Mzozo wa DRC: 'Nililazimika kubakwa ili kuokoa maisha yangu'

Muda wa kusoma: Dakika 3

Onyo: Makala hii ina maudhui yanayoweza kukuhuzunisha

"Aliniambia kwamba nikijaribu kutoroka, angeniua."

Pascaline, binti mwenye umri wa miaka 22, anakumbuka maneno ya mtu aliyembaka katika gereza la Munzenze, lililopo Goma, mji mkubwa wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika usiku wa kuamkia tarehe 27 Januari.

"Nililazimika kukubali kutendewa hivyo ili kutetea uhai wangu," anasema Pascaline alipokuwa akizungumza na BBC.

Huyo alikuwa mwanamume wa pili kumbaka. Tukio la kwanza lilikuwa na ghasia kiasi kwamba alipoteza mpaka fahamu.

Anasema wahalifu hao walitokea upande wa gereza la wanaume lililoko karibu, linaloitwa "Safina."

"Tuliposikia sauti waliporuka juu ya matanki ya maji, tulihisi hofu kubwa. Walikuja wengi sana. Waaio na bahati walibakwa. Waliokuwa na bahati walitoka bila kubakwa."

Kulikua na vurugu gerezani na katika jiji zima. Wakati huo, waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda walikuwa wakikaribia katika mji wa Goma kwa kasi kubwa.

Walinzi wengi wa gereza na viongozi wa serikali ya mji huo walikuwa tayari wameshakimbia. Risasi zilikuwa zikisikika nje ya jela.

Masaa machache baadaye, ndani ya gereza, moto ulizuka, inaaminika kuwa uliwashwa na wafungwa wa kiume waliokuwa wakijaribu kutoroka.

Asubuhi ilipofika, takribani wafungwa wa kiume 4,000 walikuwa wametoroka. Lakini ni wachache kati ya wanawake walioweza kutoroka. Jumla ya wafungwa wa kike 132 na angalau watoto 25 waliteketea hadi kufa, kwa mujibu wa vyanzo viwili.

Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa aliiambia BBC kwamba "walau wanawake 153 walipoteza maisha," akinukuu vyanzo vya kuaminika kutoka gerezani.

Mwezi mmoja baadaye, Pascaline amerudi katika mabaki ya gereza lililoungua.

"Wakati fulani sikujua tena nini kilikuwa kinaendelea," anasema. "Baada ya kuwaona wengine wakifa, ndipo nikaanza kujipa moyo. Naweza kusema kwamba ilikuwa ni Mungu tu aliyeniokoa."

Pascaline ni muuza vitunguu tu na amejikuta jela baada ya muajiri wake kumtuhumu kuiba.

Kwa upande wa binti mwingine Nadine, naye mwenye umri wa miaka 22, anasema pia alibakwa na wanaume wawili.

Nadine, pia amerudi kwa mara ya kwanza kwenye eneo la gereza. Lakini kiakili, hajawahi kuondoka huko.

"Nikilala usiku, kila kitu nilichoona hapa kinanirudia. Naona maiti tena, miili mingi kama niliyoshuhudia hapa kabla sijatoka. Badala ya kufungua mlango, walituacha tufe kama wanyama hapa."

Wafungwa wa kike wanaruhusiwa kuishi na watoto wao jela. Ni watoto wawili tu kati ya 28 walionusurika katika moto na vhasia hilo. Watoto ambao walikua kwenye jengo lingine tofauti wao walinusurika kwa kuondolewa mapema.

Nadine anasema nae amebakwa na wanaume wawili.

"Walikuja na pombe," anaiambia BBC. "Walitaka kutulewesha. Walinichukua mie kwa nguvu. Walichukua wanawake wote waliokuwepo hapa."

BBC haiwezi kuthibitisha ni wanawake wangapi walibakwa usiku huo, kati ya 167 waliokuwa wakishikiliwa gerezani kulingana na vyanzo vya habari.

Nadine ana hasira na mamlaka za DRC, kwanza kwa kumtupa gerezani kwa deni aliloshindwa kulipa, anavyodai, na pili kwa kushindwa kuwaokoa wasife.

"Sidhani kama kuna haki DRC," anasema. "Ninakemea jinsi serikali inavyoendesha mambo yake."

Serikali ya DRC iliyoko Kinshasa umbali wa zaidi ya kilomita 1,500 haina tena udhibiti wowote katika eneo la Goma. Waasi sasa wanatawala kikamilifu na wanaendelea kusonga mbele katika maeneo mengine ya mashariki mwa nchi.

Mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 38, tunayemwita Florence kwa usalama wake, anasema watoto walianza kufa baada ya polisi kurusha mabomu ya machozi jela katika sehemu ya wanawake.

"Gereza lilizungukwa na wanajeshi na polisi ambao, badala ya kuzima moto, walikuwa wakifyatua risasi na kurushia mabomu ya machozi," anasema Florence.

Alisema sehemu ya wanawake ilifunguliwa mwendo wa saa tano asubuhi, lakini hakujua ni nani aliyefungua milango hiyo. Alitoka na wanawake wengine 18 waliokuwa wamenusurika.

"Hata polisi tuliowakuta barabarani hawakuuliza habari zozote kuhusu wafungwa, wala kuuliza kama kuna waliojeruhiwa au walihitaji msaada," anasema.

Kwa wakati huo, waasi walikuwa tayari wameingia sehemu za jiji na eneo la karibu na gereza wakiwa wameanza kuingia kuanzia saa mbili asubuhi. Mji wa Goma ulikuwa ukielekea kutekwa na waasi hao.

Katika hema lililo katika uwanja wa hospitali ya Goma, tunakutana na Sifa, mwenye umri wa miaka 25, aliyenusurika kwa kuokolewa kutoka kwenye moto na rafiki yake.

Binti yake Esther, mwenye umri wa miaka miwili, alifariki katika gereza.

"Nilikuwa na Esther mgongoni mwangu. Tulipotaka kutoroka, kitu fulani kilimuangukia. Bomu? Sijui ni nini. Alikufa papo hapo," Sifa anaiambia BBC.

Sifa alifungwa kwa tuhuma za wizi, ambazo anazikana.

Sifa na wanawake wengine walionusurika wanasema hakuna yeyote aliyewasiliana nao ili kuchukua maelezo na ushuhuda wao juu ya mkasa wa tarehe 27 Januari, si waasi walioko madarakani Goma sasa, wala serikali ya Kinshasa iliyokuwa ikiendesha gereza hilo.

*"Hakuna mtu atakayefuatilia kesi hii," anasema Sifa. "Hakuna mtu atakayewajibishwa. Tayari limeshapita hili."

Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi