Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Kuna bomu linasubiri kulipuka Mashariki ya Kati" - gazeti la The Guardian
Tunaanza ziara yetu ya magazeti na gazeti la Uingereza, The Guardian, limechapisha makala ya Simon Tisdale kuhusu mvutano wa sasa Mashariki ya Kati na athari ya mauaji ya askari watatu wa Marekani na kujeruhiwa makumi katika kituo cha kijeshi cha Marekani huko Jordan.
"Kuna bomu kubwa linasubiri kulipuka Mashariki ya Kati, Biden hapaswi kuwasha fyuzi kwa kuishambulia Iran," mwandishi anasema shambulio la Oktoba 7 lililoanzishwa na Hamas dhidi ya Israeli liliwasha fyuzi inayowaka Mashariki ya Kati nzima, na bomu kubwa limeunganishwa na fyuzi hiyo, na Vita vya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran viko karibu kulipuka, na matokeo yake yatakuwa mabaya.
Mwandishi anasema: “Wakati mashambulizi mabaya ya kila siku ya Israel yanaendelea Gaza, na vifo vya Wapalestina ni maelfu, mlipuko mkubwa unazidi kukaribia. Na hatari inaongezeka kutoka Bahari ya Shamu hadi Iraq, Syria na Lebanon, ambapo kuna wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.
Mwandishi huyo anasema Iran inasisitiza haihusiki na shambulio la Jordan, lakini ni wachache jijini Washington wanaoamini madai hayo, kwa kuzingatia historia ndefu ya uungaji mkono na kutoa mafunzo na kuwapa silaha wanamgambo katika eneo hilo, katika kuendeleza sera iliyoanzishwa na Jenerali Qassem Soleimani, ambaye aliuawa na Marekani Januari 2020.
Mwandishi anaamini Iran, ambayo ina lengo la kuyatimua majeshi ya Marekani katika kambi zao za Iraq, Syria na Ghuba na hatimaye kukomesha uwepo wa Marekani katika eneo ambalo Iran inataka kulitawala. Shambulio la Oktoba 7 na jibu la Israel linaloungwa mkono na Marekani ni fursa ya Iran kutimiza lengo hilo.
Anasema, "bado haijabainika iwapo shambulio la Jordan lilikuwa ni la makusudi kwa upande wa Iran na mshirika wake, wanamgambo wa Iraq Islamic Resistance. Au lilikuwa shambulio la bahati nasibu ambalo lilifanikiwa."
Mwandishi anasema Marekani itajibu kwa namna moja kati ya hizi mbili: Ikiwa Marekani ina hakika shambulio hilo lilikuwa la kubahatisha tu, basi inawezakulipiza kisasi kwa kushambulia vituo vya wanamgambo ambao walifanya mashambulizi hayo. Lakini ikiwa itahitimisha kuwa shambulio hilo lilifanywa kwa makusudi, jibu la Marekani linaweza kujumuisha mali na maeneo ya Iran.
Vyovyote iwavyo, mwandishi wa makala hiyo anaamini kuna shinikizo kubwa la kisiasa kwa Rais wa Marekani, Joe Biden, ambaye huenda akakabiliana na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump katika uchaguzi ujao wa rais, ambaye anadai Biden ni dhaifu kujibu mashambulizi.
Mwandishi anasema jibu la moja kwa moja la kijeshi la Marekani kwa Iran yenyewe litaleta "janga, kwani litavifanya vita vya Gaza kutanuka, na bila shaka litachochea mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israeli. Linaweza kuamsha mapigano Iraq na Syria na kuvuruga tawala za kirafiki huko Misri, Jordan, na Ghuba, na litazigawanya za Magharibi.
Makala hiyo inamalizia kwa kusema njia salama na ya busara zaidi ni kwa Biden kushughulikia mizizi wa tatizo bila kuchelewa. Biden lazima "ashinikize kusitishwa kwa mashambulio ya Israel huko Gaza, kuwepo usitishaji mapigano utakaopelekea kuachiliwa kwa mateka wa Israel, na kuongoza hatua ya kimataifa ambayo hatimaye itapelekea kupatikana suluhu ya mataifa mawili."
Umuhimu wa nguvu za kijeshi baharini
Tunaligeukia gazeti la Israel la "Maariv," lililochapisha makala ya balozi wa zamani wa Israel nchini Marekani, Zalman Shoval, kuhusu haja ya Israel kutengeneza silaha zake za kivita kwa kuzingatia vitisho vya baharini baada ya mashambulizi ya Wahouthi tangu Novemba katika bahari ya Shamu.
Mwandishi anasema Wahouthi wanahusisha mashambulizi yao, likiwemo shambulio la kombora ambalo hivi karibuni lililenga meli ya mafuta ya Uingereza, na vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza, lakini ukweli, kama mwandishi anavyoona, shambulio dhidi ya meli hiyo ni sehemu ya mashambulizi yaliyoelekezwa na Iran dhidi ya maslahi ya Magharibi, hasa yale ya Marekani na Uingereza, katika Mashariki ya Kati, ambayo pia ni pamoja na mashambulizi yaliyoanzishwa na mashirika ya kigaidi ya Kishia dhidi ya wanajeshi wa Marekani.
Mwandishi anaeleza, "mwitikio wa Marekani kwa mashambulizi hayo hadi sasa umekuwa wa wastani, kulingana na nia ya Marekani ya kuepuka mzozo wa kikanda ambao unaweza kusababisha vita dhidi ya Iran yenyewe. Lakini mauaji ya askari watatu wa Marekani huko Jordan yaliyofanywa na wanamgambo wa kishia yanaweza kubadilisha hilo.''
Mwandishi anasema, “Marekani haijakosea kuhusu kuhusika Iran katika matukio hayo, lakini nia yake katika hatua hii ni kufikia maelewano nayo, ikiwa ni pamoja na suala la nyuklia. Inagwa hilo linaweza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa Warepublican katika Congress.
Anasema mgogoro wa Bahari ya Shamu umesababisha tathmini mpya kwa nchi za Magharibi kuhusiana na umuhimu wa vikosi vya majini hususan nyambizi kuzuia makundi ya kigaidi kama vile Houthis na maadui hatari zaidi.
Anaongeza, "Marekani, Uingereza na Australia, kwa mfano, tayari wamefikia hitimisho la vitendo, kwani nchi hii ya mwisho imetenga mabilioni ya dola katika bajeti yake kwa miongo ijayo ili kukodisha manowari kutoka Marekani."
Anahitimisha kwa kusema, "Israel ni yenye nguvu ya ardhini na angani, lakini haina nguvu ya baharini. Hili lazima libadilike. Jeshi la Israeli linapaswa kununua idadi kubwa ya manowari kuliko ilivyopangwa."
Kuiuwa UNRWA
Tunahitimisha ziara yetu katika gazeti la Al-Ayyam la Palestina kwa makala ya Dkt. Saniya Al-Husseini, binti wa marehemu kiongozi wa Palestina, Faisal Al-Husseini, kuhusu kile anachokiona kama kampeni ya Israel dhidi ya Shirika la Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), kwa madai ya ushiriki wa wafanyakazi wake 12 katika shambulio la Oktoba 7.
Mwandishi wa makala hiyo anasema, "Ingawa uhusiano kati ya Israel na UNRWA haujawa wa kirafiki katika miaka iliyopita, na umekabiliwa na changamoto nyingi huko nyuma, mazingira ya mapigano ya wakati huu yana mwelekeo mpya.
UNRWA ni muhimu kwa Gaza. Shirika hilo lilianzishwa baada ya Nakba ya 1948. Mwandishi wa makala hiyo anasema baada ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Ukombozi na kuliweka suala la Palestina katika majukwaa ya kimataifa, na PLO ikiwa ni harakati ya ukombozi.