wa kaskazini mwa Pakistan wa Gilgit-Baltistan. Nilitaka kuwaonyesha watoto wangu mandhari ya kuvutia ambayo nchi yetu inayo.
Katika mwinuko wa ajabu wa mita 4,693, Khunjerab Pass ni kivuko cha juu zaidi cha lami duniani, na ni mojawapo ya njia za kushangaza zaidi duniani.
Mlima wa Karakoram uliofunikwa na theluji huweka uzio katika maeneo ya pembezoni, na Mbuga ya Kitaifa ya Khunjerab - nyumbani kwa chui wa theluji na alama za alama, mnyama wa kitaifa wa Pakistani - hutawanyika hadi jicho linavyoweza kuona.
Kwa nini ATM hii inayofanya kazi kikamilifu kujengwa katikati ya barafu milimani?

Chanzo cha picha, Aysha Imtiaz
Mashine hii inayoshikilia Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa mashine iliyojengwa juu zaidi duniani, inafanya kazi kama nyingine yoyote; inaweza kutumika kutoa pesa taslimu, kulipa bili za matumizi na kufanya uhamisho wa fedha baina ya benki.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini mimi na watoto, kilichotuvutia zaidi ni sherehe isiyotarajiwa kieleni mwa mlima wene thaluji, watu wengi walionekana kufurahia na kuizunguka ATM hii ili kupata picha bora zaidi (Selfie).
Mwalimu wa shule ya Karachi Atiya Saeed alikuwa ameleta wanafunzi wake 39 wa shule ya sekondari - wote wasichana - hapa kwenye mpaka wa Pakistan na China.
"Ni mara ya kwanza baada ya muda mrefu kwamba tumesafiri nchini Pakistan," alisema.
Ingawa hawakuja kutazama ATM hii peke yake, ziara yao ya mpakani ilikuwa, ni kuhusu somo la jiografia, historia na uchumi, hakika walikuwa wanajifunza katika mazingira yenye kupendeza zaidi.
ATM hii ilijengwa na Benki ya Kitaifa ya Pakistani (NBP) mnamo mwaka 2016, mashine inayotumia nishati ya jua na upepo ikihudumia idadi ndogo ya wakaazi na wafanyakazi katika kivuko hiki cha mpaka - na wasafiri wengine wajasiri wakiwemo watalii, ambao humiminika kupiga pichaw, huku wakitoa na kuweka fedha na kulta maana mpya kwa maneno "pesa ya baridi".
"Akaunti yangu imeganda!" alitania mtalii mmoja, mwalimu mkuu mstaafu wa Afrika Kusini Ayesha Bayat, ambaye alikuwa likizoni na mumewe. "Tumetoka katika nchi ambayo tuna safu za milima… lakini si kama hii. Ninapata kuona mandhari nzuri kabisa," alisema.
Lakini kujenga mashine hii halikuwa jambo dogo, kuliko hata kuitunza kwake. Mradi huo ulichukua takriban miezi minne, alisema afisa wa ufuatiliaji wa ATM wa benki ya NBP Shah Bibi.
Benki ya NBP iliyo karibu kabisa na eneo hili iko umbali wa kilomita 87 huko Sost, na meneja wa tawi la Sost, Zahid Hussain husafiri mara kwa mara kwenda na kurudi, akivumilia hali mbaya ya hewa, njia ngumu za milimani na maporomoko ya ardhi mara kwa mara ili kuiwekea pesa ATM hii.
"Kwa wastani, takriban rupia milioni 4 hadi 5 sawa na dola kati ya 17,646–£22,060$] hutolewa ndani ya muda wa siku 15," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bibi anasema husimami na kutoa taarifa kwenye tawi la Sost. Anapaswa pia kushughulika na dharura zinazohusiana na muunganisho wa satelaiti, nishati ya jua ya ATMA, uondoaji wa pesa taslimu na kadi zilizokwama na anasema mwaka jana, upepo mkali ulisababisha wakafunga kwa muda ATM.
"Inachukua takriban saa mbili hadi mbili na nusu kwa mtu kutoka chini mpaka kuifikia ATM na kufanya matengenezo," Bibi alielezea.
Hakika, wengine wanahoji matumizi ya ATM katika eneo hili ambalo ni mbali, shida kufikika na lililo juu milimani.
"[Lakini] mara nyingi tunasahau watu wanaolinda mipaka yetu masaa 24," Hussain alisema. "Wanaweza kuwa wachache kwa idadi, lakini mara nyingi wanaishi katika kama jangwani [na] hawana njia nyingine ya kuwatumia wapendwa na familia, pesa za mishahara yao."
Walinzi sio wafanyikazi pekee hapa. Bakhtawar Hussain ametumia muda mwingi wa maisha yake katika eneo hili, akiwafuatilia chui wa theluji au kusaidia wanasayansi na watafiti kupima kuyeyuka kwa barafu. Aliendesha mgahawa mdogo karibu na ATM hii hadi pale Covid ilipoingia akafunga. "Niliuza chai, kahawa na biryani ... nyakati zilikuwa nzuri," alikumbuka.

Chanzo cha picha, Aysha Imtiaz
Sasa anaendesha bafu linalotembea katika eneo hilo Khunjerab Pass kwa malipo kidogo, na ameweka gari lake tanki maalumu la oksijeni ili kutoa huduma ya kwanza bila malipo kwa wageni wanaopata shida ya oksijeni wawapo eneo hilo la juu mlimani.
"Katika saa chache zilizopita pekee, nimewapa wanawake watatu oksijeni. Jana, walikuwa saba," Bakhtawar aliniambia.
Pia ameeleza wasiwasi wake mkubwa kwa watalii ni kupata kadi zao zinazokwama, ingawa alikadiria kuwa huenda hutokea mara kwa mara - au mara chache - kama zilivyo kwenye ATM nyingine yoyote zilizozoeleka. Bado, hapa inahitaji muda wa kusubiri wa angalau saa mbili ukiwa katika hali mbaya ya hewa - au kurudi tena siku inayofuata.
"Sio safari rahisi kuipata," Bakhtawar alisema kwa tabasamu.















