Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Siku 10 zilizoitikisa Mashariki ya Kati' – gazeti la Washington Post
Tunafuatilia hisia za kimataifa juu ya matukio ya hivi karibuni nchini Syria, ambayo yalipelekea kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.
Tunaanza ziara yetu na makala katika gazeti la Marekani la Washington Post na mwandishi Max Boot, yenye kichwa "Siku Kumi Zilizotikisa Mashariki ya Kati. "
Mwandishi anaamini "matukio ya hivi karibuni nchini Syria yanaonyesha jinsi historia isivyotabirika unapotazama wakati wa sasa na sio zamani."
Mwandishi anajadili jinsi vita vya Syria, vilivyoanza mwaka 2011, vilionekana ni kama "mzozo uliopoa," huku Bashar al-Assad akionekana kushikilia madaraka.
Mwandishi anahusisha kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad na "kutotumia nguvu ya uingiliaji kati iliyotolewa na Urusi na Iran kupanua nguvu zake, kuunga mkono mamlaka yake, au kuwajibu wapinzani wake."
Mwandishi anazungumzia tabia ya Bashar al-Assad na upinzani wa Syria, akisema "wakati al-Assad akiendelea kutawala kwa njia ya ugaidi, kiongozi wa Hay'at Tahrir al-Sham alikuwa na shughuli nyingi za kulibadilisha kundi lake kutoka kutokuwa na ushirika na al-Qaeda hadi kuwa kundi pana la Kiislamu lenye uwezo wa kupata uungwaji mkono wa Wasyria wenye msimamo wa wastani.
Anasema, "Al-Assad hajafanya lolote kupata uungwaji mkono kutoka kwa watu wengi, lakini Al-Julani, akitokea katika mizizi ya Uislamu wenye msimamo mkali, amepata mafanikio ya kushangaza.
Mwandishi anaeleza juu ya athari za vita vya Ukraine na vita vya Israel na Hamas na uwezo wa Urusi na Iran kutoa msaada kwa utawala wa Syria.
Kwa kumalizia, mwandishi anabainisha kuwa Syria inaweza kukabiliwa na changamoto mpya baada ya kuanguka kwa Assad, kama vile migogoro kati ya makundi ya wanamapinduzi, huku ujuzi wa kisiasa wa Al-Julani ukiwa katika changamoto kubwa kujaribu kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, na kujaribu kuepusha migongano na vikundi vya Wakurdi.
Mwandishi anatarajia Syria hawatamtoa "dikteta mmoja na kumuweka dikteta mwingine."
Kuanguka kwa Assad: Ujumbe kwa wale wanaoitegemea Iran na Urusi
Makala yenye kichwa cha habari, "Anguko la Assad: Ujumbe kwa Wale Wanaoitegemea Iran na Urusi," katika gazeti la Jerusalem Post, na mwandishi Judah Waxelbaum.
Mwandishi anaanza makala yake kwa kuangazia mabadiliko ya kijiografia yanayoweza kutokea baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria, na "jinsi Syria na Ulimwengu ulivyojibu na ikiwa anguko hilo litaamua muongo ujao wa migogoro ya kimataifa."
Mwandishi anauliza: "Anguko hili linamaanisha nini kwa uwezo wa Urusi na Iran?" Akibainisha kuwa "nchi hizo mbili hazikufanya lolote kumwokoa Assad."
Mwandishi anaamini "kuporomoka kwa utawala wa Syria kutapelekea Iran kupoteza uhusiano na Hezbollah, na Iran haiko katika nafasi ya kukabiliana na Israel moja kwa moja," akitoa wito kwa Israel kuchukua fursa ya hali hii.
"Israel inaweza kutumia fursa hiyo kwa kujiimarisha katika Miinuko ya Golan na kuhakikisha kuwa njia zote za kaskazini hadi Lebanon zinazuiwa.
Kuhusu Urusi, mwandishi anadokeza kwamba "vita vya Ukraine vimemaliza rasilimali zake, kwani Urusi imepoteza zaidi ya wanajeshi 600,000 nchini Ukraine.
Mwandishi anatarajia kwamba "vitega uchumi vya Urusi nchini Libya na kote Afrika ya Kati vitalengwa ikiwa Urusi haitaweza kutetea shughuli zake katika Mashariki ya Kati."
Anaamini kuwa Marekani inaweza kuiunga mkono Ukraine zaidi, kwani hilo litaidhoofisha Urusi katika kiwango cha kimataifa, na hivyo kuathiri miungano yake katika eneo hilo.
Mwandishi anaongeza kuwa "kuifadhili Ukraine dhidi ya Urusi ni bora kuliko kupigana nayo moja kwa moja na Marekani, na ni kwa maslahi ya Marekani kwamba washirika wa kimataifa wa Urusi wanadondoka."
Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kusema, "Israel na Marekani zinaweza kutuma ujumbe kwa kila mtu anayesimama chini ya mwavuli wa Iran-Urusi, kwamba nchi hizo si marafiki zako na hazitakuokoa ikiwa utazipinga nchi zetu."
Mwandishi anatoa wito wa kuongezwa uungwaji mkono kwa vikosi vya Wakurdi kaskazini mwa Syria kama hatua ya kukabiliana na makundi yenye itikadi kali kama vile Hay'at Tahrir al-Sha
Matumaini yenye misukosuko na halitete nchini Syria
Tunageukia tahariri ya gazeti la Uingereza The Guardian, yenye kichwa ,"Mtazamo wa The Guardian juu ya kuanguka kwa Assad: Tumaini lenye misukosuko na dhaifu nchini Syria."
Jukwaa la wahariri wa gazeti hilo linaangazia madhara ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria, ambako kumekuja ghafla na haraka.
Taifa lililoingia katika ukatili na hofu na utawala wa kimabavu - litageuka kuwa nguvu moja katika kujenga taifa jipya, au ni utangulizi wa migawanyiko zaidi?
The Guardian linaonya tawala za kidikteta duniani, kwamba "Anguko la Assad linapaswa kuwa onyo kwa tawala za kidikteta, kwa sababu jamii haziwezi kuvumilia ukiukwaji wa utaratibu, kama vile propaganda zinazofadhiliwa na serikali, rushwa na vurugu."
Bodi ya tahariri inajadili mustakabali wa Syria baada ya kuanguka kwa Assad, na kiongozi Abu Muhammad al-Julani wa Hay'at Tahrir al-Sham, baada ya kubadilisha mienendo kutoka kuwa kikundi cha jihadi hadi kundi la Kiislamu lenye msimamo wa wastani linalotaka kujenga uhalali wa kitaifa.
Gazeti hilo linaonyesha uwezekano wa Ufalme wa Saudi Arabia na Falme za Kiarabu, kusaidia kwa rasilimali zao za kifedha, katika ujenzi wa Syria.
Mwishoni mwa tahariri, gazeti hilo linasisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja za kimataifa kuelekea utulivu wa kisiasa, maridhiano na ujenzi wa Syria mpya na kuhakikisha kwamba mapambano yao yanaleta amani ya kudumu.
Watu wa Syria ambao kwa muda mrefu wamekumbwa na dhulma, hawatakiwi tena kuachwa wakabiliane na hatima yao peke yao, na matumaini ya kujenga mustakbali mwema lazima yaungwe mkono kikamilifu na jumuiya ya kimataifa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla