Fahamu majiji manne yanayooachana na magari na kuhamia kwenye baiskeli na miguu

Wakati wimbi la kwanza la Covid lilizuia mikusanyiko ya ndani katika nchi nyingi ulimwenguni, miji mingi ilifikiria haraka kuhusu maisha yanavyoweza kuwa.

Baadhi walianzisha barabara za watembea kwa miguu pekee, wakageuza maeneo ya kuegesha magari kuwa migahawa na kuongeza njia zaidi za baiskeli - kubadilisha maeneo ambayo yalikuwa yakitumika na magari kuwa maeneo yanayofaa kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.

Mabadiliko hayo yalileta faida, sio tu katika kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, lakini tafiti pia zilionyesha virusi havisambai sana na kwa haraka katika vitongoji ambavyo watu wake wanatembea zaidi.

Na ingawa maeneo mengi sasa yamerudisha nyuma mipango hii maisha yanaporejea katika hali mpya ya kawaida, baadhi ya miji imeendelea kushikilia mipango ya watembea kwa miguu na imekuwa ikishinikiza kutengwa kwa nafasi nyingi zaidi zisizotumia magari.

Tunaangazia miji minne ulimwenguni ambayo ilifanya baadhi ya mabadiliko ya ujasiri na ya haraka sana ya watembea kwa miguu wakati wa janga hili - na iliweka mipango na juhudi nyingi kati ya hizo ili kuhimiza wakaazi na wageni kutembea kwa miguu.

Paris, Ufaransa

Hata kabla ya janga hilo, Paris ilikuwa na mazingira rafiki zaidi kwa watembea kwa miguu. Kama sehemu ya juhudi za jiji hilo la kupunguza idadi ya magari, vituo vya chini kando ya mto Seine vilitumiwa zaidi kwa miguu mwishoni mwa 2016, hatua ambayo ilifanywa kuwa ya kudumu mnamo 2018.

Mnamo 2020, Meya Anne Hidalgo alichaguliwa tena kushika wadhifa huo kutokana na kile kinachoitwa "mji wa dakika 15": dhana mpya ya kupanga mji ambayo inaruhusu wakazi kufanya kazi zao zote za kila siku - kuanzia manunuzi, shule hadi kazini - ndani ya dakika 15 kwa kutembea tu kwa miguu au kwa baiskeli.

"Nimeishi Paris kwa miaka 14, na ninaweza kusema kwa ujasiri kwamba sijawahi kuona mageuzi makubwa zaidi ya jiji zima kuliko yale ambayo yametokea hivi majuzi ili kuwatia moyo waendesha baiskeli," alisema Sadie Sumner, ambaye anaendesha tawi la Paris la kampuni ya waendesha baiskeli ya Fat Tire Tours.

Bogotá, Colombia

Wakati mji wa Bogotá na Colombia kwa ujumla imekuwa na utamaduni dhabiti wa baiskeli, na baiskeli pia ni kama mchezo wa kitaifa wa nchi hiyo. Janga Covid_19 liliharakisha mabadiliko mengi ya kupunguza matumizi ya magari.

Mnamo mwaka wa 2020, Meya Claudia Lopez aliiongeza njia za ziada za kilomita 84 kwa ajili ya baiskeli za muda katika mtandao wa kuliomita 550 uliopo katika jiji la Ciclorruta.

Mtandao huo wa barabara za Baiskeli ni moja mitandao mikubwa zaidi ulimwenguni - na tangu wakati huo zimekuwa njia za kudumu. Bogotá ilikuwa kati ya miji ya kwanza ulimwenguni kuongeza njia za miguu wakati wa janga hilo, na wakaazi wamegundua mabadiliko hayo ya kudumu yamekuwa bora.

Milan, Italia

Italia ilikuwa moja ya nchi zilizoathiriwa zaidi na janga la Covid_19, na miji yake ililazimika kuzoea haraka kutafuta njia mbadala za usafiri wa umma unaoweza kutumika na watu wengi.

Katika msimu wa joto wa 2020, Milan ilianza mpango kabambe wa kupanua barabara na kupanua njia za baiskeli kando, jumla ya kilomita 35 za barabara ambazo hapo awali ziikuwa na msongamano wa magari.

Mabadiliko hayo yamebadilisha jiji. "Siyo Milan ninayokumbuka miaka 10 iliyopita wakati wa siku zangu za chuo," alisema mkazi Luisa Favaretto, mwanzilishi wa tovuti ya Strategistico inayoishi nje ya nchi.

"Ninapenda wazo la jiji la dakika 15 [mpango ambao Milan pia anaufuatilia] na nilivutiwa na muundo msingi wa jiji ambao unatanguliza watu kwanza dhidi ya magari."

Ameona ukuaji katika kile anachokiita "ulimwengu wa kale" wenye hisia ya jumuiya, kwani kuna sababu zaidi za kutoka nje, kutembea na kukutana na jamii.

San Francisco, Marekani

Jiji hili la kaskazini mwa California lilichukua hatua ya haraka wakati wa janga la kwanza la Covid_19, kwa kuzindua kile kinachoitwa 'Mitaa ya Polepole - mpango ambao ulitumia alama na vizuizi kupunguza mwendo na misongamano ya magari na kasi kwenye njia karibu 30 katika juhudi za kuzifanya ziwe rafiki zaidi kwa watembea kwa miguu na baiskeli.

Kwa mujibu wa data zilizokusanywa na jiji, programu hiyo ilishuhudia kupungua kwa kasi na misongamano ya magari kwa 50% , ongezeko la 17% la watembea kwa miguu na ongezeko la 65% la waendesha baiskeli.