Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Euro 2024: Ni wachezaji gani ambao mashabiki wa Ligi Kuu ya Uingereza wanataka wasajiliwe?
Mojawapo ya jambo kubwa katika soka la kimataifa; mchezaji anayefanya vyema kwenye mashindano makubwa anakuwa na uwezekano wa kusonga mbele zaidi.
Mfikirie Enzo Fernandez baada ya kombe la dunia la Qatar 2022. Jack Grealish baada ya Euro 2020. Au mfano bora kabisa - Karel Poborsky baada ya Euro '96.
Kwa hivyo ni nani anapaswa kusajiliwa kutoka mashindano ya Euro ya msimu huu huko Ujerumani?
Tuliwauliza mashabiki wa vilabu vya Ligi Kuu ya Uingereza, kutoa mapendekezo yao.
Nico Williams (Athletic Bilbao)
Mshambuliaji wa Athletic Bilbao mwenye umri wa miaka 21, amecheza zaidi ya mechi 120 dhidi ya klabu kubwa, winga huyo amefanya vyema kwenye michuano ya Euro 2024.
Alifunga bao zuri dhidi ya Georgia, na kudhihirisha kipaji chake. Anaweza kuwa mmoja wa wachezaji wa Ulaya wanaohitajika sana baada ya michuano hiyo.
Sean, shabiki wa Liverpool: Nico Williams anafaa kucheza mbele chini ya kocha Arne Slot. Ana kasi, mwepesi, analiona goli na ana ujasiri wa ujana. Mohamed Salah anaweza kuondoka kwenye timu hii mwaka ujao na tunahitaji kujipanga kwa hilo.
Robert, shabiki wa Manchester United: Nico Williams kwa kushirikiana na mawinga wetu wa sasa anaweza kutufaa na anaweza kucheza pande zote mbili. Yeye upande wa kulia na Alejandro Garnacho upande wa kushoto, itakuwa safi kabisa.
Ben, shabiki wa Tottenham: Nico Williams ni kijana na ana kipaji, mwepesi sana na ni fundi. Anafaa kwa mfumo wa uchezeshaji wa kocha Ange Postecoglou.
Christoph Baumgartner (RB Leipzig)
Mchezaji wa timu wa Austria chini ya kocha Ralf Rangnick. Ni mchezaji wa klabu ya RB Leipzig. Christoph Baumgartner ni kiungo mkabaji mwenye umri wa miaka 24, mwenye jicho la kulenga lango.
Alishinda dhidi ya Poland na kutengeneza bao la ushindi la Marcel Sabitzer dhidi ya Uholanzi katika mchezo wa mwisho wa kundi na kuisaidia Austria kuingia Kundi C juu ya Ufaransa.
Tomos, shabiki wa Aston Villa: Ningependa Villa wamsajili Baumgartner. Anaonekana ni mchezaji mzuri lakini pia ni mtukutu katika mtindo na ustadi wake. Mleteni katika uwanja wa Unai Emery.
Andrew, shabiki wa Brighton: Anavutiwa na Baumgartner. Anaamini ni mshambuliaji anaefaa kuwepo Brighton.
Stanis, shabiki wa Crystal Palace: Chini ya kocha Oliver Glasner, tunahitaji mshambuliaji wa Austria anaecheza soka katika ligi ya Bundesliga ya Ujerumani, hasa Baumgartner.
Riccardo Calafiori (Bologna)
Italia daima imekuwa ikizalisha walinzi wazuri, Calafiori mwenye umri wa miaka 22, anaweza kuwa mlinzi mwingine bora. Anafanana na gwiji wa miaka ya 2000 Alessandro Nesta.
Calafiori alitajwa katika kikosi cha kocha mkuu Luciano Spalletti kilichoshiriki Euro 2024, Calafiori alikuwa muhimu sana. Alikosa mechi ya hatua ya 16 bora dhidi ya Sweden na Italia ikatolewa.
Leon, shabiki wa Arsenal: Calafiori anaweza kuleta usaidizi mzuri kwa Gabriel ikiwa atasajiliwa.
Josh, Chelsea: Calafiori ni chaguo bora. Bado ni mchanga lakini tayari ana uzoefu wa kutosha na anaweza kuimarisha safu yetu ya nyuma.
David, shabiki wa West Ham: Tunahitaji kumsajili Calafiori. Mchezaji wa kati ambaye anajua kucheza mpira na ana ustadi. Ni mzuri sana.
Georges Mikautadze (Metz)
Katika mshangao wa wengi wa ushindi wa Georgia dhidi ya Ureno, Mikautadze alifunga katika kila mechi kati ya mechi zao tatu za kundi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 pia alifanikiwa kufunga mabao 13 katika mechi 20 za Ligue 1 akiwa na klabu ya Metz msimu uliopita licha ya kushuka daraja.
Sonny, shabiki wa Ipswich Town: Mikautadze atakuwa usajili mzuri kutokana na jinsi anavyocheza vizuri. Ingawa yuko juu ya bajeti yetu, ila anafaa.
Mark, shabiki wa Leicester City: Bila shaka, ni Mikautadze. Ni mchezaji bora kutoka ligi ya chini ya Ufaransa, kama Riyad Mahrez.
Tom, shabiki wa Wolves: Nitataka Mikautadze asajiliwe. Mwepesi, kijana na anajua kutupia katika wavu. Amenivutia sana.
Giorgi Mamadashvili (Valencia)
Mchezaji mwingine wa timu ya Georgia, kipa Mamadashvili amekuwa bora nchini Ujerumani.
Ana umri wa miaka 23, alionyesha uwezo mkubwa katika mchezo wa pili wa kundi dhidi ya Jamhuri ya Czech, akiokoa mara 11 ili kujihakikishia pointi muhimu.
Jack, shabiki wa Newcastle United: Ikiwa tunatafuta kwa dhati namba moja mpya wa muda mrefu, Mamadashvili anatufaa.
Tom, shabiki wa Nottingham Forest: Dirisha zuri la uhamisho litajumuisha kusajili golikipa. Mamadashvili amenivutia sana kwa kuokoa vizuri na itakuwa bora tukimsajili.
Ethan, shabiki wa Southampton: Mamadashvili amekuwa kipa mzuri katika goli la Georgia, huku Gavin Bazunu akiwa nje kwa muda mrefu, anaweza kuwa golikipa anaetufaa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Abdalla Seif