Cheche za maneno kati ya Rais William Ruto na Raila zinaashiria nini?

    • Author, Abdallah Dzungu
    • Nafasi, BBC NEWS

Huku Wakenya wakiendelea na kukabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha duniani, hali iliyosababishwa na vita vya Ukraine na hali mbaya ya ukame , mzozo wa kisiasa umechipuka nchini humo, hali ambayo huenda ikaendeleza hali mbaya ya kimaisha na kuwa mzigo kwa Wakenya wengi iwapo haitaangaziwa kwa haraka kulingana na wachanganuzi wa kisiasa nchini humo.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2022 uliomuidinisha Rais William Ruto kuwa mshindi halali wa kiti cha Urais, kiongozi wa Upinzani Raila Odinga aliwasilisha pingamizi mahakamani akidai kwamba tume ya uchaguzi ilihusika katika kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo ili kumpendelea mpinzani wake William Ruto.

Hata hivyo mahakama ya juu iliidhinisha matokeo ya tume ya uchaguzi ya IEBC na kumpatia ushindi bwana William Ruto, uamuzi uliopingwa na Raila Odinga na upinzani.

Akizungumza saa chache baada ya kutoka ziarani Afrika Kusini, Raila Odinga aliyevurumiza moja kwa moja akiandamana na maelfu wa wafuasi wake hadi katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji jijini Nairobi , alisema kwamba ana ushahidi kwamba, tume ya Uchaguzi ya IEBC ilichakachua matokeo ya uchaguzi huo ili kumpa ushindi mpinzani wake William Ruto.

Raila alisema kwamba afisa wa IEBC aliyejitolea na ambaye hakumtaja alifanya uchunguzi uliobani kwamba alimshinda William Ruto kwa zaidi ya kura milioni mbili na sio kama ilivyotangazwa na tume ya IEBC iliompatia Ruto Ushindi.

Bw Odinga alitoa wito mara nane kwa Wakenya, akisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza ilikuwa madarakani kinyume cha sheria.

"Kwanza, sisi kama Azimio tunakataa matokeo ya uchaguzi wa 2022. Hatuwezi na hatutatambua utawala wa Kenya Kwanza na tunachukulia serikali ya Kenya Kwanza kuwa haramu," Bw Odinga alisema.

Bw Odinga alisema kwamba miundo msingi na rekodi zote za uchaguzi wa 2022 katika tume ya uchaguzi , IEBC ziwekwe hadharani na kukaguliwa na chombo kisichoegemea upande wowote -na kwamba ukaguzi wa kimahakama wa matokeo na seva za IEBC hauwezi kujadiliwa.

Alitoa Wito kwa kila Mkenya kupinga na kutaka kuondolewa kwa ushuru wa adhabu ambao umesababisha gharama za juu za bidhaa na huduma za kimsingi zikiwemo unga, maziwa, sukari, vitabu vya shule, mafuta, umeme, nauli, mafuta ya taa na karo za shule kupanda. ."

Lakini akizungumza muda mfupi baada ya tangazo hilo la bwana Raila Odinga , Rais William Ruto alisema kwamba , Kiongozi huyo wa Muungano wa azimio alikuwa akijaribu kuilazimisha serikali yake kuingia katika makubaliano fulani ili aweze kukimu mahitaji ya kifamilia.

Rais huyo aliapa kwamba hatukubali kudanganywa na akafutilia mbali mapatano na Bw Odinga kama ilivyokuwa mwaka 2018 ambapo kiongozi huyo alifanya makubaliano ya handshake na aliyekuwa rais wakati huo Uhuru Kenyatta kufuatia uchaguzi wa 2017 uliokumbwa na utata.

“Nataka kuwaambia wasahau handshake, na usituambie hutaki handshake. Tunakufahamu na tunaweza kukuona,’’ Dkt Ruto alisema alipohutubia waombolezaji kaunti ya Kiambu wakati wa ibada ya mazishi ya Pauline Nyokabi, dadake Waziri wa Biashara Moses Kuria.

Ruto: Sitatishika

Cheche hizo za maneno kati ya viongozi hao wawili zilivunja uhusiano mzuri wa muda mfupi kati ya viongozi hao wawili ambapo ulipelekea wandani wa Raila Odinga kumkaribisha rais Ruto wakati wa ziara yake huko Nyanza.

Akizungumzia kuhusu mikutano ya maandamano iliopangwa na Raila Odinga, rais Ruto alisema kwamba kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akipanga kutumia ufuasi wake wa kisiasa ili kujinufaisha mwenyewe, wandani wake na familia yake

“Hii maandamano yote wanafanya hawafanyi juu ya wananchi, wanafanya juu ya ubinafsi, familia zao na biashara zao, Ruto alinukuliwa akisema.

Kiongozi huyo wa nchi alitangaza kuwa yeye si mtu wa kutishwa na akaapa kuwa serikali yake itakabiliana na majaribio yoyote ya kuvuruga amani na kukosekana kwa utulivu.

Je Cheche hizi za maneno zinaashiria nini?

Miezi mitatu tu baada ya mahakama kuamua kuhusu uchaguzi wa Urais uliokumbwa na Utata, na Wakenya kuamua kuendelea na maisha yao ya kawaida hata baada ya tofauti iliokuwepo baina yao, ving'ora vya makabiliano ya kisiasa vimeanza kusikika.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa kisiasa makabiliano haya kati ya viongozi wawili walio na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini Kenya huenda yakachochea mapambano ya kisiasa kati ya wafuasi wao, kuligawanya taifa katika mirengo mbali mbali ya kisiasa na hivyo basi kuibua mjadala mwengine wa kisiasa kuhusu uongozi wa taifa hili ikiwa imesalia miaka minne kabla ya uchaguzi mwengine wa urais kufanyika.

Alutalala Mukhwana – Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Kenya

Kwa mujibu wa Alutalala Mukhwana mikutano inayoitwa na Raila Odinga kusudio lake ni kuchemsha hisia za wafuasi wake ili waone haki yao imenyakuliwa.

Bwana Alutalala anasema kwamba matokeo ya mikutano hiyo italeta hasira na uharibifu wa mali.

''Kwa upande wake Rais William Ruto ataamrisha vyombo vya ujasusi na usalama kukabiliana na mikutano hiyo'', alisema mchambuzi huyo.

Alutalala anaongezea kwamba nia yake Raila Odinga ni kuitwa na Ruto na kufanya handishake, licha ya kiongozi huyo wa upinzani kudai kwamba hataki Handshake

''Analozungumzia mwanasiasa sio analonuia'' alisema bwana Alutalala

''Kama kweli alitaka kurekebisha anayotaka kubadili mbona hakufanya hivyo wakati wa handishake na Uhuru''?

Mchambuzi mwengine wa masuala ya kisiasa nchini Kenya ambaye hakutaka kutajwa , amesema kauli ya Raila Odinga inatokana na matamshi ya Rais William Ruto kwamba baadhi ya viongozi katika serikali iliopita walikuwa na njama ya kumuua aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini IEBC Wafula Chebukati.

Mchambuzi huyo anasema kwamba hatua ya Raila ililenga kujibu matamshi hayo ya William Ruto na kwamba wito wa maandamano dhidi ya serikali hautafua dafu kwani Wakenya wengi hawangependa kujihusisha katika masuala ambayo yangezidi kuendeleza hali ngumu ya kiuchumi.

‘’Masuala ambayo Raila anawasilisha yamepitwa na wakati ,ila serikali itampatia ajenda iwapo watatumia gesi ya kutoa machozi katika mkutano wake wa siku ya Jumapili’’, alihitimisha..

Athari za maandamano ya kupinga serikali

Mwaka wa 2017 baada ya Kenya kushiriki katika uchaguzi uliokumbwa na utata na kupelekea mahakama ya juu kuufutilia mbali na kuitisha marudio ya uchaguzi huo , Kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliitisha maandamano ya kupinga kufanyika kwa marudio hayo akitoa masharti ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Miongoni mwa masharti yake Bwana Raila Odinga aliomba kufanyika kwa mabadiliko katika tume ya uchaguzi iliokosolewa pakubwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.

Vilevile kufutiliwa mbali kwa uchaguzi huo kulitarajiwa kutoa fursa ya kuimarisha demokrasia katika taifa ambalo kila uchaguzi ulikumbwa na mzozano.

Hatahivyo tume hiyo ilitangaza tarehe mpya ya uchaguzi bila kutilia maanani marekebisho hayo hatua iliomshinikiza kiongozi wa upinzani kususia uchaguzi huo wa marudio na badala yake kuitisha maandamano kote nchini siku ambayo uchaguzi huo ungefanyika.

Wito kama huo unajirudia baada ya uchaguzi wa 2022 ambapo tume hiyo inahitaji makamishna wapya baada ya muda wa kuhudumu wa makamishna watatu wakiongozwa na Wafula Chebukati kuisha huku wengine watatu wakijiuzulu kufuatia madai kwamba walikuwa na njama ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi kumpendelea Raila Odinga.

Tayari upinzani umeionya serikali dhidi ya kuwachagua makamishna hao kinyume cha sheria.

Hatahivyo Uchaguzi huo wa marudio wa 2017 ulifanyika kama ulivyopangwa baada ya serikali iliokuwepo kuimarisha usalama katika vituo vyote vya kupiga kura licha ya kususiwa na viongozi wa upinzani.

Na baada ya kumtangaza rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa marudio , Raila aliendeleza wito wake wa maandamano yalioshirikisha kususia bidhaa kadhaa nchini.

Maandamano hayo yaliosababisha vifo na vurugu miongoni mwa wafuasi wa bwana Odinga na wale wa Uhuru kenyatta, yalisimamisha biashara katikati ya jiji la Nairobi na kuathiri uchumi.

Baadhi ya biashara na makampuni yanayotoa huduma zao katikati ya mji zililazimika kufungwa huku wafanyakazi wengi wakipoteza kazi zao hali ilioyoathiri uchumi kwa kiwango kikubwa.

Hali hiyo ya kutisha iliwafukuza wawekezaji na kuathiri sekta ya utalii kwa muda mrefu.

Mazingira mabaya kama hayo yaliripotiwa wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo maelfu ya Wakenya walipoteza maisha yao, uchumi kuathirika na gharama ya maisha kupanda huku wawekezaji na watalii wakiondoka na kuelekea katika mataifa yanayowavutia zaidi.

Shinikizo hizo za baada ya uchaguzi wa 2017 hatahivyo zilizaa matunda mwishoni baada ya aliyekuwa rais Uhuru kenyatta kuonana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika kile kilichotajwa kuwa 'handshake'.

Mkutano kati ya viongozi hao wawili hatimaye ulishuhudia amani nchini na maridhiano ya kisiasa.

Na huku Wakenya wakiendelea kuyumbishwa katika wimbi la kisiasa kati ya viongozi hawa, swali ni je ni nani atakayepigania gharama ya juu ya maisha, haki zao za kimsingi na ukosefu wa ajira.

Je mgogoro huu wa kisiasa ni muendelezo wa matatizo yanayowakumba kwa sasa?