Wasiwasi waibuka Trump kukifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi Marekani

,

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 5

Na Sammy Awami

Wakati Kiingereza kimekuwa lugha rasmi nchini Tanzania, Kenya na Uganda kwa zaidi ya miaka 60 sasa, nchini Marekani, ni tarehe 1 Machi tu ndio lugha hiyo ilifanywa kuwa rasmi.

Hiyo ni baada ya Rais Donald Trump kusaini amri ya rais (executive order) inayoipa Kiingereza hadhi ya kuwa lugha rasmi ya taifa hilo ambalo karibu shughuli zake zote za kiofisi na kijamii hufanywa kwa lugha ya Kiingereza.

Marekani ndilo taifa linaloongoza duniani kuwa na wazungumzaji wengi zaidi wa lugha hiyo. Kati ya wazungumzaji bilioni 1.52 wa lugha ya Kiingereza duniani, karibu robo (19.74%) wapo Marekani, mara tano zaidi ya Waingereza wenyewe kutoka Uingereza (milioni 60) wanaoshika nafasi ya pili na Canada (milioni 29) wanaoshika nafasi ya tatu.

Unaweza kujiuliza ni kwanini taifa hili ambalo ndilo linaongoza duniani kuwa na wazungumzaji wengi zaidi wa Kiingereza, haikuifanya lugha hiyo kuwa rasmi kwa miaka yote ya uhai wa taifa hilo?

Lakini ipo sababu ya kukifanya sasa kuwa lugha rasmi.

"Kufanya Kiingereza kuwa lugha rasmi kutawezesha mawasiliano kuwa rahisi zaidi, kuimarisha maadili ya pamoja ya kitaifa, na kuunda jamii iliyo na mshikamano na ufanisi zaidi" ilisema sehemu ya amri ya Raisi

Pia unaweza kusoma:
t

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump

Inakadiriwa Marekani kuna ligha zaidi ya 350 tofauti na Kiingereza zinazozungumzwa. Hii ni pamoja na lugha zaidi ya 160 zinazozungumzwa na Wamarekani wa asili. Pamoja na lugha hizo, takribani 80% ya Wamarekani wanazungumza Kiingereza.

Lakini mjadala wa ikiwa Kiingereza kifanywe lugha rasmi au lah umekuwepo kwa miongo mingi, huku mvutano ukiwa juu ya uhalali wa hatua hiyo katika taifa ambalo takribani wananchi milioni 68 wanazungumza lugha tofauti na Kiingereza.

Hata hivyo Trump amekuwa mkosoaji mkubwa wa matumizi ya lugha zingine, hasa katika mazungumzo rasmi.

"Hili ni jambo la ajabu kabisa – wanazungumza lugha ambazo hakuna mtu yeyote katika nchi hii aliyewahi kusikia. Ni jambo baya sana" alisema Trump katika moja ya mikutano yake ya hadhara

Wakosoaji nchini Marekani wamefananisha hatua hii ya kukifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi ni kama muhuri wa kauli mbiu ya Trump ya "Marekani Kwanza" inayoonekana kubagua watu na jamii zinazozungumza lugha zingine

Kwa mfano, mara baada ya kuingia madarakani – katika awamu ya kwanza na ya pili - serikali ya Trump iliishusha tovuti ya Ikulu ya Whitehouse ambayo imeandikwa kwa lugha ya Kihispaniora.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moja ya mabango yaliyopata umaarufu nchini Marekani likisomeka "Nataka kuongea kiingereza" kwenye moja ya fukwe huko South Caolina, Septemba 13, 2018, kama ishara ya kubeza wanaopigania zaidi kiingereza.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kispanyola ni lugha ya pili inayozungumzwa zaidi Marekani, huku pakiwa na watu zaidi ya milioni 43 wenye umri wa miaka kati ya 5 na zaidi wakizungumza lugha hiyo nyumbani.

Wakati Trump amedai kwamba amri yake inaendana na waanzilishi wa taifa hilo walioandika katiba na nyaraka zingine muhimu kwa lugha ya Kiingereza.

Hata hivyo, wanahistoria wanakumbusha kwamba baada ya kuandikwa kwa Kiingereza, nyaraka hizo muhimu zilitafsiriwa pia kwa lugha ya kiholanzi kwa wazungumzaji wake wengi waliokuwa wakiishi New York na kwa Kijerumani pia kwa wazungumzaji waliokuwa wakiishi jimbo la Pennsylvania.

Amri hii ya kukifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi ya Marekani, kutaidhoofidha amri iliyowekwa na Rais mstaafu Bill Clinton kwamba taasisi zote zinazopokea fedha za umma kutoa tafsiri za nyaraka zake katika lugha zinazofaa au kuhitajika na watumiaji wake.

Tayari ni kawaida kwa wageni kushambuliwa kwa maneno pale wanapozungumza lugha zao za asili maeneo ya umma kama vile katika njia za usafiri, sokoni au taasisi za elimu.

Baada ya amri hii, kuna wasiwasi wa kuongezeka kwa ubaguzi na unyanyasaji kwa Wamarekani wageni ambao aidha hawajamudu kuzungumza vizuri Kiingereza au wanazungumza kwa rafudhi za lugha zao za asili.

Lugha kuwa ramsi kunamaanisha nini?

G

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Moja ya eneo la uwanja wa ndege huko Winston Marekani likiandikwa kwa kiingereza kuonyesha kuwa ni maalumu kwa ajili ya kuvutia sigara

Lugha rasmi ni lugha iliyopewa hadhi maalumu katika nchi fulani, ili kutumika kwenye mawasiliano ya shughuli zote rasmi za serikali.

Kuwa rasmi maana yake ni kutumika kwa mfano kwenye mawasiliano yote kati ya ofisi zake na pia kutumika kwenye matangazo rasmi, kwa mfano kwa kutangaza sheria, sera, kutoa waraka wa Rais, hotuba na mijadala bungeni. Ni pia lugha ya kuendesha kesi mahakamani na pamoja na kutumika kuandika hukumu.

Nchi nyingi hasa zilizotawaliwa na wakoloni, zinatumia lugha ya asili ama za asili na lugha ya kigeni hasa ya waliowatawala kama lugha rasmi. Tanzania na Kenya zinatumia Kiswahili na kiingereza kama lugha rasmi.

Kwa mfano huwezi kuendesha kesi na kuandika hukumu kwa lugha ya kisukuma au kichaga nchini Tanzania, kwa kuwa lugha hizo si rasmi. Kitatumika kiswahili au kiingereza kama ilivyo Kenya, kwa kuwa ndizo lugha zilizopewa hadhi hiyo.

Lugha kuwa rasmi kunaweza kuwekwa kwenye katiba au sheria, kwa lengo ya kuitambua au isiwekwe huko lakini ikatolewa waraka wa rais kama ilivyofanya Marekani sasa. Japo shughuli zake nyingi zimekuwa ikitumia kiingereza, kwa waraka wa Machi 1, sasa imekuwa rasmi Marekani.

Kwa nini Kiingereza hakikuwa lugha rasmi Marekani?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiingereza kinafundishwa karibu katika shule zote nchini Marekani, huku katika Vyuo Vikuu, hii imekuwa lugha rasmi ya kufundishia kwa miaka mingi

Marekani haikuwa na lugha rasmi kwa karibu miaka 250 tangu nchi hiyo ilipoanzishwa. Lakini kiingereza kilikuwa kinatumika zaidi kuliko lugha zingine nchini humo.

Wasomi wanasema kwamba wakati Marekani ilipoanzishwa, watu wengi walizungumza Kiingereza na wale walioandika katiba ya nchi hiyo hawakuona ulazima wa kukifanya Kiimgereza kuwa lugha rasmi. Lakini pia, hawakutaka kuwatenga raia waliokuwa wakizungumza lugha nyingine.

Pamoja na jituhada kadhaa wakati huo za kukifanya kuwa lugha rasmi, waanzilishi wa taifa hilo hawakuona haja ya kutangaza lugha moja kuwa rasmi kama alivyowahi iambia na CNN mwaka 2018, Dk. Wayne Wright, profesa katika Chuo Kikuu cha Purdue

Profesa huyu alisema kwamba hawakufanya hivyo ili kutowakosea Wamarekani wengine waliokuwa wamesaidia kupigania uhuru wa taifa hilo. Wakaona hakukuwa na haja ya kukilinda Kiingereza wala kukifanya lugha rasmi ya nchi hiyo.

Duniani kote nchi zaidi ya 180 zina lugha rasmi, huku baadhi ya nchi zikitambua lugha zaidi ya moja kuwa lugha rasmi. Afrika ya Kusini, kwa mfano, ina lugha rasmi 11 huku Rwanda ikiwa na lugha rasmi nne ambazo ni Kinyarwanda, Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili.

Tanzania na Kenya wanatumia Kiingereza na Kiswahili kama lugha rasmi, huku kuna baadhi ya nchi – kama Uingereza na Eritrea zenyewe mpaka leo hazina lugha rasmi. Wakati Marekani imeamua sasa kiingereza kuwa lugha rasmi, mjadala unaendele kwa miaka mingi nchini Uingereza, nchi yenye asili ya lugha hiyo namba moja duniani na yenye kushika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na wazungumzaji wengi wa kiingereza. Je na yenyewe itafuata?