Uchaguzi wa Angola: Chama tawala MPLA kwa muda mrefu chakabiliwa na upinzani kubwa kutoka Unita

Kampeni za uchaguzi Angola 2022

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wafuasi wa Unita wanatumai kuwa wakati huu chama chao kinaweza kuing’oa kile cha MPLA, ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo minne

Uchaguzi wa Angola siku ya Jumatano unatarajiwa kuwa wenye ushindi mkali zaidi tangu uhuru mwaka 1975.

Huku chama cha MPLA kikiongoza kwa zaidi ya miongo minne, inaweza kuwa vigumu kufikiria kwamba kinaweza kupoteza nafasi yake katika kilele cha mamlaka.

Lakini kinakabiliwa na wimbi linaloongezeka la kutoridhika kunakochochewa na viwango vya juu vya umaskini na ukosefu wa ajira.

Licha ya Angola kuwa na utajiri wa mafuta na madini, wengi hawajafaidika na utajiri huo.

Na ingawa miaka 20 ya amani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu kumekaribishwa, hakujaleta mafanikio ambayo wengi walitarajia.

Kuna vyama vinane vinavyoshiriki, lakini mpinzani mkuu wa MPLA ni Unita - vuguvugu ambalo wakati fulani lilikuwa kundi la waasi.

Unita inatafuta kufaidika na ukosefu wa furaha huku takriban wapiga kura milioni 15 waliojiandikisha wakichagua rais wao na wabunge kwa miaka mitano ijayo.

Idadi kubwa ya wapinzani dhid ya MPLA inaweza kuvunja kura ya upinzani, lakini wakati huu Unita imeunda muungano usio rasmi na mashirika ya kiraia na wanaharakati ili kupanua ushawishi wake.

Wapiga kura watapiga kura moja na kiongozi wa chama mwenye kura nyingi ndiye atakuwa rais.

Mji mkuu, Luanda, umepambwa kwa propaganda za chama.

Mabango makubwa yenye sura za wagombea urais yametapakaa katika jiji hilo, ambapo siku za kampeni mitaa imetanda muziki katika kujaribu kuwavuta wapiga kura.

Nyekundu, nyeusi na njano ya MPLA inatawala na kauli mbiu yake ‘’nguvu ya watu’’.

Rangi nyekundu na kijani za Unita pia zinaweza kuonekana katika baadhi ya maeneo ya jiji na mabango yanayotangaza kwamba ‘’wakati ni sasa’’.

Wagombea wakuu wawili wa urais ni:

  • Kiongozi wa MPLA João Lourenço - mwenye umri wa miaka 68 ambaye anawania muhula wa pili wa
  • Unita Adalberto Costa Júnior - hii ni mara ya kwanza kwa mzee huyo wa miaka 60 kuwania urais.

Katika mji mkuu, pia kuna uwepo mkubwa wa polisi wenye silaha na wanajeshi, ambako kunazidisha hisia za mvutano kabla ya uchaguzi ambao unaweza kuwa wa kihistoria.

Wanaounga mkono MPLA wanasema chama hicho kinasikiliza maswala ya mashinani

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wanaounga mkono MPLA wanasema chama hicho kinasikiliza maswala ya mashinani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi ya wachambuzi wanasema watu wanaanza kufikiria chama tofauti madarakani.

‘’Maoni ya jumla ni kwamba nchi iko tayari kwa mambo kubadilika,’’ mwanauchumi Âurea Mouzinho aliiambia BBC.

‘’Watu wamekomaa zaidi na hofu yao ni kidogo kwamba wanataka mambo yawe tofauti.’’

Mara ya mwisho mambo yalikuwa karibu hivi mwaka wa 1992 wakati rais wakati huo, José Eduardo Dos Santos, alipokabiliana na kiongozi wa kundi la waasi la Unita, Jonas Savimbi.

Mzozo juu ya matokeo ulisababisha kuanza tena kwa vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Lakini kuna tofauti wakati huu.

‘’Miaka thelathini baadaye, tunaweza kusema kwamba tuna wananchi ambao wako makini zaidi katika mchakato wa uchaguzi, kuchambua, kukosoa na kukemea vitendo wanavyoona si sahihi,’’ Cesaltina Abreu, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Angola alisema.

Lakini MPLA inasalia na imani kuwa bado inaweza kutoa msaada kwa Waangola.

‘’Tuna uhakika wa ushindi. Kufanya kazi mashinani na kuhamasisha watu, tunazungumza nao na tunapima kile wanachosema,’’ Arsénio Satyohamba, kiongozi wa vijana wa MPLA aliyesimama kama mbunge, aliiambia BBC.

Licha ya kuingia mamlakani 2017 kwa ahadi za kupambana na ufisadi ndani ya chama chake na serikali na vile vile kutoa nafasi za kazi 500,000 kwa vijana, muhula wa kwanza wa Bw Lourenço umekuwa na matatizo na kusababisha kupungua kwa umaarufu wake.

‘’Mwaka wa 2017 João Lourenço alileta mtazamo mpya kwa MPLA, licha ya kwamba Angola ilikuwa ikipitia mdororo wa kiuchumi kutokana na mambo mbalimbali. Ameweka baadhi ya programu za kuleta afueni katika uchumi wetu na leo hii tunaweza kuona hilo likifanyika,’’ Bw Satyohamba alisema.

‘’Kando na Covid-19 na changamoto zingine, Rais Lourenço ameweza kuboresha uchumi wetu,’’ akaongeza.

João Lourenço (kushoto) ambaye anawania muhula wa pili wa urais anakabiliwa na Adalberto Costa Júnio wa Unita.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, João Lourenço (kushoto) ambaye anawania muhula wa pili wa urais anakabiliwa na Adalberto Costa Júnio wa Unita.

Hata hivyo, hali ngumu ambazo watu wengi hukabili, ikiwa ni pamoja na ongezeko la njaa na umaskini uliokithiri, hazifanyi kila mtu awe na matumaini hivyo.

Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Angola ni karibu 30%, lakini miongoni mwa vijana idadi hiyo inafikia 60%, takwimu rasmi zinasema.

‘’Tulichoona tangu 2017 ni kuzorota kwa hali ya maisha kwa kila mtu,’’ mwanauchumi Bi Mouzinho alisema.

‘’Tunaona uchumi ambao unazidi kuwa mbaya zaidi katika suala la kile unaweza kutoa kwa watu.’’

Ukosefu wa baadhi ya mambo ya msingi kama vile upatikanaji wa maji safi, umeme, elimu na huduma za afya unawasumbua vijana wengi mijini na vijijini.

Na ndio walio wengi, huku umri wa wastani ukiwa chini ya miaka 16.

Mfuasi wa Unita Ana de Sousa, 22, hana shaka kwamba nchi inahitaji mabadiliko.

‘’Hatuna kazi, tunajaribu kuomba kazi katika zabuni za umma lakini hata hatuwezi kufanya hivyo,’’ aliambia BBC.

‘’Tuna watoto wengi wanaohitaji elimu na afya.’’

Ana de Sousa (kushoto) anatumai kunaweza kuwa na nafasi zaidi za kazi
Maelezo ya picha, Ana de Sousa (kushoto) anatumai kunaweza kuwa na nafasi zaidi za kazi

Mwanafunzi wa historia mwenye umri wa miaka 24 Lígio Katukuluka anataka sauti za vijana kuchukuliwa kwa uzito.

‘’Kuna haja ya kuwafanya vijana, ambao ni wengi barani Afrika, wahusika wakuu wa maamuzi ya serikali,’’ alisema.

‘’Ninahisi kwamba utamaduni na elimu vimekuwa maeneo yaliyotengwa sana. Nataka uwekezaji zaidi ufanywe katika kukuza utamaduni [wa Kiafrika].’’

‘’Nchi yetu imekuwa katika amani kwa miaka 20 sasa lakini matatizo mengi kama hayo yanaendelea,’’ mjasiriamali mdogo Cláudio Silva, 34, alisema.

‘’Unita inapata usaidizi mwingi [wa vijana] kwa sababu wanatoa suluhisho, wanatoa njia mbadala tofauti na ile tuliyoizoea tangu uhuru.’’

Licha ya imani kuwa huu unaweza kuwa uchaguzi wenyeushindani mkali, pia kuna wasiwasi kwamba unaweza kuibiwa, jambo ambalo linaongeza wasiwasi.

Vuguvugu linaloitwa ‘Vote and Sit Down’ limeteka fikira za baadhi ya watu.

Linatoa wito kwa watu wanaojitokeza kubaki karibu na kituo cha kupigia kura hadi mwisho wa mchakato wa kuhesabu kura ili ‘’kutetea kura zao’’.

Hata hivyo, mamlaka imesema watu wanapaswa kurudi nyumbani baada ya kupiga kura yao.