Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy akodolea macho bandari ya Bahari Nyekundu, na kuzua hali ya wasiwasi
Na Alex de Waal
Mchambuzi wa Afrika
Kuna fununu zinazomsambaa Ethiopia kuhusu vita vipya - ambavyo vitakuwa vya nne kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed katika kipindi cha miaka mitano.
Pamoja na kuagiza silaha na kuhamasisha jeshi lake, Bw Abiy - ambaye alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2019 kwa kurejesha tena hali ya amani na Eritrea - amekuwa akisema kwamba nchi yake kufikia eneo la bandari ni swala muhimu la 'kufa kupona'.
Lengo kuu la Ethiopia ni bandari ya Bahari Nyekundu ya Eritrea ya Assab, ambayo ilikuwa sehemu ya Ethiopia hadi Eritrea ilipopata uhuru zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Tangu vita vya Ethiopia na Eritrea vya 1998 na kufungwa kwa mpaka kati ya nchi hizo mbili, vifaa katika bandari ya Assab vimekuwa vikiharibika, huku biashara ya Ethiopia ikifanyika katika nchi jirani ya Djibouti.
Taratibu zote za kibiashara na uchumi Djibouti unaweza kutekelezeka kikamilifu, lakini si eneo la Ethiopia.
Waethiopia wengi - na majirani zao - walitafsiri hilo kumaanisha kwamba waziri mkuu anatishia kutumia nguvu.
Lakini Bw Abiy anakanusha hadharani kwamba ana nia ya kuivamia Eritrea, akiwaambia wanajeshi hivi majuzi siku ya jeshi: "Ethiopia haijawahi kuivamia nchi yoyote na haitafanya hivyo katika siku zijazo."
Pia ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kupitia mkutano wa dharura wa muungano wa kikanda wa (Igad), jumuiya ya mataifa manane ya kaskazini-mashariki mwa Afrika.
Hata hivyo kujihai vikali kwa Ethiopia na na msimamo wake mkali kuhusu suala la bandari lina matokeo.
Mnamo Julai, Bw Abiy aliibua hadharani swali la Ethiopia kufikia baharini.
Alisisitiza kuwa Ethiopia ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi isiyo na bahari - ina watu milioni 125 - na kwamba upatikanaji wa bahari ulikuwa kipaumbele cha juu kwa wafalme wa Ethiopia, hasa Haile Selassie ambaye alitawala kutoka 1930 hadi 1974.
Akimnukuu jenerali maarufu wa Karne ya 19, Ras Alula, Bw Abiy alisema kuwa Bahari Nyekundu ulikuwa mpaka wa asili wa Ethiopia .
Inasemekana aliuambia mkutano wa wafanyabiashara kwamba "tunataka kupata bandari kwa njia ya amani. Lakini kama hilo litashindikana tutatumia nguvu ".
Wengine waliona hii kama njia ya kupata uungwaji mkono wa kisiasa nyumbani.
Kauli hiyo huenda iliwafuruhahisha watu wenye ushawishi kutoka kabila la Amhara ambao wanatetea Ethiopia kubwa zaidi.
Bw Abiy alitenga kundi hili alipofanya amani na Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) kaskazini mwa Ethiopia mwaka mmoja uliopita, kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha umwagaji damu.
Alizidi kuwachukiza kwa kuanzisha operesheni ya kijeshi mwezi Aprili ili kuwapokonya silaha wanamgambo wa Amhara, ambao walishirikiana naye katika mzozo katika eneo la Tigray.
Waethiopia wengi pia wanaamini, kwa kupotoshwa , kwamba sheria ya kimataifa inaipa nchi kubwa haki ya kuwa na bandari.
Tafsiri nyingine ni kwamba Bw Abiy anahangaishwa na urithi wake, na anaona kupata bandari, kwa nguvu ikiwa haiwezi kufanywa kwa mazungumzo, kama mchango wake kwa ukuu wa Ethiopia.
Kwa miongo kadhaa, sera ya kigeni ya Ethiopia ilitabirika. Ilitaka kuleta utulivu katika Pembe ya Afrika chini ya uongozi wake yenyewe.
Sehemu ya haya ilikuwa ikishirikiana na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika juhudi za amani nchini Sudan na Somalia. Ethiopia imekuwa mchangiaji mkubwa wa Afrika katika misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Sehemu nyingine ilikuwa miradi kabambe ya miundombinu ya mipakani, ikiwa ni pamoja na njia za usafiri na njia za umeme.
Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance kwenye Mto Nile lilibuniwa kuzalisha umeme wa kutosha ambao ungeweza kuuzwa nje kwa nchi jirani. Wazo lilikuwa kuifunga Pembe ya Afrika pamoja kama kambi moja ya kiuchumi.
Leo, Bw Abiy amepata sifa ya kutotabirika. Ndivyo ilivyo kwa mambo ya ndani na nje ya nchi.
Katika mabadiliko ya kustaajabisha, Eritrea, ambayo wakati mmoja iliepukwa sana kwa kuyumbisha Pembe ya Afrika, inajiweka kama taifa linalowajibika, na kutetea hali iliyopo sasa .
Kumjibu Bw Abiy, kauli zake zimekuwa za ukali na za uchungu, na kukataa kabisa kujiunga na "mijadala" ya mshirika wake wa zamani kuhusu suala ambalo "limewashangaza waangalizi wote wanaohusika ".
Majirani wengine wa Ethiopia wamekumbw ana wasi wasi pia, na Djibouti, Jamhuri ya Somaliland-iliyojitangazia uhuru kutoka Somalia na Kenya zinaungana na Eritrea katika kambi isiyo rasmi ili kuidhibiti Ethiopia - zikitoa taarifa zinazoelezea wasiwasi wa kila mmoja.
Nchi za Mashariki ya Kati zipo katika njia panda. Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ni mlezi mkuu wa Bw Abiy - kinachoonekana zaidi ni kufadhili jumba lake la kifahari, pamoja na kutoa ndege zisizo na rubani.
Ndege za Imarati zimeshuhudiwa zikishusha mizigo katika vituo vya ndege vya Ethiopia katika siku za hivi karibuni.
Abu Dhabi pia inaunga mkono kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) la Sudan linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagolo, anayejulikana kama "Hemeti", ambaye anadhibiti sehemu kubwa ya Sudan ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya mji mkuu wake, Khartoum, na hivi karibuni anaweza kuunda serikali.
Kwa UAE, ubabe wa Bw Abiy ni fursa na pia ni hatari: Ethiopia inaweza kuwa nguvu muhimu ya Bahari Nyekundu - na 'nchi mtej' ama inayotumiwa na Imarati; au vita vipya katika Pembe hii vinaweza kuhatarisha mafanikio yao nchini Sudan.
Saudi Arabia, kwa upande mwingine, inafadhili mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Sudan kwa pamoja na Marekani na inaripotiwa kusikitishwa na jinsi Ethiopia ya Bw Abiy inavyojitayarisha kwa mzozo mwingine.
Iwapo Bw Abiy atavuka mipaka, Saudi Arabia inaweza kuamua kumuunga mkono Rais wa Eritrea Isaias Afewerki liha yakuwa na mashaka naye .
Ikiwa yuko makini kuhusu vita vipya, Bw Abiy anakabiliwa na changamoto mbili kuu. Moja ni nani atapigana.
Jeshi la Ethiopia limepunguzwa nguvu na vita vitatu vilivyopita. Kwanza ilikuwa vita dhidi ya Jeshi la Ukombozi la Oromo, na bado havijaisha.
Vita vya pili, dhidi ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), vilipiganwa kwa ushirikiano na Eritrea, na vilimalizika kwa kusitishwa kwa mapigano mwaka mmoja uliopita. Jeshi la Ethiopia lilipoteza, kwa hesabu yake yenyewe, kati ya wanajeshi 260,000 na 520,000 waliouawa au kutoweka kazini, pamoja na 374,000 waliojeruhiwa.
Vita vya tatu, dhidi ya wanamgambo wa Amhara, vilianza mwezi Aprili na vinadhoofisha sehemu kubwa ya jeshi katika kile kinachozidi kuonekana kama hali ya kutoshana nguvu - na ripoti kwamba Eritrea inawapa silaha wanamgambo wa Amhara, wanaojulikana kama Fano pia zinafanya hali kuwa tete zaidi .
Ikiwa Addis Ababa itaingia vitani, pengine itahitaji ushiriki kamili wa Tigray, inayopakana kwa njia ya kimkkakati na Eritrea.
Lakini uchumi na huduma za Tigray ziliharibiwa katika vita vya miaka miwili vilivyomalizika mwaka jana, na watu wake wamechoka.
Wachache wana hamu ya mapigano mapya. Lakini kuna hasira kali na iliyoenea kwa ukatili uliofanywa na jeshi la Eritrea.
Zaidi ya hayo, ikiwa jeshi la shirikisho lingeanzisha vita na Eritrea, Tigray bila shaka itakokotwa ndani ya mzozo huo.
Baadhi ya watu wa Tigray, wakihofia kwamba vita vipya haviepukiki, wanahoji kwamba Tigray inapaswa kuweka masharti yake kwanza, kama vile kurejeshewa kwa Tigray magharibi - iliyotekwa na eneo jirani la Amhara miaka mitatu iliyopita - na kudhibiti baadhi ya mali za kijeshi za kitaifa kama vile ndege.
Changamoto ya pili ni kulipia vita. Uchumi wa Ethiopia uko katika hali mbaya, na unahitaji sana uokozi kutoka kwa wafadhili wa nchi za magharibi pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.
Bw Abiy anaweza kutumaini kwamba UAE itafidia pesa zozote zilizopotea, lakini ingawaje Rais wa UAE Mohamed bin Zayed al-Nahyan anaweza kutoa pesa taslimu kwa waziri mkuu, pesa zake haziwezi kufidia hasara kubwa ya kiuchumi ambayo inaweza kusababishwa na vita. .
Iwe Ethiopia itaanzisha uvamizi au la, Bw Abiy amefanya vita kuweza kufikirika sasa.
Milio ya ngomza vita kumetengeza mazingira hatari. Mashindano ya silaha katika eneo hilo yanazidi kushika kasi. Ethiopia inanunua silaha zaidi. Eritrea na Djibouti huenda zikafuata mkondo huo. Uondoaji silaha mikononi mwa wapiganaji wa Tigray umesitishwa. Mizozo nchini Somalia inaweza kuwa mibaya zaidi. Eritrea inaweza kumwaga silaha kwa wanamgambo wa Amhara ili kuzidisha vita hivyo.
Kuna hatari kwamba tukio lolote dogo linaweza kuwasha moto.
Kitu cha mwisho ambacho Pembe ya Afrika inahitaji ni vita vipya. Lakini hatari sasa ni kubwa sana.
Alex de Waal ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa Amani Ulimwenguni katika Shule ya Sheria na Diplomasia ya Fletcher katika Chuo Kikuu cha Tufts nchini Marekani.