Shambulio la droni dhidi ya Israel lafichua udhaifu wa Iron Dome

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Jonah Fisher
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Northern Israel
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Zinatembea polepole, ndogo na za bei nafuu katika kutengeneza, ndege zisizo na rubani zimekuwa zikiiumiza kichwa Israel katika vita hivi vya mwaka mzima.
Shambulio la Hezbollah kwenye kambi ya jeshi huko Binyamina kaskazini mwa Israel siku ya Jumapili, liliua wanajeshi wanne na kujeruhi makumi ya wengine, lilikuwa shambulio baya zaidi la ndege zisizo na rubani nchini humo hadi sasa.
Shambulio hilo limesababisha maswali mapya kuhusu jinsi mfumo wa ulinzi wa anga wa bei ghali wa Israel ulivyoshindwa kuzuia droni.
Alipotembelea kambi ya jeshi iliyoshambuliwa siku ya Jumatatu asubuhi, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant alisema "juhudi kubwa" zinafanyika ili kuzuia mashambulizi ya baadaye ya ndege zisizo na rubani.
Mfumo wa ulinzi wa anga hufanya kazi vizuri dhidi ya makombora. Kaskazini mwa Israel tunasikia milipuko ya mara kwa mara huku Iron Dome ikizuia makombora ambayo Hezbollah inarusha kutoka kusini mwa Lebanon. Israel inasema huzuia zaidi ya 90% ya mashambulizi.
Iron Dome inafanya kazi vizuri dhidi ya roketi za Hezbollah kwa sababu inawezekana kukokotoa wapi roketi zitatokea na kisha kuzizuia.
Kuzuia droni ni changamoto
Lakini kuzuia droni ni kazi ngumu zaidi. Na katika vita hivi hilo limekuwa tatizo la mara kwa mara.
Mwezi Julai ndege isiyo na rubani iliyorushwa na Wahouthi wa Yemen ilifika Tel Aviv. Mapema mwezi Oktoba Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema ndege isiyo na rubani iliyorushwa kutoka Iraq iliua wanajeshi wawili katika eneo la Golan Heights. Wiki iliyopita tu ndege nyingine isiyo na rubani ilipiga nyumba ya wazee katikati mwa Israel.
"Ndege nyingi, ikiwa sio zote, zinatengenezwa na Iran na kisha hutolewa kwa vikundi vyenye silaha huko Lebanon, Iraq na Yemen," anasema Dk Yehoshua Kalisky, mtafiti mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama wa Taifa huko Tel Aviv. .
Ndege zisizo na rubani zina rada ndogo na zinaweza kupaa chini chini - jambo ambalo hufanya kugunduliwa mapema kuwa kugumu. Zinaweza hata kudhaniwa ni ndege (mnyama).
"Pia ni vigumu kuzizuia kwa sababu huruka polepole," anaeleza Dk Kalisky. "Zinatembea kwa takribani kilomita 200 kwa saaa (124mph) ikilinganishwa na kilomita 900 kwa saa (559mph) kasi ya ndege ya kivita.”
Shambulio la Jumapili

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zinaonyesha kuwa siku ya Jumapili ndege mbili zisizo na rubani za Hezbollah, aina ya Ziyad 107, zilivuka kuingia Israel kutoka anga ya Lebanon juu ya bahari ya Mediterania.
Mmoja ilidunguliwa na nyingine ikatoweka - ikidhaniwa kuwa ilianguka - kwa hivyo hakuna king'ora cha onyo kilicholia. Na ikaenda kushambulia kantini ya kambi ya jeshi.
Sarit Zehani kutoka Taasisi ya Utafiti ya Alma - ambayo inajishughulisha na masuala ya usalama kwenye mpaka wa kaskazini – hafikirii kuwa ilikuwa bahati kwamba droni imepenya.
“Ilipangwa,” anasema.
Bi Zehani anaishi kilomita 9 kutoka mpaka wa Lebanon magharibi mwa Galilaya na aliona tukio la Jumapili kupitia roshani ya nyumba yake. Anasema kulikuwa na roketi zilizorushwa na arifa ikatolewa katika eneo lote la mpaka wakati ndege zisizo na rubani zikirushwa, mfumo wa anga ulizidiwa na kufanya droni kupita.
Taasisi ya Utafiti ya Alma imehesabu matukio 559 ya ndege zisizo na rubani kuvuka mpaka wa kaskazini kwa ajili ya ufuatiliaji au mashambulizi tangu vita kuanza mwaka mmoja uliopita. Ukiondoa shambulio la Jumapili huko Binyamina, inasema kuna majeruhi 11 kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.
Kuongeza ulinzi wa anga
Mbali na Iron Dome, mifumo ya ulinzia wa anga ya Adam’s Sling, Arrow 2 na Arrow 3 imeundwa kuharibu makombora ya balestiki. Na hivi karibuni mfumo wa ulinzi wa anga utaimarishwa kwa kuwasili mfumo wa Terminal High Altitude Area Defence (Thaad) kutoka Marekani ambao utaendeshwa na karibu wanajeshi 100 wa Marekani.
Mifumo bora zaidi na ya kudumu ya kuangusha ndege zisizo na rubani kwa sasa inabuniwa.
"Ulinzi wa anga wa mionzi yenye nguvu unafanyiwa kazi na teknolojia nyingine ya mizinga ya mawimbi ya frikwensi ili kuharibu vifaa vya kielektroniki vya droni," anasema Dk Kalisky.
Anasema teknolojia hizi "zitapatikana katika siku za usoni."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












