Haiti: Bunduki kutoka Marekani zafurika Port-au-Prince na kuchochea ongezeko la ghasia

Zaidi ya wiki mbili baada ya waziri mkuu wa Haiti kujiuzulu, kufuatia kuongezeka kwa ghasia huko Port-au-Prince, maelezo ya baraza la mpito la rais bado hayajafichuliwa.

Mojawapo ya changamoto ambazo baraza hili italazimika kukabiliana nazo ni biashara haramu ya bunduki, ambayo imeyapa nguvu magenge ambayo yameteka mji mkuu.

Kuongezeka kwa ghasia kumesababisha watu kuhama mji mkuu.

Miongoni mwa wanaoondoka ni David Charles mwenye umri wa miaka 14 ambaye baba yake Israel ana wasiwasi anaposubiri basi la mwanawe kuwasili Cap-Haitien.

Kisha basi hilo linawasili na kusimama kando ya barabara. Anatabasamu kwa matumaini. Mwanawe David mwenye umri wa miaka 14 anashuka ngazi akiwa na mizigo yake. Wanakumbatiana kwa nguvu.

David amefanikiwa kutoroka Port-au-Prince, mji ambao sasa umesambaratishwa na magenge yenye silaha na machafuko ya kisiasa. Ghasia nyingi zinazoikumba Haiti zimejikita katika mji mkuu: Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa asilimia 80 ya mji sasa inadhibitiwa na magenge.

Alikuwa ameishi huko kwa miaka miwili bila wazazi wake, ili kumaliza elimu yake, lakini Israel hakutaka "awe mwathirika".

Machafuko ya mwezi huu yalimchochea kumtoa mwanawe hadi Cap-Haitien, jiji lililo kaskazini mwa nchi ambalo ni salama zaidi.

"Safari ilikuwa ndefu sana, zaidi ya saa sita. Nilikuwa nikiomba njia nzima," anasema David. "Dereva wa basi baadaye alituambia kulikuwa na milio mingi ya risasi katika eneo moja, basi letu lilinusurika."

Abiria wengine kwenye basi wanaonekana wamechoka, wamefarijika lakini pia wamekasirika. Mwanaume mmoja aliyevalia fulana nyeusi na miwani ya jua anaongea kwa utulivu huku tukimuuliza hali yake. Lakini anaonekana kuwa na hasira anapotuambia ana ujumbe kwa Marekani.

"Bunduki zote hapa zinatoka Marekani, kila mtu anajua. Ikiwa Marekani inataka kukomesha hili, wanaweza kuifanya kwa urahisi!" Anasihi: "Tunaiomba Marekani itupe nafasi ya kuishi, itupe nafasi tu."

Kwa nchi ambayo haitengenezi silaha, ripoti ya Umoja wa Mataifa mnamo Januari iligundua kuwa kila aina ya bunduki ilikuwa ikifurika Port-au-Prince: bunduki zenye nguvu nyingi kama vile AK-47.

Silaha hizo zinachochea kuongezeka kwa kasi ghasia zinazohusiana na magenge ya Haiti.

Hakuna idadi kamili kuwa ni silaha ngapi zinazouzwa Haiti kwa sasa.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema baadhi ya makadirio yanaiweka kuwa nusu milioni ya silaha halali na haramu kufikia 2020.

Iliripoti kuwa bunduki na risasi zilikuwa zikiingizwa kinyemela kutoka nchi kavu, angani na baharini kutoka majimbo ya Marekani kama vile Florida, Texas na Georgia.

Kumekuwa na visa vya kukamatwa silaha katika bandari kuu za nchi huko Port-au-Prince, Port-de-Paix na Cap-Haitien. Silaha haramu zimefichwa kwenye vyombo vya usafirishaji kati ya vinyago na nguo.

Mnamo Julai 2022, mamlaka ya Haiti ilikamata silaha nyingi na risasi 15,000. Zilikutwa kwenye shehena kutoka Florida kuelekea kanisa la Episcopal huko Haiti.

Umoja wa Mataifa pia ulibainisha matumizi ya viwanja kadhaa vya ndege vya siri vilivyojengwa kwa madhumuni ya kibinadamu baada ya tetemeko la ardhi lililoharibu mwaka 2010, ambavyo sasa havifuatiliwi.

Mapema mwezi huu, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, aliwaambia waandishi wa habari kuwa ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa magenge nchini Haiti ni "kunyamazisha bunduki".

Katika kona ya ofisi yake, mwendesha mashtaka mkuu wa Cap-Haitien, Charles-Edward Durant, anaweka bunduki ya otomatiki.

Anasema anahitaji usalama kila anaposafiri. Kwake, mambo hayajawahi kuwa mabaya sana huko Haiti. "Hii ni ndoto mbaya, ni ndoto ya kutisha. Ningependa raia wa Haiti waamke na kufanya kazi ili kuwa na nchi bora."

Marekani inasema inaweka uzito wake katika tatizo la bunduki na magenge, pia.

Mwaka jana, Wizara ya Mambo ya Nje ilionesha kuwa ina mipango ya kusaidia kuanzisha kitengo kipya cha polisi nchini Haiti kushughulikia silaha zinazosafirishwa nchini humo.

Hata hivyo, bila mkuu wa nchi, na serikali, watu wa Haiti wamenaswa katika mzunguko mwingine mbaya wa vurugu unaoendeshwa na bunduki haramu.

Mmoja wao ni Juliette Dorson. Mwnamke huyo mwenye umri wa miaka 50 alitoroka Port-au-Prince baada ya kunusurika kupigwa risasi.

Mpangaji huyo wa karamu bado ana makovu ya risasi zilizompata alipoviziwa kwenye hafla aliyokuwa akiihudumia.

"Nilisema kimbia, kimbia, kimbia kwa sababu wanapiga risasi. Wakati huo, nilipigwa risasi mbili: moja kwenye miguu yangu na nyingine kwenye mkono."

Watu kumi waliuawa, akiwemo mshirika wake wa biashara mwenye umri wa miaka 22, Luc.

Analia huku akiongea juu yake. Kumbukumbu ya yote ni kiwewe sana kuweza kuizungumzia kwa kirefu.

Juliette anatuonyesha nafasi ndogo anayoishi kwa sasa, akitumia kitanda kimoja na rafiki.

Ni ulimwengu ulio mbali na nyumba aliyokuwa akimiliki katika mji mkuu. Magenge yamichukua. Hawezi kurudi.

"Wakati magenge na ghasia zilipoanza huko Port-au-Prince, serikali haikufanya lolote kukomesha. Na waliacha hili likue na kukua. Sasa ni jambo gumu mno kukomesha."