Taiwan:Meli mbili za kivita za Marekani zapita karibu na lango la Bahari ya Taiwan

Chanzo cha picha, US 7TH FLEET
Meli mbili za kivita za Marekani zimepitia kwenye Mlango-Bahari wa Taiwan, Jeshi la Wanamaji la Marekani limetangaza.
Ni operesheni ya kwanza ya aina hiyo kufanyika tangu mvutano kati ya Taiwan na China kuongezeka kufuatia ziara ya Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi nchini Taiwan mapema mwezi huu.
Marekani na majeshi ya wanamaji wengine wa nchi za Magharibi wamekuwa wakisafiri mara kwa mara kupitia bahari hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Uchina ilijibu ziara ya Bi Pelosi kwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika eneo hilo.
Siku ya Jumapili, wizara ya ulinzi ya Taiwan ilisema iligundua ndege 23 za China na meli nane za China zikifanya kazi karibu na Taiwan.
Miongoni mwa ndege zilizogunduliwa, saba zilivuka mstari wa kati wa Taiwan Strait - kizuizi kisicho rasmi kati ya Taiwan na Uchina.
Washington inasema meli zake mbili za makombora - USS Antietam na USS Chancellorsville - zinaonyesha uhuru wa kupitia katika maji ya kimataifa.
Beijing inaona vitendo hivyo kuwa vya uchochezi na inashikilia kuwa kisiwa cha Taiwan ni sehemu muhimu ya eneo la China.
Siku ya Jumapili, jeshi lake lilisema linafuatilia shughuli za meli hizo mbili, likiwa na tahadhari kubwa, na liko tayari kupambana na uchochezi wowote, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jeshi la Wanamaji la Marekani lilisema katika taarifa kwamba usafiri kupitia Mlango-Bahari wa Taiwan ulionyesha "kujitolea kwa Marekani kwa eneo la Indo-Pacific huru na wazi".
"Meli hizi zilipitia kwenye korido katika mlango wa bahari ambao uko nje ya bahari ya eneo lolote la pwani," taarifa hiyo iliongeza.
Wizara ya ulinzi ya Taiwan ilisema meli hizo zilikuwa zikielekea kusini na kwamba vikosi vyake vinatazama, lakini "hali ilikuwa ya kawaida".
Taiwan inajitawala, lakini China inaiona kama jimbo lililojitenga na ambalo hatimaye itaungana, kwa nguvu ikiwa ni lazima.
Taiwan imekuwa kivutio kingine kati ya Washington na Beijing katika miaka ya hivi karibuni, huku Marekani ikijipata katika hali tete ya kidiplomasia kuhusu kisiwa hicho.
Marekani inatii sera ya "China Moja" - msingi wa uhusiano wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili ambayo inatambua serikali moja tu ya China - na ina uhusiano rasmi na Beijing na sio Taiwan.
Lakini pia inadumisha uhusiano "usio rasmi" na kisiwa hicho. Hiyo ni pamoja na kuuza silaha kwa ajili ya Taiwan kujilinda.















