Kwa nini Simba SC ya Tanzania imeshinda kwa 'kufungwa' Zanzibar?

Chanzo cha picha, BZ
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
'Tumeshinda lakini sijafurahia', mmoja wa mashabiki wa Simba SC ya Tanzania, baada ya kipyenga cha mwisho cha mchezo wao dhidi ya Stellenbosch FC katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho CAF.
Na ndipo tunapoanzia: Simba SC imeshinda bao 1-0 dhidi ya timu hiyo ya Afrika Kusini. Lakini kwa mashabiki wengi wa soka, huu ni ushindi wenye ladha ya kushindwa. Ushindi ambao unaficha udhaifu kuliko kuonyesha ubabe.
Wengi walikuwa na matarajio makubwa zaidi. Kupatikana kwa ushindi mkubwa zaidi. Katika mechi iliyochezwa Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, Simba walikuwa nyumbani. Walikuwa na uzoefu mkubwa zaidi, walikuwa na historia.
Stellenbosch walikuwa wageni, wachanga, na kwa mara ya kwanza wanashiriki michuano ya Afrika. Lakini dakika 90 zilisema vingine: Simba walishinda na ni kitu kizuri katika michuano hii mikubwa na hatua hii kubwa ya nusu fainali , lakini mashabiki hawana furaha.
Ukongwe dhidi ya Ugeni
Kwa miaka sasa, Simba SC imekuwa moja ya timu tishio Afrika. Nafasi ya 4 inayoshika sasa kwa uborwa Afrika kwa viwango vya CAF haiji kwa bahati. Mashabiki wa Simba wamezoea kuiona timu yao ikicheza na kutawala robo fainali za CAF, wakipambana na wakongwe kama Al Ahly na TP Mazembe.
Stellenbosch, kwa upande mwingine, ni timu iliyoanzishwa mwaka 2016, na huu ndiyo msimu wake wa kwanza kabisa kucheza michuano ya CAF. Ni wageni na ilitarajiwa Simba wataonyesha tofauti hiyo kubwa ya uzoefu.
Lakini ndani ya uwanja, tofauti hiyo haikuonekana sana. Stellenbosch walionekana kuwa na mpangilio, walicheza kwa nidhamu, na walikuwa na mwelekeo wa kujilinda na kushambulia kwa akili. Kwa kipindi chote cha kwanza, walikaba kwa nidhamu na walitengeneza presha isiyotarajiwa kwa Simba.
Kama timu yenye uzoefu haikuweza kudhihirisha ukubwa wake dhidi ya timu mpya. Kwa maana ya kutawala mchezo, simba ilifanya hivyo,
Ubabe wa nyumbani kwa Mkapa haukuonekana sana Zanzibar

Chanzo cha picha, Simba
Simba walikuwa wenyeji wa mechi, na mara zote hutumia Uwanja wa Benjamini Mkapa. Uwanja huu umewapa matokeo ya zaidi ya asilimia 90% katika mechi 11 zilizopita. Lakini waliamua kuhamia Zanzibar kwa sababu maboresho ya uwanja huu. Uwanja wa kisasa wa Amaan ulijaa mashabiki, wengi wao wa upande wa Simba, waliokuja kushuhudia karamu ya mabao. Lakini waliondoka na mshangao kiasi, ushindi kiduchu.
Bao pekee la Simba lilifungwa na Jean Charles Ahoua dakika ya 44, kwa smkwaju wa moja kwa moja lililohusisha utulivu mkubwa. Lakini bao hilo halikuashiria mwanzo wa karamu. Simba hawakuweza kuongeza bao jengine, licha ya mazingira yote kuwapa nafasi.
Kwa timu kubwa Afrika, bao 1-0 nyumbani si kitu cha kusherehekewa sana hasa ikiwa wapinzani ni wageni wa CAF kama Stellenbosch. Ushindi mdogo nyumbani ni mzigo mzito unapokwenda ugenini, hasa dhidi ya timu zinazocheza vizuri mbele ya mashabiki wao.
Jean Charles Ahoua ndiye aliamua matokeo haya

Chanzo cha picha, Simba
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mchango wa Jean Charles Ahoua hauwezi kubezwa tangu ajiunge na Simba. Ndiye aliyewapa Simba bao muhimu Simba pale Zanzibar. Ahoua alionyesha utulivu mkubwa kwa kupiga shuti la chini lililomshinda kipa wa Stellenbosch.
Na hata Simba kufika hatua hii ya nusu fainali kwa mara ya tatu katika historia ya klabu hiyo, raia huyu wa Ivory Coast amekuwa na mchango mkubwa. Toka katika hatua za awali za michuano ya mwaka huu, amefunga mabao matatu na kutoa pasi za mabao 2, katika mechi 9 za CAF. Alifunga katika ushindiwa wa Simba wa bao 10- dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, akafunga tena dhidi ya CS Sfaxien, Simba ikishinda 1-0 ugenini Tunisia na Jumapili hii anafunga bao lingine muhimu dhidi ya Stellenbosch.
Lakini, historia ya mechi ya Jumapili hii haikuishia kwa yeye kufunga bao muhimu lililowapa simba ushindi muhimu wa bao 1-0 Zanzibar. Dakika za lala salama, Ahoua alipata nafasi ya wazi kabisa kufunga bao la pili, alipokea pasi akiwa ndani ya boksi akiwa anaangaliana uso kwa uso na kipa, alimpiga chenga na kubaki na nyavu lakini akapiga shuti nje ya lango kwa mguu wa kushoto.
Kama angefunga, furaha ya mashabiki wa Simba ingejionyesha zaidi kuliko sasa na lingewapa imani ya kutinga fainali kwa mara ya kwanza kwa miongo mingi. Lakini pia lingewavunja matumaini kabida Stellenbosch. Kwa bao hili moja, Waafrika Kusini hawa wana matumiani wakijua bado wana nafasi kubwa ya kusonga mbele.
Ameamua matokeo ya mchezo huu kuwa yalivyo, lakini angewez akuamua vinginevyo zaidi na kuamua sura na hisia za mashabiki wake kuelekea mchezo ujao Afrika Kusini.
"Namuhukumu Ahoua kwa bao alilofunga, sio alilokosa. Amehusika na mabao matano kwenye mechi 9 za kimataifa, kwneye ligi ya ndani mabao yake ndiyo yameiweka Simba kwenye nafasi ya kupambania ubingwa. Ni mchezaji bora wa simba msimu huu', anaandika Geoff Lea , mmoja wa wachambuzi wa mechezo Tanzania
"Mechi ya mkondo wa pili, Simba itacheza kama bingwa wa Afrika"
'Sisi hatuna hofu ya kucheza na timu yoyote sehemu yoyote, tulieni, msipaniki, nimekosa magoli, nmefanya makosa mengi , sahauni hayo, tujielekeze kwenye mchezo ujao, msijitie hofu", alisema Murtaza Mangugu, mwenyekiti wa Simba akizungumza na wachezaji akiwapa moyo mara baada ya mchezo wa kwanza pale Zanzibar.
Lugha ya Mangungu inakuonyesha matarajio yalikuwa tofauti kwa timu hiyo na wachezaji wake. Na ni kitu kizuri kuamini kwenye kupata matokeo makubwa. Na kwa sababu Stellenbosch ilishawahi kupata matokeo ya kushangaza dhidi ya timu kubwa na zenye uzoefu Afrika, ikiwemo Zamalek, unaweza kuwasifu Simba angalau kwa kupata bao.
Ushindi wao wa 1-0 unaweza kuonekana ni matokeo mazuri kuliko kufungwa, lakini katika mashindano ya CAF, si matokeo salama sana. Stellenbosch ni timu yenye rekodi nzuri sana nyumbani. Uwanja wao wa Danie Craven huko Afrika Kusini ni ngome ambayo timu nyingi zinapoteza. Simba wanakwenda kukutana na mazingira tofauti: hewa baridi, mazingira ya uwanda wa juu, na mashabiki wa Afrika Kusini waliojaa hamasa.
Kwa sababu hii, inawapa hofu mashabiki wa Simba, wakiwaza ugumu wa mchezo ujao.
"Mechi ya mkondo wa pili, Simba itacheza kama bingwa wa Afrika", mmoja wa mashabiki wa Simba, Boniface Selemani akiwapa moyo wenzake waliokuwa wakifuatilia mechi kupitia runinga.
Kwa ufupi Simba SC imeshinda nyumbani kwa bao 1, lakini imeshindwa kwa hofu. Hofu ya mashabiki wake kwa mchezo ujao. Je inaweza kufanya kile kinachotarajiwa Jumapili ya April 27, 2025 kule Afrika Kusini na kufuzu fainali ya CAF baada ya miaka 32 tangu mwaka 1993?














